WAKAZI wawili wa Kijiji cha Bukigi kilichopo Kata ya Malampaka mkoani Simiyu, wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kupatikana na viungo vya binadamu.
Waliofikishwa juzi katika Mahakama ya Wilaya ya Maswa mbele wa Hakimu Tumaini Marwa, ni Matheyo Yumbu (50) na Juma Mihangwa (28).
Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Nassibu Swedy kuwa Mei 5, mwaka huu, saa 11 alfajiri katika Kijiji cha Bukigi, washitakiwa hao walikutwa wakiwa na viungo hivyo.
Alidai viungo walivyokutwa navyo washitakiwa hao ni fuvu la kichwa, mifupa ya miguu na mikono ya binadamu wakiwa wamevihifadhi katika mfuko wa sandarusi katika nyumba waliyoishi.
Hata hivyo, washtakiwa hao walikana kosa hilo na kunyimwa dhamana na walipelekwa mahabusu hadi hapo kesi itakapotajwa tena Mei 29, mwaka huu na upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Post a Comment