Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amesema anawatakia kila la heri wanaobeza nguvu ya umma.
Kutokana
na umati wa watu waliojitokeza jana kumlaki kuanzia Uwanja wa Ndege wa
Mwanza alikowasili saa saba mchana, iliuchukua zaidi ya saa mbili
msafara wake kuingia Viwanja vya Furahisha saa tisa alasiri, ambako ni
takriban kilomita nane.
Katika hotuba yake iliyochukua dakika 14
kuanzia saa 11.53 hadi 12.07 jioni, Lowassa alisema anawasikitikia
wanaobeza nguvu hiyo ya umma.
“Haya siyo mapenzi, haya ni mahaba.
Wanaobeza nguvu hii ya umma nawatakia kila la heri,” alisema Lowassa
huku akishangiliwa na umati huo.
Akizungumzia idadi hiyo ya
wananchi, mke wa mgombea huyo, Regina Lowassa alisema haijawahi kutokea
maeneo yote waliyotembelea Dar es Salaam, Mbeya na Arusha.
“Mwanza nimewapenda, nafikiri baba (Lowassa) akitoka hapa atalala usingizi mzuri mzito,” alisema Regina.
Lowassa
aliwataka polisi kutoingilia mchakato wa uchaguzi na kutumiwa na CCM
kupambana na wapinzani na kwamba, wakiendelea watakuwa wanajitafutia
tiketi ya kupelekwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), mjini The
Hegue.
“Nimesikitishwa sana kuwa watu wamepigwa mabomu asubuhi.
Mkiendelea na mchezo huu tukimaliza uchaguzi tutawapeleka The Hague
mkakipate cha mtoto na huko hamtarudi tena,” alisema.
Polisi
mkoani hapa jana walilazimika kutumia mabomu ya machozi, kuwatawanya
wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa ambao walifurika Uwanja vya Ndege wa
Mwanza kumpokea Lowassa.
Lowassa aliwasili akiwa ameambatana na
mgombea mwenza, Juma Duni Haji, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Twaha
Taslima na Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi.
Mabomu ya
machozi yalianza kurindima saa tano asubuhi, baada ya baadhi ya wafuasi
wa Ukawa kutaka kuingia kwenye lango la uwanja wa ndege, huku wengine
wakijaribu kuwatunishia misuli polisi kwa kuwatupia mawe.
Hekaheka
za mapokezi ya Lowassa zilianza saa mbili asubuhi, baada ya maelfu ya
wafuasi wa Ukawa wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali ikiwamo: “Oil
chafu ni kiboko ya mchwa” kutanda kwenye barabara inayoelekea uwanja wa
ndege.
Msafara wa Lowassa kutoka uwanja vya ndege
uliongozwa na pikipiki ambazo zilikuwa zinapeperusha bendera za vyama
vya CUF, Chadema ,NCCR Mageuzi na NLD, huku viongozi hao wakiwa kwenye
magari ya wazi.
Lowassa alisema ziara yake hiyo inahusu
kujitambulisha na asingependa kuwapa nafasi wapinzani wake kumtafsiri
kuwa hajui sheria, lakini kero za Mwanza anazifahamu hivyo akaahidi
kurejea na mikakati ya kuzitatua.
Loading...
Post a Comment