Dar/Makete.
Mawaziri wawili wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete wameanguka kwenye
marudio ya kura za maoni zilizofanyika juzi, huku matokeo ya Jimbo la
Busega yakikwama baada ya Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk
Titus Kamani kumshambulia msimamizi wa uchaguzi.
Walioanguka
ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid (Rufiji) na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais (Mazingira), Dk. Binilith Mahenge (Makete), huku
Dk Raphael Chegeni akiongoza kwenye Jimbo la Busega.
Vurugu kubwa Busega
Hali
ilikuwa mbaya jimboni Busega ambako baada ya Dk Kamani na wafuasi
walizuia matokeo kutangazwa na kuibuka kwa vurugu zilizosababisha polisi
kuingilia kati na kukamata watu wanne walioonekana kumuunga mkono.
“Napigania
haki yangu,” alisema Dk Kamani baada ya kutulia kwa vurugu ambazo
zilihusisha kupigwa kwa msimamizi wa kura hizo za maoni, Jonathan
Mabiya.
(VICTOR)
“Huu ni
ushindani. Uchaguzi uliopita tulikubaliana na matokeo na tulisaini,
lakini uongozi umesema turudie, leo hatujasaini wanataka kutangaza kwa
nguvu, hatujakubaliana.”
Mkuu wa
Wilaya ya Busega, Paul Mzindakaya, licha ya matokeo kutotatangazwa
alisema watu hawana budi kukubaliana na matokeo na kusema kitendo cha Dk
Kamani kwa kuhusika kwenye vurugu hizo ni cha kibinadamu.
“Aliyeshinda
ameshinda tu hakuna namna. Kilichofanywa na Waziri Kamani kumpiga
msimamizi huyo ni mambo ya binadamu tu... lakini walioshindwa lazima
wakubali matokeo na lazima yatangazwe,” alisema Mzindakaya.
Halmashauri
Kuu ya CCM iliagiza kurudiwa kwa kura za maoni za ubunge kwenye jimbo
hilo baada ya kubaini kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa kanuni. Katika kura
za Awali, Dk Kamani na Dk Chegeni, kila mmoja kwa wakati wake
alijitangaza kuwa mshindi, lakini baada ya matokeo rasmi kutangaza Dk
Chegeni aliibuka mshindi kwa kupata kura 13,048 dhidi ya 11,829 za Dk
Kamani.
Jana,
vurugu zilianza saa 4:00 asubuhi baada ya Dk Kamani, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Simiyu, kuingilia kati wakati Mabiya,
ambaye ni katibu wa Wilaya ya Meatu, akianza kutangaza matokeo.
Vurugu
hizo zilisababisha wafuasi wanne wa Dk Kamani kukamatwa na polisi.
Walikuwa wakigomea ujumlishaji matokeo, lakini baada ya kushindwa
kuzuia, walianza kupiga huku wakitukana, hali iliyosababisha ofisa wa
polisi Wilaya ya Busega aliyefahamika kwa jina moja la Nyaoga, kutoa
onyo.
Hali
iliyosababisha wananchi waliokuwa kwenye uwanja wa ofisi za CCM wilayani
Busega, kushangilia huku wakiimba: “Tuna imani na Chegeni, Chegeni
jembe, Kamani siyo chaguo letu.”
Baada ya
Polisi waliokuwa na silaha kuimarisha ulinzi, Mabiya alisimama kutangaza
matokeo lakini akakatishwa baada ya kurukiwa na watu walioonekana
kumuunga mkono Waziri Kamani na kupigwa makonde mbele ya polisi na
Mzindakaya.
Kipigo
hicho kilimfanya Mabiya akimbilie ndani ya ofisi za chama hicho na
kuacha askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakitumia nguvu
kudhibiti watu hao.
Wakati
wote wa vurugu hizo, Dk. Chegeni alikuwa amesimama pembezoni mwa ofisi
za chama hicho akishuhudia matukio hayo, lakini baadaye akaondoka akiwa
amepanda gari lake huku akishangiliwa.
Baada ya
polisi kufanikiwa kutuliza ghasia, Mabiya alisimama tena kutangaza
matokeo hayo, lakini Dk Kamani alimfuata na kumshambulia kwa makonde,
hali iliyozua tafrani kubwa zaidi.
Wafuasi wanne wa waziri huyo walikamatwa.
Lakini mtu wa karibu na Dk Kamani alikanusha waziri huyo kumshambulia msimamizi wala kuhusika kwenye vurugu.
“Hivi
unamfahamu mheshimiwa Kamani? Ni mtu muadilifu na wala asingeweza
kupigana,” alisema mtu huyo baada ya Waziri Kamani kutopatikana
kuzungumzia suala hilo.
“Tunachokipinga
sisi ni Chegeni kushinda usiku mzima na viongozi wa wilaya wakihesabu
kura wakati watu wetu sisi hawakuwapo. Tunauliza ameshindaje, hawasemi.”
