Kwa
masikitiko na mshangao mkubwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepokea
taarifa ya kutokea kwa mauaji katika Kijiji cha Mangucha Halmashauri ya
Wilaya ya Tarime wakati wa Kampeni za Uchaguzi ambapo Bwana Mwita Bhoke
Waitegi aliuawa.
Tume
inakemea vikali na kwa nguvu zote ukiukwaji wa Maadili unaopelekea
uvunjifu wa amani na kusababisha vurugu ambazo hatimaye wakati wa
Kampeni mauaji yametokea.
Kwa
mujibu wa Taarifa zilizopokelewa na Tume, pamoja na mambo mengine, kwa
kiwango kikubwa kifo kilisababishwa na fujo, vurugu na kurupushani kati
ya wafuasi wa Vyama vya CCM na CHADEMA.
Vurugu
na fujo hizo ni kinyume kabisa cha Maadili ya Uchaguzi ya 2015
yaliyotiwa saini na Vyama vyote vya Siasa vilivyosajili tarehe
27/08/2015.
Kwa
mujibu wa Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka
2015 kifungu cha 2.2 (a) Viongozi wa Vyama vya Siasa, Wagombea wao
hawatakiwi kufanya fujo au kusababisha vurugu ya aina yoyote katika
mkutano wa Chama kingine, (b) Viongozi wa Vyama vya Siasa, Wagombea wao
hawatakiwi kutumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli, udhalilishaji na
vitisho au lugha inayochochea uvunjaji wa amani, au kuashiria ubaguzi wa
kijinsia, ulemavu au maumbile, kwenye mikutano ya Kampeni.
Aidha,
Maadili hayo kifungu (c) kinaeleza kuwa mtu yeyote haruhusiwi kuwa
na/au kubeba silaha yoyote ikiwa ni pamoja na silaha za jadi au zana
yoyote inayoweza kumdhuru mtu katika mkutano wa Kampeni au mkusanyiko
wowote wa kisiasa, na kifungu (d) kinaeleza kuwa hairuhusiwi kuwa na/au
kubeba sanamu, kinyago au kitu chochote ambacho kinaonyesha
kudhalilisha, kukebehi au kufedhehesha Chama kingine cha Siasa au
Kiongozi wake au Serikali katika mkutano au mkusanyiko wowote wa
Kisiasa.
Kwa
vile kutokana na kutozingatiwa kwa Maadili ya Uchaguzi, 2015 kifo
kimetokea na baadhi ya wananchi, wanachama wa Vyama hivi vya Siasa
kuumia, Tume kwa mara nyingine inakumbusha na kusisitiza Vyama vyote vya
Siasa na Wanachama wao kuzingatia Maadili ya Uchaguzi ya 2015.
Tume
pia imepata taarifa ya kuwepo kwa baadhi ya Vyama vya Siasa ambavyo
vinaandaa vijana zaidi ya 1500 na kuwapa mafunzo ya kijeshi ili kufanya
vurugu wakati wa Uchaguzi.
Taarifa hizo japo ni za upande mmoja Tume inaliomba Jeshi la Polisi kuchunguza suala hilo na kuchukua hatua ili kudhibiti viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani. Hili nalo, Tume inalikemea kwa nguvu.
Taarifa hizo japo ni za upande mmoja Tume inaliomba Jeshi la Polisi kuchunguza suala hilo na kuchukua hatua ili kudhibiti viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani. Hili nalo, Tume inalikemea kwa nguvu.
Chama chochote hakiruhusiwi kuwa na vikundi vya aina hii. Ni kinyume cha Sheria na Maadili ya Uchaguzi.
Imetolewa na:
Mh. Jaji (Mst.) Damian Z. Lubuva
MWENYEKITI
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI
Tarehe 18 Septemba, 2015
Post a Comment