Katika
hali ya kustaajabisha, kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Ramadhan,
ambaye mwishoni mwa wiki amejikuta akishushiwa kipigo kwa kudhaniwa
kuwa kibaka, alisalimika baada ya kuanza kusali kwa kuwashtakia kwa
Mwenyezi Mungu waliokuwa wakimpiga, akisema hakuwa na hatia na ghafla
watu hao kusitisha kipigo.
Ramadhan alikutana na hali hiyo baada ya kutuhumiwa kuiba redio kutoka katika duka moja lililopo stendi ya daladala mjini hapa.
Ilidaiwa
kuwa kibaka huyo baada ya kuchukua redio hiyo alianza kukimbia kutokana
na mwenye duka kumwitia mwizi na Ramadhan akawa mmoja kati ya watu
waliokuwa wakimfukuza, kabla ya mdokozi huyo kujichanganya na watu hivyo
kutotambulika kirahisi.
Baada
ya kuona hivyo, wananchi hao wenye hasira walimgeukia kijana huyo na
kuanza kumpa kipigo kama cha mbwa mwizi kwa vile nguo zake zilikuwa
zimefanana na zile zilizokuwa zimevaliwa na kibaka aliyekuwa akifukuzwa.
”Ewe
Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, kwa msaada wako niepushie na mtihani
huu niliosingiziwa kwani wewe ndiwe unayejua ukweli wa tukio hili,” mtu
huyo alisikika akisema kufuatia kipigo alichokuwa akikipata, baada ya
kukimbia na kwenda kujibanza pembeni ya duka linalouza vinywaji baridi.
Kufuatia
maneno hayo, watu wote walijikuta wakisitisha zoezi la kumpiga na mmoja
wa bodaboda wa kijiwe cha Juwata aliingia kati na kusema; “Jamani huyu
jamaa anaonekana siyo mwizi na ni mtu wa dini, hivyo naomba aliyeibiwa
ajitokeze na kutoa ushuhuda,” alisema na hakuna aliyejitokeza.
Kijana Ramadhan akishusha dua zito baada ya kushushiwa kipigo kikali.
Baada
ya kuona hivyo, kijana huyo aliwataka watu hao kumuacha aende zake huku
baadhi ya walioshiriki kumpiga wakimuomba msamaha mtu huyo aliyekuwa
akivuja damu mwili mzima.Akizungumza na mwandishi wetu, Ramadhan alisema
alishuka kwenye daladala na kuungana na watu waliokuwa wakimfukuza
mwizi kabla hawajamgeuzia kibao kutokana na nguo zake kufanana na za
kibaka.
“Mwizi
alijichanganya na watu ndipo nikageukiwa mimi, nikakimbilia hapa dukani
kwa Mhindi na kuamua kuomba msaada kwa Mungu kwa kuomba na akafanikiwa
kuniokoa,” alisema kijana huyo.
Katika
stendi ya daladala, mfanyabiashara wa duka lililoibiwa,
aliyejitambulisha kwa jina la Shaaban, alisema alikuwa amekwenda
kutafuta chenchi, ndipo alipomuona mtu akiondoka na redio yake na yeye
akapiga kelele za mwizi, akadondosha bidhaa hiyo na kukimbia, lakini
akashindwa kuungana na watu kumkimbiza kwa vile hakukuwa na mtu mwingine
dukani.
Post a Comment