Mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa), ameipenya ngome ya mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, wilayani kwake Chato na kupata mapokezi makubwa.
Mkutano wa jana ulikuwa wa kwanza kufanyika mjini hapo akiwa ametokea Morogoro, mkutano mwingine aliufanya mjini Geita.
"Nikiutazama
huu umma nashtuka sana, hapa ni nyumbani kwa Magufuli. Wazanzibari
wanasema haya ni mahaba nami nayapokea. Mnanifanya nideke na hapa ni
nyumbani kwa Magufuli, watakaonipa kura wanyooshe mikono juu...mikono
namna hii inanipa faraja, nimepokea mahaba yenu," alisema Lowassa.
Akizungumzia
matatizo elimu Chato alisema atapiga marufuku michango ya wanafunzi na
kuanzia Januari watoto wote watasoma bure na elimu bora.
Alisema hatasahau kilimo na akasema wakulima wataruhusiwa kuuza mazao yao popote wanapotaka bila kubugudhiwa.
Alisema
atahakikisha pia wakazi wa Chato wanapata maji toka Ziwa Victoria kama
alivyowafanyia wakazi wa Mkoa wa Shinyanga ambao wanapata maji toka ziwa
hilo.
Aidha, alisema atafufua kiwanda cha kuchambua pamba kichopo wilayani hapa ambacho kimekufa wakati wa CCM.
Wakazi hao walimuahidi kura za ndiyo na kumuangusha Dk. Magufuli mapema asubuhi Oktoba 25, mwaka huu.
Alifanya mkutano huo katika eneo la stendi ya zamani ya mabasi mjini hapa jana.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alisema wapinzani hawana nia ya kuleta vita na vurugu.
"Sisi hakuna vita, tutawaondoa CCM kwa amani kabisa," alisema na kuongeza: "Chini ya CCM hakuna maendeleo."
Aidha alimtaka Dk. Magufuli kutoka CCM kama anaona kitanda chao kina kunguni na yeye hawezi kukilalia.
Mapema
Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, alisema yupo tayari
kurudi tena mahabusu ya Segerea tena na tena hadi Oktoba 25, mwaka huu.
Alisema
lengo la serikali kumbambikia kesi na kumnyima dhamana, ilikuwa ni
kuwatisha wananchi ili wakiona waziri mstaafu kama yeye anapelekwa
mahakamani na Segerea, watishike na kuingiwa na woga zaidi ili waachane
na Ukawa.
"Lengo
lilikuwa watu waone mimi kama waziri mstaafu na mwanasheria maarufu
nimefunguliwa mashitaka, wananchi waogope kujiunga na Ukawa," alisema.
Aliwaomba wakazi wa hapa hata kama wanaipenda CCM kukumbuka hali itakavyokuwa kwa watoto wao chini ya CCM.
Alisema
wakumbuke pale wanapokwenda hospitali na kukosa dawa, watoto wao kukosa
elimu na ajira, hivyo matatizo hayo yawafanye kuachana na CCM.
Alisema serikali atakayoiunda Lowassa itakuwa na uwezo mkubwa wa kuongoza kuliko ilivyo kwa Serikali hii ya CCM.
Alisema Dk. Magufuli haijui CCM kwa sababu hajawahi kuwa hata balozi wa nyumba kumi, hivyo hawezi kuwa kiongozi.
Alisema alijiunga na CCM mwaka 1991, lakini akiikumbuka CCM ya wakati huo na hii iliyoshika dola sasa, hazifanani kabisa.
"Kilichobaki kwa CCM hii ya sasa ni rangi ya kijani, alama ya rangi ya njano za jembe na nyundo, basi.
"Hiki
siyo tena chama cha wakulima na wafanyakazi, ni chama kilichokosa
maadili ya uongozi kiasi cha kuwasafisha watuhumiwa wa Escrow na Epa.
"Ilifikia
hatua sisi nafsi zetu zilitusuta, nikiwa nawaangalia watoto wangu
nilikuwa napata uchungu kuhusu hatma yao chini ya dola ya CCM," alisema.
Bila
kuwataja majina, alisema CCM imewapitisha baadhi ya wanachama wao
waliokuwa wakituhumiwa na ufisadi wa Escrow na EPA kugombea ubunge.
Kwa upande wake, Richard Tambwe Hizza, alisema huu ni mwaka ambao Mungu ametaka Lowassa awe rais.
Alisema Ukawa wana uwezo wa kuwaletea wananchi maendeleo tofauti na CCM.
'Mkitaka
kujua CCM ni watu wa ovyo, mliona jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM
wote walivyoimba, 'Tuna imani ni Lowassa, lakini Rais Jakaya Kikwete,
hakutaka kuwasikiliza," alisema.
Aliwataka wananchi wasigombane huko mitaani bali waelimishane.
Alisema hawawezi kuwaacha Watanzania wakiwa katika hali mbaya namna hii.
Alisema amezunguka nchi hii na kuona jinsi watu wanavyomkubali Lowassa utadhani walikuwa wanaishi nyumba moja.
"Mwaka huu Nyerere atafufuka na kumshuhudia Lowassa akiapishwa kuwa rais," alisema.
Alisema wananchi watakaoipigia kura CCM Oktoba 25, atatakiwa kujipima kwa kwenda hospitali.
Katika
hatua nyingine, aliyejitambulisha kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Walimu
Tanzania Wilaya ya Chato, Lucas Michael, alipanda jukwaani na kusema
katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato, ndiyo pekee ambayo walimu
wanalazimika kujinunulia chaki.
Alisema
walimu wilayani humo wananyanyasika na hata walimu wastaafu wanashindwa
kurudi makwao baada ya halmashauri kushindwa kuwapatia fedha za nauli.
Aliwataka walimu wenzake mbali na kufundisha popote walipo wasiwe waoga, wawafundishe wanafunzi ukweli.
"Walimu kokote kule mliko kafanyeni uamuzi sahihi, bila woga na wakati ndiyo huu wa kufanya maamuzi ya mabadiliko," alisema.
Mgombea
ubunge wa Jimbo la Chato, Dk. Benedickt Lukanima, alimweleza Lowassa
kuhusu matatizo ya maji ingawa wana ziwa, matatizo ya elimu bora kwa
watoto wao na dawa hospitalini.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema wamekubaliana na wenzake kurudi tena hapa kuzungumza mambo ya Chato.
Hata
hivyo, wananchi walipaza sauti zao wakimtaka azungumze wakati huo naye
akasema, namna pekee ya kuing'oa na kuizika CCM ni lazima ianzie hapa
Chato.
"Ili nchi hii iishi, tunahitaji kuizika CCM na mahali pa kuanzia ni hapa Chato," alisema.
Huku
baadhi ya vijana wakiwa wanapitisha mfano wa jeneza lililokuwa
limezungushwa bendera ya CCM, Lissu alisema Ukawa wamekuwa wakipata
matusi na kejeli nyingi na namna pekee ya kuiondoa madarakani ni
kumng'oa Dk. Magufuli na kuizika CCM.
Post a Comment