MAAJABU! Mtoto Irene Emmanuel Joseph (1) mkazi wa Kibamba-Mji Mpya jijini Dar, ameendelea kuwa gumzo kufuatia kufariki dunia Agosti, mwaka jana akiwa na miezi 9 na kudaiwa kufufuka katika mazingira ya ajabu hivi karibuni akiwa na umri wa mwaka mmoja na miezi minne.
Tukio la kupatikana kwa mtoto huyo akiwa hai lilitikisa Jiji la Dar, Jumamosi iliyopita ambapo umati ulifika nyumbani kwa wazazi wa mtoto huyo ili kumshuhudia kwa macho.
MAZINGIRA YA KIFO CHAKE
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi nyumbani hapo, mama mzazi wa mtoto huyo, Helena Raphael alisema kuwa, ilikuwa Agosti mwaka jana akiwa kwenye eneo la biashara yake, Mbezi Mwisho, Dar, Irene aliugua ghafla. Alionesha kulegea na kuwa kama mtoto mwenye degedege.
“Nilimwambia mume wangu, tukampeleka kwenye zahanati moja iliyopo palepale Mbezi ambapo daktari akabaini kuwa tatizo la mwanangu ni kubwa hivyo akatushauri tumkimbize Hospitali ya Tumbi, Kibaha, Pwani ambapo iligundulika kwamba alikuwa na upungufu mkubwa wa damu.
“Pale hospitali madaktari walianza kutafuta mishipa ili wamchome kwa lengo la kumwongezea damu lakini cha ajabu mishipa ya mwanangu ikawa inavimba tu. Ilipofika saa 6 usiku, alifariki dunia bila kuwekewa damu. Nililia sana kama mzazi!”
Irene Emmanuel akiwa na baba'ke |
MAITI YAMDUWAZA MAMA MTU
“Baada ya kifo, sikuwahi kuuona mwili wa mwanangu maana waliupeleka mochwari. Siku ya kuaga mwili hapa nyumbani kwa ajili ya mazishi, nilishangaa sana kumwona mwanangu ana alama ya duara kwenye shavu kama zile alama za Wamasai.
“Niliwasimulia baadhi ya waombolezaji wakasema kwa upande wao waliuona mwili wa mwanangu ukitoka jasho jingi kama mtu aliyetoka kufanya kazi ngumu juani na ulivimba sana,” alisimulia mama huyo na kuongeza:
“Pamoja na hayo, tulimzika mwanangu kwenye makaburi yaliyopo hapahapa Mji Mpya huku tukiwa na shaka juu ya kifo chake.”
MAMA AANZA KUZUNGUKA MAKANISANI
Helena anasema baada ya mazishi, alianza kwenda kwenye makanisa mbalimbali kumwomba Mungu amrejeshe mwanaye na mwishowe akajikuta amefika kwenye kanisa la Nabii Flora lililopo Salasala, Dar ambako aliambiwa mtoto wake alikuwa hai.
“Nilikuwa naenda kusali kila siku ndipo siku moja Nabii Flora alinifuata na kuniambia mwanangu hajafa alikuwa yupo sehemu lakini nguvu zake haziwezi kumrudisha tena.
MGANGA ADAI AMEMPATA MTOTO
“Siku ya kwanza kumpigia simu huyo mganga alituambia tushike shilingi mia moja mkononi, tukafanya hivyo, akasema kweli mtoto wetu yupo hai na atamrudisha. Siku chache mbele tulimtumia hela alizotuagiza na akatuambia tusafiri kwenda Dodoma tukamchukue mtoto wetu kwani tayari alishampata.”
WAZAZI WAONANA NA MTOTO
Helena anasema kuwa, Februari mwaka huu yeye na mume wake walisafiri mpaka Dodoma eneo la Pandambili na kuonana na mganga huyo akiwa na mtoto wao ambaye alionekana kutokuwa na afya nzuri. Walitakiwa wamuache kwa muda ili aendelee na matibabu mpaka arejee kwenye hali ya kawaida.
MGANGA ATINGA DAR NA MTOTO
“Baada ya miezi miwili kupita mganga alitutaarifu kuwa anakuja Dar na mtoto. Kweli, alifika hapa usiku wa Aprili 10 akiwa na mtoto wetu ambaye kwa sasa ni mzima kabisa.
“Tuna furaha sana kuonana na mwanetu tena haya kweli ni maajabu ndiyo maana watu wengi wamefika hapa kushuhudia na wengine wamelala hapahapa tangu jana,” alisema mama huyo.
MGANGA ANENA
Naye mganga aliyedai kumfufua mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina la Bino alikiri kupokea simu kutoka kwa wazazi hao na kusema:
“Niliongea na mizimu ikaniambia mtoto yupo hai katika mazingira ya kawaida ila alichezewa kimazingara. Nimewasaidia wengi tu na ninao watu wengi niliowarudisha huko Dodoma,” alisema mganga huyo.
MJUMBE ATHIBITISHA KUZIKWA KWA MTOTO HUYO
Mjumbe wa mtaa huo, Maimuna Abdallah alithibitisha kupokea taarifa ya kifo cha mtoto Irene, Agosti mwaka jana na kuongeza kuwa yeye ndiye aliyetoa barua ya utambulisho wa makazi kwa baba mzazi wa mtoto huyo ili aweze kupatiwa mwili wa mwanaye kutoka Hospitali ya Tumbi kwa ajili ya mazishi.
“Na mimi nimeshangazwa sana na tukio hili kwa sababu tangu nizaliwe sijawahi kusikia wala kuona mambo haya, niwaambieni tu kuwa kweli yametokea mtaani kwangu,” alisema mjumbe huyo.
MAJIRANI WAO
Baadhi ya majirani na wazazi wa Irene walisema kwamba, japokuwa mtoto huyo alifariki dunia mwaka jana na kuzikwa lakini walivyomwona wao ni yeye yule waliyemzika!
“Yaani hakuna shaka kabisa kwamba huyo mtoto ni Irene mwenyewe, sijui nini kilifanyika lakini kusema kweli ni mwenyewe na kweli kifo chake kiliacha maswali hapa mtaani,” alisema jirani mmoja.
KABURINI
Ili kuthibitisha kuzikwa kwa mtoto huyo, mwandishi alifika kwenye kaburi alilozikwa mtoto Irene mwaka jana na kulikuta limeshaota majani huku mchwa wakiwa wameanza kuutafuna msalaba sehemu ya chini.
Msalaba huo ulisomeka hivi; IRENE EMMANUEL, KUZALIWA 01/10/2013. Hata hivyo, sehemu yenye tarehe ya kifo ndiyo ililiwa na mchwa.
MPANGO WA KULIFUKUA KABURI
Baba mzazi wa Irene alipoulizwa kama wana mpango wa kulifukua kaburi alilozikwa binti yake, alisema hawajafikiria hilo.
KWA SASA IRENE
Kwa sasa, mtoto Irene yuko kwa wazazi wake huku mganga huyo akisema ataendelea kumpatia dawa mpaka atakapoimarika zaidi na kuendelea na makuzi.
CHANZO:GPL
Post a Comment