Mkuu wa Jeshi hilo IGP, Ernest Mangu.
Matukio
ya uvamizi wa vituo vya polisi yanayokwenda sambamba na kupora silaha,
kuua askari na kujeruhi imebainika kuwa yanasukwa na baadhi ya watumishi
wasiokuwa waaminifu waliopo ndani ya Jeshi la Polisi au waliofukuzwa
kwa makosa mbalimbali ukiwa ni mkakati wa kumdhoofisha kiutendaji Mkuu
wa Jeshi hilo IGP, Ernest Mangu.
Uchunguzi
wa kina ambao umefanywa kwa takribani wiki tatu sasa umebaini kuwa
hatua ya baadhi ya askari polisi kuasi ndani ya jeshi hilo kunatokana na
kuchukizwa na mambo kadhaa yaliyofanywa na IGP Mangu tangu alipoteuliwa
na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo.
Baadhi
ya watumishi wa serikali waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati
tofauti walisema mambo ambayo yamechukizwa baadhi ya watu ndani ya jeshi
hilo ni kutokana na kufukuzwa kazi askari wengi na wengine
kubadilishwa vituo vyao vya kazi kwa sababu mbalimbali, mambo ambayo
yamefanyika kipindi cha IGP Mangu.
“Unakumbuka
wakati Sanya (Laurance Sanya) alipokuwa RPC Mbeya kulitokea tukio moja
la uvamizi wa Kituo cha Polisi Tunduma lakini kipindi cha utawala wa IGP
Mangu yamejitokeza mengi hapa kuna sababu,” alisema.
Alisema
IGP Mangu amekuwa mkuu wa Jeshi la Polisi ambaye ameongoza kufukuza
askari hususani wanaokula rushwa ambao hakuwavumilia na ndiyo hao hao
wamegeuka kuwa adui wa jeshi hilo kwa kushirikiana na jamaa na ndugu zao
ambao bado wapo ndani ya utumishi wa jeshi hilo.
Jambo
la pili lililojenga hasira kwa askari hao ni hatua ya IGP Mangu kutoa
tishio kwamba askari wote ambao wana vyeti vya kughushi wajisalimishe.
“Taarifa
za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inaonyesha kuwa zaidi ya
watumishi 10,000 wa Jeshi la Polisi wana vyeti vya kughushi lakini kwa
bahati mbaya katika awamu zote za utawala wahusika wamekuwa wakiachwa
bila kuchukuliwa hatua na sasa IGP Mangu amekuja kuyavumbua,” kilisema
chanzo kutoka ndani ya serikali.
Chanzo
hicho kilieleza kuwa baada ya IGP Mangu kutoa tamko la kutaka watumishi
ndani ya jeshi hilo wenye vyeti vya kughushi wajisalimishe ndipo
matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi yalipoibuka kwa kasi ili mkuu
huyo wa Jeshi la Polisi aonekane ameshindwa kazi na kufukuzwa.
Anaeleza
kuwa kuhusisha matukio ya uvamizi huo na suala la ugaidi inaweza kuwa
siyo kweli kwa asilimia kubwa kwa sababu mara nyingi magaidi wanaofanya
matukio makubwa mfano nchi jirani wanakuwa na silaha kubwa kama AK-47
sasa inawezekanaje kama kweli ni magaidi hapa kwetu wawe wanapora
bunduki ndogo za SMG.
Mkurugenzi
wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijobisimba,
alisema matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi yameanza kujitengeneza
pole pole na sasa yamekuwa makubwa.
“Matuki
ya vituo kuvamiwa yalianza kwa wananchi wenye hasira kutaka kutoa watu
waliokamtwa na baadaye wakaona kama kumbe ni rahisi kuvamia kuiba
silaha, kujeruhi askari na kuua,” alisema.
Alisema
wakati hali ya kiuslama ikibadilika, Jeshi la Polisi kwa upande wake
bado halijabadilika ili kukabiliana na matukio hayo.
