Matokeo ya utafiti wa Twaweza kuhusu Uchaguzi Mkuu yamepingwa na wasomi, wanaharakati na wanasiasa, akiwamo mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa ambaye ameuponda na kueleza kuwa matokeo halisi yatapatikana Oktoba 25.
Utafiti
huo unaonyesha kuwa kama kura zingepigwa kati ya Agosti na Septemba,
mgombea wa CCM, Dk John Magufuli angeibuka na ushindi wa asilimia 65,
wakati Lowassa angepata asilimia 25.
Lakini
wadau wanasema utafiti huo haujaakisi hali halisi inavyoonekana kwenye
mikutano ya kampeni, ambayo inaonyesha wawili hao wanachuana vikali
kutokana na kukusanya mashabiki wengi.
“Watanzania tusipumbazwe na tafiti ambazo hatujashiriki. Tushiriki kwa mafuriko Oktoba 25, majibu ya kweli tutayapata,” alisema Lowassa kwenye akaunti yake ya twitter.
Kwenye
mkutano wa kampeni uliofanyika Jimbo la Ndanda jana, ikiwa ni muda
mfupi baada ya Twaweza kutangaza matokeo ya utafiti huo, Lowassa alisema
anashangazwa kwa kuwa wananchi wanaomuunga mkono ni wengi.
“Kuna
utafiti wa kura ya maoni umetolewa ukisema eti Magufuli amepata
asilimia 65 na mimi 25. Nawashangaa kwa kuwa wanaoniunga mkono wako
wengi,” alisema Lowassa na kuwaoji wananchi wangapi watampigia kura katika uwanja huo.
Huku wakishangilia wananchi hao walimjibu Lowassa “Tutakupigia” huku wakinyoosha mikono juu.
Baadaye Lowassa alisema: “Tutawajibu kwenye kura tarehe 25 na hamuwezi kukosea kwa kuwa mnaziona mvi hizi. Nangojea mafuriko ya kura kutoka kwenu.”
Lowassa
alijiondoa CCM baada ya jina lake kuenguliwa na Kamati Kuu na kujiunga
na Chadema Julai mwishoni. Chama hicho kilimpa fursa ya kugombea urais,
akiungwa mkono na vyama vingine vya NLD, NCCR-Mageuzi na CUF vinavyounda
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Maoni ya Wadau
Maoni ya Wadau
Mbali na Lowassa kutokubaliana na matokeo ya utafiti huo, watu mbalimbali pia wameupinga utafiti huo.
Mwenyekiti
wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Profesa Penina Mlama amesema
matokeo ya utafiti wa Twaweza hayalingani na hali halisi ya kisiasa
inavyoendelea nchini.
“Kile kinachoonekana huko nje ni picha mbili tofauti,” alisema Profesa Mlama.
Amesema
licha ya kwamba Twaweza wamefanya utafiti huo kwa kutumia vigezo vyao,
matokeo yasingeonyesha tofauti kubwa kati ya wagombea hao.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Profesa Kitila Mkumbo ambaye alisema: “Matokeo halisi tutapata baada ya wananchi kupiga kura Oktoba 25.”
Wakati
wadau hao wakizungumzia tofauti ya uhalisia wa hali ilivyo na matokeo
ya utafiti, mhadhari wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Paul Loisulie
aliwataka wapinzani kutopuuzia maoni hayo ya wananchi, hasa kutoelewa
nafasi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Wanaweza
wakapuuzia utafiti huo kwa kuwa unampa ushindi Dk Magufuli, lakini sio
hili la Ukawa si chama cha siasa kilichosajiriwa kwa sababu itakapofika
Oktoba 25 watu wanaweza kwenda kwenye karatasi ya kupigia kura kutafuta
Ukawa,” alisema.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema licha ya
kukosa uhalisia kwa hali ya kisiasa iliyopo, matokeo hayo yanaweza kuwa
changamoto kwa Ukawa, kujipanga upya na kuangalia mbinu za kuongeza
ushawishi kwa siku zilizobakia.
Hata hivyo, Mbunda alisema matokeo hayo hayawezi kutabiri ushindi wa urais kati ya Dk Magufuli na Lowassa.
“Haileti
mantiki kwa mashabiki wa Lowassa halafu utafiti uonyeshe amepata
asilimia 25 ya kura. Ningependa ufanyike utafiti mwingine ili kuondoa
maswali yaliyopo kwa sasa,” alisema.