Alilaumu
kitendo cha polisi kukamata watu watatu waliokuwa wanamuunga mkono Dk
Kamani wakati kwenye vurugu hizo kulikuwa na watu wa pande zote.
Dk Kamani
aliondoka eneo hilo saa 5:12 na gari aina Toyota Land Cruiser huku
kukiwa na ulinzi mkali wa polisi. Matokeo ya awali ya kura hizo
yalionyesha kuwa Dk Chegeni alikuwa anaongoza kwa tofauti ya takriban
kura 2,300.
Chegeni anena
Akizungumzia
sakata hilo, Dk Chegeni alisema:“Sikutarajia kama mwenyekiti wa CCM wa
mkoa, mbunge na waziri aliyekuwa mgombea urais na mzee wa familia
kumpiga msimamizi wa uchaguzi.
“Kitendo
cha kumshambulia msimamizi wa uchaguzi ni aibu na kinadhalilisha nafasi
na utu wake. Akiwa kiongozi. alipaswa kusoma alama za nyakati siyo
kupiga watu. Kama nisingekomaa mimi lolote lingeweza kutokea maana
uchaguzi uliopita alichakachua.”
Rufiji
Kwenye
jimbo la Rufiji, katibu wa CCM wa wilaya, Musa Liliyo alisema Waziri
Seif alishindwa baada ya kupata kura 5,010 dhidi ya Mohamed Mchengerwa
aliyeshinda kwa kupata kura 6,002.
Katibu
huyo aliwataja wagombea wengine walioshiriki uchaguzi huo na kura zao
kwenye mabano kuwa ni Hassan Sule (325), Shaaban Matwebe (126), Mohamed
Salehe Afif (121), Jamal Rwambo (78) Juma Kiolobele (51) na Tano Seif
Mwera (17). Hata hivyo, Dk Seif alikubali matokeo hayo akisema
hayatasababisha ahame CCM.
“Haiwezekani
katika baadhi ya vituo, inaonyesha idadi ya watu waliojiandikisha ni
300, lakini waliopiga kura ni 800, huu ni uhuni mkubwa unaokivuruga
chama chetu cha CCM,” alisema Dk Seif.
Dk Seif
anabainisha kuwa hatishwi na matokeo hayo kwa kuwa kwa taratibu za CCM,
wingi wa kura si kigezo cha mwisho mtu kupitishwa na chama kugombea
nafasi aliyoshinda.
Kwa
mujibu wa Dk Seif, mwanasiasa yeyote aliyebobea hawezi kuhama chama kwa
sababu ya kushindwa kwenye uchaguzi, hivyo hafikiri kabisa kuondoka CCM
ila ametoa wito kwa viongozi kuzitazama upya taratibu za namna ya kupata
haki pale mtu anapokuwa ameonewa.
Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM Wilaya ya Rufiji, Musa Nyelesa amekiri kuwepo
kasoro katika uchaguzi huo na kubainisha kuwa hata hivyo idadi ya
wapigakura ilikuwa ndogo ikilinganishwa na uchaguzi uliopita.
Nyelesa
alikitahadharisha chama hicho kuwa makini ili CCM iendelee kuwa chama
cha wananchi, vinginevyo kitakuwa chama cha matajiri na wafanyabiashara
wakubwa ambao hutumia fedha nyingi kupata madaraka.
“Tumeshuhudia
genge kubwa la wahuni waliotoka Dar es Salaam kuja kusimamia kura hapa
Rufiji. Hawa watu wametumia kila aina ya mbinu kuhakikisha kuwa mtu wao
anapita katika mchakato huu, hii si sawa, ila kwa kuwa nina imani na
chama changu najua kitarekebisha hizi kasoro,”alisema Nyelesa.
Kuhusu
ushindi huo, Mchengerwa alisema: “Matokeo hayo ni faraja kwa Wanarufiji
na yamenipa somo kwamba natakiwa kuwatumikia Wanarufiji na si kuwa
kiongozi wao.”
Makete
Waziri mwingine, Dk.Binilith Mahenge ameanguka baada ya kupata kura kura 7,885 huku Dk Norman Sigala King akipata kura 8,838.
Katibu wa
CCM wa Mkoa wa Njombe, Hosea Mpagike aliwataja wagombea wengine kuwa ni
Bonic Mhami, aliyepata kura 124, Fabian Nkinga (74) na Lufunyo Nkinda
(42).
Matokeo hayo yanasubiri kupitishwa na Kamati Kuu ya CCM.
Ukonga
Jimboni
Ukonga, matokeo ya marudio ya kura za maoni yameendelea kumpa ushindi
Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa baada ya kupata kura 10,965 dhidi
ya mpinzani wake Ramesh Patel aliyepata kura 6,960.
“Huwezi
kutofautisha Ukonga na Silaa, wananchi wananikubali. Ndiyo maana
niliamua kukaa kimya wakati haya yote yakitokea kwa sababu mimi ni
kiongozi wa CCM ninajua nini ninachokifanya,” alisema Silaa.
Habari hii imeandaliwa na Shaban Lupimo na Bakari Kiango.
Post a Comment