Mmoja wa makada wa CCM aliyekuwa rafiki wa karibu na Edward Lowassa wakati wa mchakato wa urais ndani ya CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, ameibuka na kudai kuwa, hana kinyongo na yaliyotokea Dodoma huku akionesha kuwashangaa wanaoendelea kunung’unika, akisema watu wa aina hiyo hawakuwa pamoja na chama.
Aidha,
Nchimbi, mmoja wa makada vijana waliokulia katika mfumo wa kisiasa
ndani ya CCM alikoshika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Mwenyekiti wa Taifa
wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Mkuu wa Wilaya, Mbunge na Waziri, amesema
sasa si wakati wa kuendelea kuwa na makundi, bali kujenga umoja kwa
lengo la kukipa chama ushindi.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la UVCCM jijini Dar es Salaam.
Nchimbi
ambaye tangu baada ya uteuzi wa mgombea wa urais wa CCM amekuwa kimya,
ikiwa pamoja na kutojitokeza kuwania ubunge katika jimbo lake la Songea
Mjini na hata kuhusishwa na mpango wa kukihama chama, amesisitiza hana
kinyongo, bali anaunganisha nguvu zake na WanaCCM wengine kuhakikisha
ushindi wa Dk John Magufuli, Waziri wa Ujenzi aliyepewa jukumu la
kupeperusha bendera ya CCM katika urais.
Alisema
ndani ya UVCCM, umoja huo umekubaliana kumaliza makundi na kwamba hivi
sasa wapo kitu kimoja kwa ajili ya ushindi wa CCM.
Sadifa Amvaa Lowassa
Kwa
upande wa Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM, Sadifa Juma Hamisi, ameendelea
kutetea uamuzi wa CCM wa kutompitisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa kuwa mgombea urais kupitia chama hicho, akidai alipoteza sifa ya
kuwa Rais tangu enzi za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere.
Akifungua
Baraza Kuu la UVCCM, Dar es Salaam juzi, Sadifa alisema makada
wanaohama chama na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), walipoteza sifa za uongozi tangu enzi za Mwalimu Nyerere.
Sadifa
alisema Lowassa ambaye ni mgombea urais wa Chadema, alipoteza sifa ya
kuwa rais tangu enzi za Mwalimu Nyerere na kwamba dhamira yake hiyo
haitafanikiwa milele.
Aliongeza
kuwa, umoja huo haushtushwi na wimbi la wanasiasa maslahi wanaohama
chama. Sadifa alisema vijana wa CCM wamejipanga kuueleza umma udhaifu wa
wanasiasa hao.
“Hatutatishwa na watu wanaotumia fedha zao kusaka madaraka. Tumeamua kuvunja makundi yetu na tutaeleza uchafu wote…,” alisema Sadifa ambaye inaaminika alikuwa akimuunga mkono Lowassa kuwania urais ndani ya CCM.
Alisema umoja huo utashirikiana na chama, kuhakikisha Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli anapata ushindi mkubwa.
Alisema
mwaka huu, umoja huo utawadhihirishia wote wanaodhani chama ni uso wa
mtu wakisahau kuwa ni taasisi kwa kukipa ushindi wa kishindo kwenye
nafasi zote za uongozi.
Alisema CCM imepata mgombea makini na kwamba hana dosari wala hakuna sababu ya kutafuta sabuni ya kumsafisha.
Sadifa alisema Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM aliendesha vikao vya Chama kwa umahiri mkubwa.
Post a Comment