Wakili
wa kujitegemea na makamu mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdalah Safari
alisema matokeo hayo ya Twaweza ni sehemu ya CCM kutapatapa na utafiti
aliouita “feki na wa kutengeneza”.
Profesa Safari alisema haiingii akilini, muungano wa Ukawa na Lowassa ukatoa asilimia 25.
“Nusu
ya vijana tumeshiriki kampeni za kuhakikisha wanajiandikisha kupiga
kura na hata utafiti wetu unaonyesha CCM watashindwa. Kwa hivyo
wanatafuta kurubuni taasisi ziwatengenezee uhalali wa kukubalika,” alisema Profesa Safari.
Maoni
kama hayo yalitolewa na Profesa Gaudence Mpangalla kutoka Chuo Kikuu
cha Ruaha ambaye alisema ni matokeo ya propaganda za CCM.
Alisema
Lowassa akiwa CCM, matokeo ya utafiti wa taasisi hiyo yaliyonyesha
alikuwa anaongoza kwa ushawishi katika nafasi ya urais.
“Nina shaka na hiyo methodolojia waliyoitumia kwa kweli,” alisema Profesa Mpangalla.
Dk James Jesse, mhadhiri wa UDSM, Kitivo cha Sheria pia alikuwa na shaka na utafiti huo.
“Matokeo haya yanaonesha walihoji watu fulani walioandaliwa na hawakuhoji watu mchanganyiko,” alisema.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (Teku), Stephen Mwakajumulo alisema
kama Twaweza iliweka vigezo sahihi vya utafiti, basi upo uwezekano wa
majibu kuwa sahihi.
“Kumbuka
mwaka 2005 ilifanya utafiti wa aina hiyo na kueleza kwamba mgombea wa
CCM Rais Jakaya Kikwete angeshinda kwa asilimia 80 na matokeo yake
yakawa kweli,’’ alisema na kuongeza mara nyingi utafiti unafanyika ili kutafuta mwelekeo wa ukweli kwa kutumia vigezo muhimu.
Wanasiasa
Mgombea
ubunge wa Jimbo la Bumbuli (CCM), January Makamba alilalamika kuwa
utafiti huo umewapunguzia asilimia za ushindi kwani wanaamini itakuwa
zaidi ya asilimia 65.
“CCM
haishangazwi na matokeo hayo kwa sababu, Magufuli amefika maeneo ya
vijijini zaidi kuliko mgombea yeyote, ameeleza sera zinazoeleweka na ana
sifa za uadilifu lakini wanaojadili mabadiliko hawaendani na historia
yao, mwonekano wao ndiyo sababu wananchi wamekatishwa tamaa na hoja
zao,” alisema ambaye wiki iliyopita alitangaza matokeo ya utafiti
uliofanywa na taasisi ambayo hakuitaja unaoonyesha kuwa Magufuli
anaongoza kwa asilimia 69.
“Mafuriko
ya (mgombea wa NCCR-Mageuzi mwaka 1995) Agustine Mrema na (mgombea wa
Chadema 2010) Dk Willibrod Slaa hayajawahi kutokea hadi sasa. Haya
yanayojitokeza kwa Lowassa badala ya kuwasaidia yanawadhalilisha kwa
kuwa mgombea wao hana uwezo hata wa kujieleza jukwaani kwa hivyo matokeo
hayo yanaakisi ukweli wa hali halisi iliyopo...sasa wanaopinga na wao
waje na utafiti wao tuone.”
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kabla ya kuzungumzia utafiti huo
wataujadili kwa kina kuangalia mazingira yaliyotumika kuufanya.
“Kwanza tuone ulivyofanyika ndiyo tutatolea ufafanuzi,” alisema.
Katibu Mkuu wa chama cha Sauti ya Wananchi (Sau), Ali Kaniki alisema matokeo hayo hayawezi kuaminika kwa asilimia kubwa.
“Kuna
taasisi Uingereza walifanya utafiti kama huo na chama cha Labour Party
kilioneokana kuongoza sana, lakini hadi matokeo yanatangazwa kilianguka
vibaya,” alisema.
“Lakini
inatakiwa kuheshimu utafiti huo na tusidanganyike na hoja za mafuriko.
