Gazeti
la Mwananchi la Tarehe 14/9/2015 toleo namba 5529 ukurasa wa 25
liliandika habari kuhusu Mwenge wa Uhuru chini ya kichwa cha Habari
“Anayeumba Mwenge wa Uhuru” huyu hapa
Wizara
ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo (WHVUM) ambayo ndiyo yenye
dhamana ya Mwenge wa Uhuru inapenda kuufahamisha umma kwamba habari hiyo
sio ya kweli na ni ya upotoshaji.
Mwenge
wa Uhuru ni Chombo maalum na moja ya alama nyeti za Taifa la Tanzania.
Mwenge wa Uhuru ni chombo chenye hadhi ya pekee na hivyo dhamana ya
kukitengeneza haiwezi kupewa mtu binafsi kama alivyodai Ndugu Shaban
Mwinchumu na kuandikwa kwenye gazeti la Mwananchi. Kwa sababu hiyo,
kitendo cha kutengeneza au kuigiza chombo chenye dhana na falsafa ya
Mwenge wa Uhuru ni ukiukwaji wa sheria za nchi.
Wizara
ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ingependa kuufahamisha umma
kuwa Mbio za Mwenge wa Uhuru zilianzishwa rasmi mwaka 1964 na sio mwaka
1961 kama ilivyoandikwa katika toleo lililotajwa. Ieleweke kwamba, Mbio
za Mwenge wa Uhuru tangu kuanzishwa kwake zimekuwa zikitumika katika
kuwahamasisha wananchi wa Tanzania kuendelea kujenga upendo, umoja na
mshikamano wa Kitaifa bila ya kubaguana kwa misingi ya kidini,rangi,
jinsia, ukabila na itikadi za kisiasa.
Vilevile,
Mbio za Mwenge wa Uhuru zimekuwa zikitumika kuhamasisha na kuchochea
shughuli mbalimbali za maendeleo ya wananchi kiuchumi na kijamii kupitia
kwenye ujumbe maalum unaotolewa kila mwaka na miradi ya maendeleo
inayobuniwa .
Wizara
pia, inapenda kuufahamisha umma wa Watanzania kuwa michango ya fedha
inayotolewa na wananchi kwa ajili ya Mbio za Mwenge wa Uhuru si kwa
ajili ya kugharamia mafuta ya Mwenge wa Uhuru unaokimbizwa kama
ilivyodaiwa na gazeti la Mwananchi. Fedha zinazochangwa ni kwa ajili ya
kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo hubuniwa na
wananchi wenyewe. Aidha, michango hiyo hutolewa kwa hiari kutoka kwa
mwananchi mmojammoja, Vikundi, Taasisi za Umma na Binafsi, Wadau wa
Maendeleo, Serikali Kuu na Halmashauri za Wilaya.
Kwa
Taarifa hii Wizara inasisitiza kuwa madai ya Ndugu Shaban Mwinchumu ni
ya upotoshaji na hayana uhusiano wowote na masuala ya Mwenge wa Uhuru.
Pia, Ndugu Shaban Mwinchumu hajawahi kupewa kazi ya kutengeneza Mwenge
wa Uhuru anayodai kuifanya kwa muda mrefu kupitia Wizara ya Kazi, Ajira
na Manendeleo ya Vijana kwani hakuna Wizara hiyo kwenye orodha ya Wizara
za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwisho
kabisa Wizara inawataka waandishi wa habari na wahariri wa vyombo vya
habari kuandika habari kwa usahihi zenye kujenga Umoja wa Kitaifa kwa
kupata ufafanuzi wa kila upande ili habari itoe picha halisi badala ya
kuegemea upande mmoja kwani kwa kuegemea upande mmoja hupotosha jamii na
si maadili ya taaluma ya habari.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Post a Comment