JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA
KWA UMMA
Wizara ya Maliasili na Utalii ikishirikiana na Shirika
la Uhifadhi Duniani WWF ofisi ya Tanzania kwa pamoja wanaadhimisha
siku ya tembo kitaifa mwaka huu tarehe 22/9/2015, kwa kujadili na
wadau mbali mbali kuhusu kumuokoa mnyama Tembo kupitia vyombo vya habari hapa
nchini. Kauli Mbiu ni ‘Wakati wa
kuhifadhi tembo waliosalia ni sasa’
Malengo ya kuadhimisha siku ya Tembo kitaifa ni;
kujenga uelewa na kuibua hamasa ya wananchi kuhusu uhifadhi wa tembo; kujadili
kwa kina madhara ya ujangili wa Tembo katika nyanja za kijamii, kiikolojia, kiutamaduni
na sekta ya utalii kwa jumla na kutoa mapendekezo na hatua za kuchukua kuzuia
ujangili wa Tembo.
Maadhimisho haya
yanatokana na mkutano wa 15 wa nchi wanachama wa Mkataba wa
Kimataifa wa kuzuia biashara ya Wanyamapori na viumbe walioko hatarini kutoweka
'Convention on International Trade in Endangered Species - CITES', uliofanyika mwaka
2010 katika mji wa Doha nchini Quatar.
Nchi 37 zilizojaliwa kuwa na tembo
barani Afrika zilikutana, na kupitisha mpango mkakati wa kuhifadhi tembo barani
Afrika (African Elephant Action Plan-2010). Mwaka uliofuatia 2011 Tanzania
ilianza kutekeleza mpango mkakati maalum wa uhifadhi wa Tembo (Tanzania Elephant
Management Plan 2010-2015).
Tanzania inasifika kwa kuwa na utajiri mkubwa wa
wanyamapori barani Afrika na Ulimwenguni kote, ni nchi ya pili duniani kwa kuwa
na rasilimali nyingi asili. Katika kuhakikisha kuwa wanyamapori hususani Tembo
wanalindwa, Tanzania imetenga zaidi ya asilimia 24 ya ardhi yake kwa ajili ya
uhifadhi.
Kipaumbele cha Mpango Mkakati wa uhifadhi ni pamoja na; kulinda
shoroba za wanyamapori hususani Tembo; kupunguza migogoro kati ya wananchi na Tembo;
kufanya tafiti za uhifadhi wa tembo na kushirikisha wadau mbalimbali katika
kuhifadhi Tembo. Serikali imekua ikifanya shughuli za uhifadhi wa
wanyamapori kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za kiserikali,
mashirika ya kimataifa kama WWF, taasisi zisizo za kiserikali, wafanyabiashara,
taasisi za kidini na wananchi kwa ujumla.
Naye mkurugenzi mkazi wa WWF Tanzania Dr. Amani Ngusaru
amesema Tembo ana mchango mkubwa kiikolojia pamoja na kusaidia uwepo na ustawi
wa viumbe wengine akiwemo binadamu.
Kumekuwa na changamoto katika utekelezaji wa kazi ya
kumlinda Tembo Ikiwemo ujangili, ukame, uhaba wa fedha, uchache wa watumishi na
vitendea kazi, ushirikiano hafifu wa wadau katika uhifadhi wa wanyamapori;
uchomaji moto misitu ambayo ni makazi ya wanyamapori; ubovu wa miundombinu
katika maeneo yaliyohifadhiwa na matumizi haramu ya wanyamapori.
Katika
kukabiliana na changamoto Wizara imepanga mikakati mbalimbali kupitia Mpango
Mkakati wake 2013 – 2016. Mikakati hiyo ni pamoja na kuendelea kuajiri
watumishi wapya, mwaka 2014 waliajiriwa askari wapya 430 na mwaka 2015
tunategemea kuajiri askari 500; kuongeza ushiriki wa wadau mbalimbali ikiwepo
WWF na kushirikiana na nchi jirani (Cross border collaboration), kununua
vitendea kazi; kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi, kupunguza quota ya uwindaji
wa Tembo kutoka 200 hadi 100; kutumia teknolojia ya kisasa kuthibiti ujangili,
kuimarisha usimamizi wa rasilimali za wanyamapori kwa kufanya doria ndani na
nje ya maeneo yaliyohifadhiwa. Vilevile, miundombinu, vitendea kazi na huduma
zitaboreshwa kwa watumishi kwenye hifadhi za Taifa, mapori ya akiba na kikosi dhidi
ya ujangili.
Wizara
ya Maliasili na Utalii katika kuadhimisha siku ya Tembo kitaifa ikishirikiana
na WWF Tanzania zinatoa wito kwa raia wema kutoa taarifa Makao Makuu ya Idara ya wanyamapori, Tanapa,
Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro, Mashirika ya kimataifa na/au kwenye kituo cha Polisi kilicho karibu
ili kufanikisha kukamatwa kwa majangili na wale wote wanaojihusisha na
biashara haramu ya nyara, hususan meno ya tembo, pembe za faru, nyama ya pori na
wanyamapori hai wakiwemo ndege, duma na nyani. Tushirikiane kuzuia uharibifu wa
rasilimali zetu ili kulinda urithi wa dunia.
IMETOLEWA
NA
KATIBU
MKUU
Post a Comment