Wanaojitokeza kwenye mafuriko siyo wote wanaopiga kura.”
Hata
hivyo, Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muhabi alisema
matokeo hayo ni chanzo cha kuashiria hatari ya machafuko, hivyo
kusingekuwa na sababu ya kutoa utafiti huo kwa muda mfupi uliosalia.
“Ukiangalia
ndani yake kuna propaganda za kisiasa zinazochezwa na CCM na inaweza
kutuletea shida. Watu wako kwenye presha sana nadhani ingekuwa sahihi
kusubiria uchaguzi ufanyike tu.”
Mwenyekiti
wa UDP mkoani Dar es Salaam, Joachimu Mwakitinga alisema hakuna
uhusiano wa hali halisi na matokeo ya asilimia 65 kwa Magufuli.
Mwakitinga ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Mamlaka na Taratibu za
Uendeshaji Uchaguzi, alisema matokeo hayo ni uchochezi wa kampeni
unaoweza kusababisha madhara makubwa kwenye Uchaguzi Mkuu.
Wanaharakati
Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), Dk.Hellen
Kijo-Bisimba alisema sampuli iliyotumika kwa matokeo ya utafiti huo
inaweza kuwa imeathiriwa na mazingira ya maeneo husika. “Wakati
mwingine sampuli inaweza kudanganya na kuwa tofauti kabisa na uhalisia
wa hali ilivyo na wakati mwingine kuelezea uhalisia wenyewe.”
Mkurugenzi
wa Taasisi ya Sikika, Irinei Kiria alisema sampuli ya Watanzania 1,848
ni idadi ndogo na isiyoakisi Watanzania milioni 23 wanaotarajiwa kupiga
kura mwaka huu.
“Lakini
pia, wiki mbili tangu kufanyika uchaguzi huo ni muda unaoweza kubadili
upepo mkubwa wa kisiasa kwa hivyo haiwezi kuwa matokeo halisi kwa hali
ya sasa.”
Kiria
alisema matokeo ya utafiti huo kwa Lowassa na Magufuli ni sawa na usiku
na mchana kutokana hali halisi ya kisiasa ilivyobadilika katika
uchaguzi wa mwaka huu.
Mratibu
wa Mtandao wa Watetezi za Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo
Olengurumwa alisema matokeo na hali ya kisiasa nchini yanaonyesha
tofauti kubwa.
Mwenyekiti
wa mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoa wa Arusha (Angonet),
Petro Ahham alisema utafiti ni mzuri, lakini pengo la ushindi wa CCM ni
kubwa sana.
“Kwa
hali ilivyo sasa huwezi kusema kuna mshindi wa asilimia 65, labda
tuelezwe walioulizwa maswali ni waliojiandikisha tu sio hawa tunaowaona
kwenye mikutano,” alisema.
Mwanafunzi
wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, Alline Ngirwa alisema utafiti
huo umeonyesha ni maeneo gani hasa ambayo wananchi wanakerwa, kwa hivyo
utawasaidia katika kipindi hiki wanapojiandaa kuamua.
“Wananchi
wanakerwa na huduma za afya, ukosefu wa maji na elimu duni. Kwa hiyo
matokeo ya utafiti huu yanatoa mwangaza kwa wapiga kura na wagombea juu
ya vitu wanavyohitaji kwenye serikali ijayo,” alisema Ngirwa.
Mkurugenzi
wa taasisi ya Compas Communication, Maria Salungi alisema utafiti huo
si matokeo ya uchaguzi na kwamba katika kipindi kilichobaki kuelekea
Uchaguzi Mkuu, yanaweza kubadilika.
“Haya
sio matokeo ya uchaguzi ni maoni ambayo yanaweza kubadilika kulingana
na wagombea watakavyoendelea kufahamika zaidi kwa wananchi, hivyo jamii
isipokee kama ndio matokeo halisi,” alisema
Alisema
katika utafiti huo, wengi waliohojiwa walitoa majibu kulingana na
wagombea kufahamika zaidi, kutokana na majina yao kutajwa mara kwa mara
ikiwemo kwenye vyombo vya habari na mabango.
Alishauri
vyama vinavyounda Ukawa kuwaelimisha wananchi ambao wanaamini kwamba
siku ya kupiga kura, watachagua Ukawa chama ambacho hakipo.
Post a Comment