MASHEHE
sita waliokuwa wametekwa na waasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo
(DRC) wamerejea nchini jana, huku wakieleza kuwa kulitaja jina la
Tanzania kumewaokoa na kifo kutoka kwa waasi hao.
Kitendo
cha mashehe hao kutaja wanatokea Tanzania kimewasaidia kwani kwa mujibu
wao, waasi hao walisema hawana shida na Tanzania, lakini Wakongo
waliwadanganya hivyo hawawapendi.
Akizungumza
baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,
kiongozi wa mashehe hao, Mohammed Abdallah Khamis alisema, wakiwa njiani
kuelekea nchini humo walivamiwa na watu hao wakiwa na silaha za kivita
kisha kutekwa na kupelekwa porini.
“Mwanzo
hatukuelewa kama ni wanajeshi wa serikali au wanajeshi wa porini,
tulipofika nao porini ndiyo wakajitambulisha wao ni askari wa porini na
wanahitaji fedha ili watuachie ama watatuua,” alisema Khamis.
Akisimulia
jinsi walivyoishi porini alisema, walikuwa wanapata tabu kwani hata
chakula walikuwa wakipewa ndizi, maharage na magimbi ambayo waliambiwa
wale ili wasife, huku wakati mwingine wakiteswa na waasi hao kwa kupigwa
na magongo na vibao.
Alisema
waasi hao walihitaji wapewe kiasi cha dola za Marekani 20,000 (zaidi ya
Sh milioni 60) ili waweze kuachiwa. Khamis aliishukuru serikali ya
Tanzania kwa jitihada ilizofanya ili kuhakikisha wapatikana wakiwa
salama.
“Kwa kweli tunaipongeza sana serikali ya Tanzania na DRC maana wamefanya juhudi kubwa sana za kutuokoa.
"Bora kuishi mwaka mmoja gerezani lakini si kukaa na watu wale siku moja,” alisema.
Khamis
alisema, hata hivyo baadaye waliachiwa na waasi hao baada ya kuona
hawana fedha lakini pia ni wazee, hivyo waliwaachia kwa huruma na hasa
kwa kuzingatia hawana shida na Watanzania.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Mahadhi Juma Maalim akizungumza baada ya kuwapokea mashehe hao alisema,
wakati wote serikali ilikuwa ikifuatilia suala hilo ili kujua usalama
wao.
Hata
hivyo, alisema kuna umuhimu kwa Watanzania wanaosafiri kwenda katika
nchi tofauti kwa shughuli mbalimbali kuhakikisha wanatoa taarifa katika
Balozi zilizopo katika nchi hizo ili serikali iwe na taarifa ya
Watanzania hao.
“Tunaishukuru
sana serikali ya Congo na jamii nzima ya watu wa Goma ambao walitoa
msaada mkubwa na hata walinzi wa amani wa Congo walishiriki vizuri
katika kuhakikisha mnapatikana mkiwa salama,” alisema.
Alisema
kutokana na kuwa vikosi vya usalama vilikuwa vikifuatilia tukio hilo
kwa ukaribu, hata baada ya kuachiwa kwa mashehe hao, vikosi hivyo
vilifanikiwa kuwakamata watekaji hao.
Balozi
wa Tanzania nchini DRC, Anthony Cheche alisema, baada ya kupokea
taarifa hizo walifuatilia na baada ya kubaini ni Watanzania ndiyo juhudi
za kuwakomboa zikaanza.
Alisema
alikuwa akipokea simu nyingi kutoka kwa vyombo vya habari na ndugu,
jamaa na marafiki za kutaka kujua hali za mashehe hao lakini wakati
mwingine alilazimika kuficha ukweli ili kuepusha kuhatarisha usalama wa
mashehe hao.
“Tulipewa
tahadhari kuwa kuna mazingira hatarishi, hivyo kuna baadhi ya taarifa
zikitolewa zinaweza kusababisha tukawapoteza watu wetu na ndiyo sababu
kuna taarifa nilikuwa nikiziminya,” alisema.
Baada
ya kuachiwa kwa mashehe hao ambao wote ni wakazi wa Zanzibar,
walipokewa na Jeshi la DRC na kupewa ulinzi hadi Mji wa Goma ambapo
walikutana na viongozi wa mji huo pamoja na Balozi Cheche ambaye
waliondoka naye hadi mjini Kigali, Rwanda kwa ajili ya kurejea nchini.
Mashehe
hao ambao walienda nchini humo kwa ajili ya kutangaza dini, walirejea
jana kwa ndege ya Shirika la Rwanda saa 9:55 mchana ambapo pia jana
hiyohiyo waliondoka saa 12:00 kuelekea Zanzibar kwa ndege ya Shirika la
Precision.
Post a Comment