“Zamani
usingeweza kuona askari anayetembea barabara ananyang’anywa silaha hata
kama huyo askari yukoje, lakini hivi sasa polisi wapo kwenye doria
wanavamia na kunyanng’anywa silaha, wanaenda kama vile nyumbani kwao na
bahati mbaya polisi wenyewe hawajashtuka,” alisema.
Kijobisimba alisema polisi wangekuwa wamebadilika kiutendaji matukio hayo yasingetokea.
Alisema
sababu nyingine ya kuibuka kwa matukio hayo ni ndani ya Jeshi la Polisi
lenyewe kuna tatizo ambalo inabidi litafutiwe ufumbuzi.
“Ukiangalia
tukio la uvamizi wa Kituo cha Polisi Stakishari ni utata, mimi nilikuwa
jeshini, utunzaji wa silaha unakuwa very secure (usalama mkubwa), sasa
wale Stakishari utunzani wao wa silaha unakuwaje kiasi kwamba wavamizi
waliingia mara moja na kuchukua silaha kama kweli hakukuwa na inside job
(kazi ya ndani),” alisema na kuongeza:
“Katika
tukio hilo pengine inawezekana hata mfungaji wa mlango wa kutunzia
ofisi akawa alisahau kufunga kwani wavamizi wasingeweza kufika kirahisi
na kupora.”
Bikijobisimba alisema mambo hayo yanaweza sehemu ambayo kuna askari ambao siyo waadilifu kutokana na jinsi wanavyopewa mafunzo.
“Zamani
kulikuwa na utaratibu mtu akitaka kuajiriwa polisi wanaangalia urefu
ndiyo wanachukuliwa, lakini leo hii hata wafupi wapo wengine na
inawezekana wanapelekwa na ndugu zao na pia mafunzo yanatolewa kwa miezi
sita wakati zamani ilikuwa miezi tisa,” alisema.
Alisema
mafunzo ya miezi sita kimsingi hayawezi kutosha kumfundisha askari kuwa
katika maadili mazuri na mkakamavu kiasi cha kuaminiwa kuwa mlinzi wa
taifa.
Kijobisimba
alisema ili kukabiliana na matukio hayo kuna umuhimu wa Jeshi la Polisi
kutafuta chimbuko la matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi kwani
lazima kutakuwa kuna tatizo.
Naye
mwanaharakati wa haki za binadamu, Julius Niselia, alisema matukio hayo
yanaonyesha kuwa mabadiliko ya uongozi ndani ya Jeshi la Polisi
yaliyomwingiza IGP Mangu hayakupokelewa vizuri ndani ya jeshi hilo na
baadhi ya askari waliokuwa watii kwa uongozi uliondoka ambao wamekumbana
na fagio la chuma la uongozi mpya na ndiyo wanaofanya njama hizo.
“Mangu
ni mkali sana hapendi askari wanaofanya uovu hivyo amekuwa akichukua
hatua haraka na kusababisha malalamiko kwa askari ambao walilelewa
vibaya ndani ya jeshi hilo na viongozi wapole wasiochukua hatua,”
alisema.
“Askari
wanaofukuzwa kwa utovu wa nidhamu ndiyo wanaounda magenge ya kihalifu
ili kumdhoofisha IGP Mangu aonekani hafai kiutendaji,” alisema.
Kwa
upande wake, Askofu wa Kanisa la Pentekoste World Mission
International, Samson Mwalyego, alisema chanzo cha matukio hayo ni
kuporomoka kwa maadili ndani ya Jeshi la Polisi.
Alisema
ndani ya jeshi hilo watumishi wanajali zaidi rushwa na wamekuwa siyo wa
siri wanapopewa taarifa jambo ambalo limewakatisha tamaa wananchi
kushirikiana nalo.
