Mgombea
Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad,
akihutubia mkutano wa kampeni katika viwanja vya Kandwi jimbo la Chaani
Unguja.
Wafuasi wa CUF wakimsikiliza mgombea wao wa Urais katika viwanja vya Kandwi jimbo la Chaani.
Wafuasi wa CUF wakimsikiliza mgombea wao wa Urais katika viwanja vya Kandwi jimbo la Chaani. (Picha na OMKR).
Na: Hassan Hamad (OMKR)
Chama Cha
Wananchi CUF kimewahakikishia wakulima wa mwani bei nzuri ya zao hilo
iwapo wananchi watakipa ridhaa ya kuingia madarakani katika uchaguzi
mkuu ujao.
Mgombea
Urais wa Zanzibar kwa Chama hicho Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad,
ameeleza hayo wakati akiwahutubia wafuasi wa chama hicho katika mkutano
wa kampeni uliofanyika viwanja vya Kandwi jimbo la Chaani.
Amesema
kwa muda mrefu wakulima wa mwani wamekuwa wakiishi maisha duni kutoka
bei ndogo ya kilimo hicho ikilinganishwa na gharama za uzalishaji, jambo
serikali yake italipa umuhimu wa kipekee.
Amesema
kama ilivyo kwa zao la karafuu, serikali atakayoiongoza itafanya utafiti
wa bei ya mwani duniani, ili wakulima ambao wengi wao ni wanawake,
waweze kunufaika ipasavyo na kilimo hicho. Sambamba na hilo Maalim Seif
amesema iwapo atachaguliwa serikali yake itafanya utaratibu wa
kulisarifu zao hilo hapahapa nchini, ili kuliongezea thamani yake katika
soko.
Aidha
Maalim Seif amesema anakusudia kufanya mapinduzi ya kijani kwa
kuwawezesha wakulima kulima mazao mengi zaidi yenye tija, na mapinduzi
ya buluu kwa kuwawezesha wavuvi kuvua katika bahari kuu.
“Tutawatoa
wakulima kutumia jembe la mkono na kuendeleza kilimo cha kisasa”,
alisisitiza. Amesema pia wakulima watapatiwa utaalamu kuweza kulima
mazao ya viungo yakiwemo tangawizi, ili kuepuka kuagizia mazao hayo
Tanzania bara. Katika hatua nyengine mgombea huyo wa urais kupitia CUF
amesema ataweka utawala wa sheria ili kila mtu aweze kupatiwa haki yake
kwa mujibu wa sheria zilizopo.
“Hakuna atakayeonewa, kila mmoja atatendewa haki sawa sawa na mwengine, na wala hakuna atakayekuwa juu ya sheria”, alieleza.
Kuhusu
vitendo vya rushwa ameahidi kupambana na vitendo hivyo kwa nguvu zake
zote, kuweka maslahi mazuri kwa wafanyakazi, ili Zanzibar iweze
kuendelea bila ya rushwa, na kwamba rushwa imekuwa kikwazo kikubwa cha
maendeleo.
Amefahamisha
kuwa sheria zinazohusiana na rushwa zitapitiwa upya kuwezesha
wanaojihusisha na vitendo hivyo kuchukuliwa hatua bila ya muhali au
kuoneana haya.
Katika
salamu zake kwa wanawake wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mwakilishi wa viti
maalum anayemaliza muda wake kutoka Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Mhe. Kazija
Kona, amewataka wanawake wa Mkoa huo kumchagua Maalim Seif, ili
waondokane na kero ya kuwalipia ada nyingi watoto wao maskulini.
Ameeleza
kuwa serikali ya inayoongozwa na CCM iliwaahidi wananchi kuwapatia elimu
bora bila ya malipo, lakini wazazi wamekuwa wakibeba mzigo mzito wa
kulipia ada watoto wao, licha ya maisha magumu yanayowakabili.
Post a Comment