Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto
Kabwe amesema ahadi ya CCM ya kutoa mgao wa Sh50milioni
kwa kila kijiji nchini, ni dalili za kutawanya ufisadi kwa kutumia
fedha hizo.
Katika
ilani ya Uchaguzi Mkuu 2015, CCM imeeleza kuwa
itaielekeza Serikali yake itenge Sh50milioni kwa kila kijiji kama Mfuko
wa Mzunguko kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wajasiriamali kupitia
Ushirika wa Kuweka na Kukopa (Saccos)
kwenye maeneo hayo.
Katika ukurasa wake wa Facebook, Zitto (pichani) amepinga
sera hiyo akisema ni ubabaishaji.
“Sera ya kumwaga Sh50 milioni kwa kila kijiji ni moja ya sera za kutawanya ufisadi nchini wakati
hatujui mabilioni ya JK yaliishia wapi,” alisema Zitto akirejea Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi
ulioanzishwa na Serikali ya Awamu ya Nne uliojulikana zaidi kama Mabilioni ya Kikwete.
Mpango huo ulikumbwa na matatizo wakati wa utekelezaji wake, kutokana na walengwa
kutoandaliwa vizuri kutumia fedha wanazopewa, na Serikali kutokuwa na utaratibu wa
kuwafutilia wanufaika wa mfuko huo.
Akihoji kuhusu mpango huo wa kugawa Sh50 milioni kwa kila kijiji, Zitto alionyesha wasiwasi
kuhusu vyanzo vya mapato vitakavyowezesha kupatikana kwa fedha hizo ili kusaidia vijana na
wanawake.
“Tanzania ina zaidi ya vijiji 12,000, itahitaji kupokea takribani Sh600 bilioni.
Fedha hizo zitatoka
wapi?” alihoji katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake huo, Septemba 20, mwaka huu na
kuongeza:
“Tukatae ubabaishaji huu kwenye uchumi wa nchi yetu. Watanzania wanataka hifadhi ya jamii ili
wapate afya bure na mafao mengine.”
Akitetea vyanzo vya mapato vitakavyowezesha utekelezaji wa sera hiyo, Mjumbe wa Kamati ya
Kampeni ya CCM, January Makamba alisema ongezeko la ukusanyaji wa mapato kila mwezi kwa
Serikali linaweza kufanikisha utekelezaji wa ahadi hiyo.
Alisema kuna wizara zilizokuwa zikipata mgao wa zaidi ya Sh800 bilioni, hivyo mfuko huo wa
kijiji hautaweza kukosa mabilioni yatakayohitajika.
“Kuhusu utaratibu wa kudhibiti fedha hizo utawekwa wazi, kutakuwa na kamati ya kijiji ambayo
itakuwa imejiwekea utaratibu wake.
Nchi ya Thailand ilikuwa na mfuko kama huo na ulitokea
kuwa mfuko mkubwa sana duniani.
Kwa hiyo hoja hiyo wapinzani wanaona tumewapiga bao na
ndiyo sababu ya kupinga bila hoja ya msingi,”alisema.
Post a Comment