Chadema imewataka wananchi kujumlisha matokeo yote yatakayotolewa kwenye vituo vya uchaguzi na kuyasambaza badala ya kusubiri kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Akizungumza
jana kwenye mkutano wa kampeni Jimbo la Kikwajuni mjini Unguja, Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema – Bara, John Mnyika aliwataka wananchi hao
kutoondoka kwenye vituo vya kupigia kura, bali wasubiri hatua 200 kutoka
vituo hivyo kupiga kura ili kulinda kura zao.
“Mjitokeze
kwa wingi kupiga kura na baada ya kupiga kura mrudi nyuma hatua 200
kulinda ushindi wenu. Nina uzoefu na hili kwa sababu lilitokea jimboni
kwangu mwaka 2010,” alisema na kuwataka Wazanzibari wasikubali kuibiwa kura zao.
Akizungumza
kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema
(Bawacha), Halima Mdee aliyeambatana na Mnyika katika kampeni za
kumuunga mkono Salum Mwalimu anayegombea ubunge wa Jimbo hilo la
Kikwajuni, aliwaeleza wananchi kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni wa muhimu
kwa sababu wakikosea kuchagua itawagharimu miaka mingine mitano.
Alisisitiza
kuwa kama wanataka kuwa na mamlaka kamili, basi wamchague Edward
Lowassa na Maalim Seif Sharif Hamad ili washirikiane kuanza upya
mchakato wa Katiba. Aliwataka pia wamchague Mwalimu kuwa mbunge wao ili
akaongeze nguvu katika mapambano bungeni na kuitetea Zanzibar.
“Moja
ya ajenda kuu za Ukawa ni kuwa na Muungano wa serikali tatu, Zanzibar
ikiwa ni mamlaka kamili. Wachagueni viongozi hawa ili mpate watetezi
wenu watakaowaletea maendeleo,” alisema Mdee.
Awali,
akiomba kura kwa wananchi, Mwalimu aliahidi kwamba akichaguliwa,
atahakikisha anasimamia kikamilifu masilahi ya jimbo lake na Zanzibar
kwa ujumla.
Alisisitiza
kuwa anatambua matatizo ya jimbo hilo na kuahidi kujitoa katika
kuyatatua kwa sababu naye pia ni sehemu ya jamii hiyo. Aliwataka
wananchi kumpigia kura kwa wingi Oktoba 25, ili atimize ahadi zake.
Post a Comment