WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda (Pichani)amesema Serikali bado inatafuta suluhisho
la kudumu litakalowezesha Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora) waweze
kupiga kura wakiwa huko waliko.
Ametoa
kauli hiyo juzi usiku (Jumatano, Agosti 19, 2015), wakati akijibu
maswali ya Watanzania waishio Uganda katika kikao kilichofanyika hoteli
ya Serena jijini Kampala.
“Serikali
tulitamani sana mchakato huu umekamilika mwaka huu ili Watanzania
waishio nje ya nchi waweze pia kushiriki uchaguzi mkuu lakini
tulipoongea na wenzetu wa NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi), ilibainika
kwamba isingekuwa rahisi kupeleka mashine za BVR nje ya nchi wakati huo
huo zoezi la uandikishaji likiwa linaendelea hapa nchini…”, alisema.
“Walisema
kuna suala la uandikishaji, likimalizika kuna suala la uhakiki wa
majina ya walioandikishwa… yote haya yanataka muda na maandalizi ya
kutosha,” aliongeza Waziri Mkuu.
Alisema
Serikali bado haijakata tamaa na yeye binafsi anaamini jambo hilo
linaweza kufanyika kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020 bila matatizo
yoyote.
Akigusia
kuhusu uandikishaji wapiga kura nchini, Waziri Mkuu alisema lengo la
awali lilikuwa ni kuandikisha wapiga kura milioni 24 lakini kutokana na
takwimu na uzoefu uliopatikana kwenye nchi za Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC), Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilishauri
lengo la Serikali liwe ni kuandikisha watu milioni 22.
“Lakini
kama wengi mlivyosikia, wakati hata hawajamaliza kuandikisha wakazi wa
mkoa wa Dar es Salaam, ambao ulikuwa wa mwisho, tayari tulishavuka lengo
la awali la kuandikisha watu milioni 24,” alisema.
Alisema
hilo ni jambo la kujivunia kwa sababu tangu mwanzoni, mchakato huo
ulikuwa umegubikwa na kelele nyingi na watu walihofia kwamba kwamba
zoezi hilo lisingekamilika. “Sote ni mashuhuda, watu wamejiandikisha na
sasa wanakamilisha taratibu za uhakiki,” aliongeza.
Waziri
Mkuu Pinda aliwasili nchini Uganda Jumatano usiku kwa ziara ya siku
moja akimwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye maadhimisho ya miaka 100
ya Chama cha Maskauti cha Uganda (Uganda Scouts Association – USA).
Amerejea nchini jana usiku.
Rais Yoweri Museveni ndiye mlezi wa chama hicho na alikuwa amemwalika Rais Kikwete kwenye maadhimisho hayo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
IJUMAA, AGOSTI 21, 2015.
Post a Comment