MAKUNDI
ya vijana jana yalionekana kumiminika mithili ya kumbikumbi warukapo
wakati wa masika wakimsindikiza mgombea urais Edward Lowassa
anayewakilisha Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Lowassa
ambaye alifika makao makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua
fomu za kugombea, alifanya hivyo chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA), ulioanzishwa wakati wa Bunge Maalum la Katiba.
Makundi
ya vijana yalionekana katika nyuso zilizojaa furaha na bashasha
wakithibitisha imani yao kwa Lowassa ambaye alihamia Chadema baada ya
kukatwa jina lake katika kile alichokieleza mwenyewe “mpango wa
kunihujumu.”
Vijana
walijitokeza na masanduku ya mfano wa jeneza, wakiimba nyimbo za
kumtaka Dk. John Magufuli anayegombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi
(CCM) ahame chama hicho na kuingia kambi ya Ukawa.
Vijana
wanaonekana kuguswa na nguvu iliyoimarika katika kundi la UKAWA
wakiamini nguvu hiyo itakidhi kiu yao ya mabadiliko ya uongozi nchini.
Lowassa
alihama CCM mapema mwezi huu na kujiunga Chadema, chama alichosema
kimepata mafanikio makubwa katika kujenga mtandao nchi nzima.
Tangu alipohama CCM, Lowassa amekuwa akirudia maneno yaliyosemwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwamba “Watanzania wanataka mabadiliko na wakiyakosa ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM,” akimaanisha
kuwa ameingia Chadema na kubeba dhamana ya UKAWA ili kusaidiana na
viongozi wao kutafuta mabadiliko waliyoshindwa kuyaleta CCM.
Hali
imekuwa tofauti na ilivyotarajiwa kuwa kujiuzulu kwa aliyekuwa
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, kuwa
kungesababisha mpasuko CUF na UKAWA, badala yake maelfu ya wanachama
wanaendelea kumuunga mkono Lowassa kuwa Rais.
“Nimepata
faraja sana kujiunga na Ukawa japo kumekuwa na misukosuko. Ni lazima
tuwe wamoja, mtunze kadi zenu za kupigia kura. Mwaka huu lazima
tushinde, tena kwa kura asilimia 90 ili wakiiba asilimia 10
tusisikitike,” alisema Lowassa alipozuru Ofisi Kuu za CUF juzi
ambako pia alihutubia Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lililofanya kikao
cha dharura kutafuta kuziba nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa
chama hicho.
Lowassa
aliondoa uvumi kwamba akichaguliwa kutakuwa na vurugu nchini. Alisema
kutakuwa na utulivu mkubwa na wafanyabiashara hawana sababu ya kuhofu.
Post a Comment