Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad akipewa
maelezo ya ujenzi wa kituo cha kuwarekebisha watu walioathirika kwa
matumizi ya dawa za kulevya huko Kidimni Wilaya ya Kati. Anayetioa
maelezo hayo (aliyenyoosha mkono) ni Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dk. Omar
Dad Shajak. Picha na Salmin Said, OMKR.
MAKAMU
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesifu
maendeleo mazuri ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha kuwarekebisha kitabia
watu walioingia katika matumizi ya dawa za kulevya kinachojengwa
Kidimni Wilaya ya Kati Unguja.
Maalim
Seif ameeleza hayo leo wakati alipotembelea ujenzi wa kituo hicho
unaofadhiliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambao unakisiwa
utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.6 na kujengwa na kampuni ya
Alhilal ya hapa Zanzibar.
Makamu
wa Kwanza wa Rais amewahimiza wasimamizi, wajenzi na mafundi
kuhakikisha wanaendelea na kasi hiyo hiyo, ili kuhakikisha jengo hilo
linapatikana katika wakati muafaka.
Akitoa
maelezo kwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dk.
Omar Dadi Shajak amesema jengo hilo litakapo kamilika litakuwa la ghora
tatu na litaweza kutumiwa na watu wapatao 400 wanaume na wanawake.
Amesema
vijana watakao kuwepo katika kituo hicho mbali ya kupatiwa matibabu na
ushauri wa kuondokana na matumizi ya dawa hizo haramu, pia watapatiwa
mafunzo ya ujasiri amali katika karakana itakayo jengwa, ambapo pia
kutakuwa na shamba kwa ajili ya kuwapatia mafunzo ya kilimo.
Naye
Mwakilishi wa kampuni ya ujenzi ya Alhilal, Hemed Nassor amesema ujenzi
wa sehemu ya chini ya jengo hilo unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba
mwaka huu, na jengo kamili linatarajiwa kuwa tayari katika kipindi
kisichozidi miaka miwili ijayo.
Katika
ziara hiyo, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad
alifuatana na Waziri wa Nchi wa Ofisi yake, Fatma Abdul Habib Ferej,
Katibu Mkuu Dk. Shajak na Naibu Katibu Mkuu, Dk. Islam Seif Salum.
Khamis Haji, OMKIR
Post a Comment