Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imesema kuwa imeunda timu ya ushindi ya kuhakikisha matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu yanatangazwa kwa wakati, ya kweli na haki kwa pande zote.
Akizungumza na gazeti la Nipashe
jana lililotaka kujua mipango ya Tume ili kuondoa malalamiko ya
wananchi, vyama vya siasa, wagombea na wadau kuhusu kucheleweshwa
matokeo na kuzua hofu ya uchakachuaji, Mkurugenzi wa Nec, Ramadhani
Kailima, alisema timu hiyo itakuwa na wajibu mkubwa na hakuna kulala
hadi matokeo yote yawe wazi.
“Tutakuwa
na timu ya ushindi kutangaza matokeo yote mapema, hakuna kulala hadi
tutoe matokeo kwa wakati, ya haki na kweli na yanayoaminika kwa
wapigakura,” alisema.
Alisema
malalamiko ya kupendelewa kwa chama chochote hayana msingi wowote kwa
kuwa Tume haina chama na haitapendelea chama zaidi ya kuweka wazi
matokeo yote itakayoyapata kwa wakati kwa kuwa watakuwa wanafanya kazi
kisasa zaidi.
Alipoulizwa
juu ya uzoefu wa Tume miaka ya nyuma kuhusiana na kuchelewesha matokeo
hata ya maeneo ya mijini kunakofikika kirahisi, Kailima alisema kama
kutakuwa na ucheleweshaji sababu zitawekwa wazi na wapigakura
watatangaziwa bila kificho.
“Ya
2010, yasizungumziwe sasa kwa kuwa tunafanya kazi kisasa kuhakikisha
matokeo yanakuwa wazi na kila hatua wananchi watatangaziwa,” alisema na
kuongeza:
“Tunawaomba
wananchi mara baada ya kupiga kura wakae mbali na ikiwezekana waende
nyumbani kwa kuwa kila kituo cha kupigia kura kutakuwa na mawakala kama
kuna tatizo lolote la kufanya matokeo yasitangazwe kwa wakati,
watajulishwa mapema.”
Kailima
alisema Nec iko huru na inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria
na kanuni na haiingiliwi kokote kwani katika kugawa majimbo, Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ambacho kinadaiwa kubebwa na Tume, kimelalamika na kama
wangekuwa wanapendelewa, ni wazi kuwa malalamiko yao yangesikilizwa,
lakini Tume imeamua kufanya kazi zake kwa uhuru.
“Uhuru
wetu siyo jina, bali ni kutekeleza majukumu ya kikatiba na sheria bila
kuingiliwa, kiwe chama au mtu hawaruhusiwi kutangaza matokeo ya
uchaguzi, bali msimamizi wa uchaguzi wa kata atatangaza ya kata, ubunge
yatatangazwa na Mkurugenzi wa Manispaa, mji au halmashauri na Tume
itatangaza matokeo ya urais,” alisema.
Alisema
watumishi wote wa Tume kabla ya kufanya kazi huapishwa kujiondoa au
kukana itikadi ya chama chake na kuanza kutekeleza majukumu yake ili
kusiwe na upendeleo kutokana na itikadi.
Alipoulizwa
kuhusu matukio kadhaa yaliyotokea katika uchanguzi mkuu wa mwaka 2010
ikiwamo wasimamizi wa baadhi ya majimbo mfano, Shinyanga mjini kutoroka
baada ya kutangaza matokeo yenye utata yaliyompa ushindi mgombea wa CCM
na kuzua vurugu, Kailima alisema:
“Tuko
2015, tumejipanga kikamilifu, ndiyo maana tuna timu ya ushindi
kuhakikisha hakuna ucheleweshwaji wa matokeo. Itakuwa Tume tofauti na ya
miaka mingine.”
Post a Comment