Mgombea
urais kwa tiketi ya Chadema na Ukawa, Edward Lowassa jana alipokewa na
maelfu ya watu mjini hapa ambao kwenye uwanja wa Ruanda, Nzovwe,
aliwaambia wananchi kuwa hatataka mchezo katika serikali atakayoiongoza.
Pamoja na
Jeshi la Polisi kutangaza kuzuia msafara wakati wa ziara ya waziri huyo
mkuu wa zamani, hali ilikuwa tofauti jana wakati zaidi ya magari 20
yalimsindikiza kutoka Uwanja wa Ndege wa Songwe huku wananchi
wakijitokeza barabarani kumshangilia hadi kwenye uwanja huo, ulio nje
kidogo ya mji wa Mbeya ambako alihutubia.
Polisi walinda msafara
Msafara
wa Lowassa uliwasili mjini hapa kwa kutumia ndege mbili, ya kwanza ikiwa
imebeba waandishi wa habari wapatao 10 na nyingine iliyombeba mbunge
huyo wa Monduli ambayo iliwasili saa 8:20.
Umati wa
watu ulikuwa ukimsubiri nje ya uwanja huo na alipotoka ilianza safari ya
kuelekea katikati ya jiji na msafara wa zaidi ya magari 20 pamoja na
pikipiki.(VICTOR)
Polisi walitanda barabarani, huku vijana wa Red Brigedi waliovalia sare nyeusi na miwani wakiwa wamesambazwa barabara yote.
Maeneo
ambayo msafara ulipita kwa shida kutokana na umati wa watu kufurika ni
Mbalizi, Mafiati Mwanjelwa, lakini polisi walifanya kazi ya ziada
kuwaondoa watu waliokuwa wakitaka kuandamana kuusindika msafara huo.
Lowassa
aliambatana na mgombea mwenza, Juma Haji Duni, mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe, mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia na kulakiwa na
viongozi wa mkoa pamoja na mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi,
maarufu kwa jina la Sugu.
Akizungumza
baada ya kukaribishwa kuhutubia na Duni Haji, Lowassa alianza kwa
kibwagizo cha “mchakamchaka chinja” na kabla ya kuwashukuru wananchi wa
mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa kufurika hadi pomoni kwenye uwanja
huo.
“Sitaki mchezo,” alisema Lowassa ambaye amekuwa akizungumzia uendeshaji wa Serikali kwa mtindo wa mchaka mchaka.
“Nataka
maendeleo. Nataka Jiji la Mbeya liwe la kimataifa wakati wa Serikali
yangu na litakuwa kama nchi ya Swaziland,’’ alisema akilifananisha jiji
hilo na nchi hiyo ndogo iliyozungukwa pande zote na Afrika Kusini.
“Nitahakikisha Uwanja wa Ndege wa Songwe unakuwa wa kimataifa.”
Lowassa,
ambaye alipata zaidi ya watu 50,000 mjini hapa wakati alipokuwa akisaka
wadhamini wa urais kwa tiketi ya CCM, alisema Serikali yake pia
itawajali walimu na wakulima, huku akisisitiza kwamba watakaochelewesha
pembejeo watakiona cha moto.
Akizungumza
polepole, Lowassa alisema katika Serikali yake hatataka mchezo katika
kazi na kwamba mawaziri wake watachapa kazi saa 24 kuwahudumia wananchi.
Kuhusu
kiu ya wananchi waliotaka kujua kauli yake kwa polisi, alisema polisi
wanatenda kazi huku wakitaka mabadiliko ya kupata mshahara mnono na
kwamba ataboresha mahitaji ya wafanyakazi kwa ujumla.
Awali
akiwakaribisha wageni, Sugu aliwashukuru wakazi wa Mbeya kwa kile
alichokieleza kuwa ni kuleta mizuka kwenye uwanja huo kutokana na
kufurika watu wengi. “Karibu Mbeya wageni, hapa siyo mafuriko ni
gharika... kilichobaki ni kupiga kura ya kukuchagua wewe Rais Lowassa,’’
alisema.
Sugu
alisema goli la mkono la CCM litazuiwa na beki makini Lowassa na kutoa
onyo kwamba CCM wasidiriki kutumia kadi bandia za wapiga kura.
Naye
Mbatia alisisitiza suala la Watanzania kulinda amani na upendo na
kuwasihi wakazi wa Mbeya wasikubali kufanya vurugu katika kipindi chote
cha kampeni na uchaguzi.
Wabunge wawili wajiunga Chadema.
Wakati
Lowassa akipata wadhamini, Chadema ilipata neema tena wakati wabunge
wawili wa CCM, Dickson Kilufi wa Mbarali na Luckson Mwanjale wa Mbeya
Vijijini walipotangazwa kujiunga na chama hicho kikuu cha upinzani.
Hata hivyo, Mbowe alimkabidhi kadi Kilufi pekee baada ya Mwanjale kutofika eneo hilo licha ya kuonekana uwanja wa ndege.CHANZO:MWANANCHI
Post a Comment