Wakati
hayo yakiendelea baadhi ya askari polisi wamelalamikia kitendo cha
serikali kupuuza malalamiko yao mbalimbali ikiwamo ubaguzi katika
upandishaji wa madaraja na nyongeza ya kima cha mshahara tangu miongoni
mwao walipopandishwa vyeo Agosti, mwaka jana.
Taarifa
za uhakika kutoka ndani ya jeshi hilo zinaeleza kwamba, kutokana na
hali hiyo kiwango cha utendaji kazi kwa polisi hao kimeshuka kutokana na
uongozi wa juu kukaa kimya.
Hata hivyo, imefahamika kwamba tatizo hilo limefanywa kuwa siri na hakuna askari anayeruhusiwa kuzungumzia kwa uwazi.
Askari
wachache ambao walikuwa mstari wa mbele kufuatilia suala hilo, imedaiwa
sasa wamenyamazishwa baada ya kupewa stahiki zao kinyemela.
“Tumevumilia
vya kutosha jambo hili, hivi vyeo tulivyopewa ni kama hewa, tukiuliza
ngazi za juu hawatupatii majibu ya kuturidhisha,” kilisema chanzo
kimoja.
Mmoja
wa askari hao ambaye alitaka jina lake lisitajwe, alisema malalamiko
hayo yanawahusu askari wengi nchi nzima ambao walikwenda katika mafunzo
mwaka jana.
Alisema
licha ya kufanya vizuri na kupandishwa vyeo mbalimbali vya kijeshi,
mishahara yao imebaki kama mwanzo jambo ambalo limewarudisha nyuma
kiutendaji.
“Huwezi kufanya kazi nzuri katika hali hii, tunachoomba serikali isikilize kilio chetu na kututatulia,” alisema askari huyo.
Askari
mwingine alisema huko nyuma waliunda kamati maalum ya kufuatilia suala
hilo ngazi za juu za jeshi hilo, lakini walikatishwa tamaa baada ya
kuona kuna tatizo katika mchakato wa kuwaongezea maslahi.
“Jambo
la kusikitisha watu wachache walionekana wasemaji waliingiziwa pesa za
nyongeza, tuliobaki hatujui tutafikiwa lini na hakuna anayethubutu
kusema kwa uwazi ili kulinda kibarua chake,” alisema.
TUME YAUNDWA
Askari
hao walidai mwanzo wa mwaka huu serikali ilifanya uhakiki wa watu
wanaotakiwa kuongezewa mishahara kulingana na nafasi zao za kazi.
Alisema
licha ya kupewa ushirikiano na askari hao katika vituo vyote
walivyotembelea, hadi sasa hakuna jibu lolote walilopewa, badala yake
walitakiwa kuukaa kimya.
“Tunajua IGP anajua tatizo hili vizuri, tunamuomba atusikilize malalamiko yetu na kuyafanyia kazi kwa haraka,” alisema.
VITUO VILIVYOVAMIWA
Katika
kipindi cha kuanzia Juni, 2014 mpaka Julai 13, mwaka huu, bunduki 53
zimeporwa katika matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi na askari 11
kuuawa.
Vituo
vya polisi vilivyovamiwa ni Newala mkoani Mtwara, ambako bunduki tatu
ziliporwa, mkoani Pwani katika wilaya ya Ikwiriri (bunduki saba),
Kimanzichana, wilaya ya Mkuranga (bunduki tano) mbili zikiwa za polisi
na tatu za raia zilizokuwa zimezihifadhiwa.
Vingine
ni Kituo cha Polisi Ushirombo wilaya ya Bukombe, mkoani Shinyanga
bunduki 18 ziliporwa, ingawa baadaye zilipatikana zote.
Kituo
cha Polisi Pugu Machinjioni, mkoani Dar es Salaam na Tanga, askari
waliokuwa katika shughuli za ulinzi na doria walishambuliwa na kuporwa
silaha tatu na Kituo cha Polisi Stakishari, Dar es Salaam ambako bunduki
20 ziliporwa na askari wanne na raia watatu kuuawa.


Post a Comment