Msanii wa filamu nchini na Mkurugenzi wa Endless Fame Production, Wema Sepetu, amedai kuwa yupo tayari kumaliza bifu lake na msanii mwenzake Kajala Masanja, baada ya kutokuwa katika maelewano mazuri kwa muda mrefu.
Bifu hilo lilichukua sura mpya ambapo Wema, alikataa kabisa kumsamehe
mwanadada Kajala, na kujiapiza kuwa kamwe hawezi kumsamehe licha ya
Kajala kutaka kumaliza tofauti hizo.
Wema amesema kuwa hakuna mwanadamu asiye na mapungufu na
kumtaka Kajala kuonana naye na kumaliza tofauti zao kwani nafsi yake
imeshamsamehe na imemuongoza kufanya hivyo.
Amedai kuwa kila jambo lina mwisho wake, hivyo amekaa chini na
kufikia uamuzi huo ambao anaamini kabisa hapa duniani hakuna mtu
asiyekuwa na moyo wa huruma na kusema kuwa hana budi kuyapuuza
yaliyopita.
Amesema kuwa hana tatizo na Kajala, na kutaka watu kuamini kuwa
amejitolea kumaliza tofauti hizo na kudai kuwa yupo radhi kukutana naye
sehemu yoyote kuongea ili wale wasiomuamini wapate kuamini.
Kwa upande wa Kajala, amedai kuwa anashukuru kusikia hivyo na kudai
kuwa hana tatizo na mtu na kumshukuru Wema, kwa uamuzi wake kwani
alijitahidi kadri ya uwezo wake kuhakikisha kuwa wanamaliza tofauti zao
kwa njia mbalimbali lakini alikataa.
“Nimekuwa nikipigania hilo kila kukicha, sasa naamini Mungu atakuwa
amesikia kilio changu kwa mara nyingine, napenda kusema sina tatizo
lolote katika hilo,” alisema Kajala.




Post a Comment