Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Hotuba Ya Mh. Edward Lowassa Aliyoitoa Leo Tarehe 24 Kwenye Viwanja Vya Jangwani Jijini Dar Wakati Wa Kufunga Kampeni Za Urais


 NDUGU
Watanzania wenzangu
•Ndugu wanachama, marafiki na wapenzi wa CHADEMA
•Ndugu Viongozi wakuu wa kitaifa na wanachama wa vyama vyetu vinne vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
•Ndugu  Wana mabadiliko na watetezi wa kweli wa maendeleo
•Mabibi kwa Mabwana

Salaam Aleikum
Bwana Yesu Asifiwe
Tumsifu Yesu Kristo

NIANZE hotuba yangu hii ya kuhitimisha ziara ndefu za kampeni, zilizonichukua mimi na timu yetu yote ya kampeni katika kaya, vijiji, kata, tarafa, wilaya na mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar katika kipindi chote cha siku takriban 60.

Kama nilivyosema jana nilipozungumza na Watanzania kupitia katika redio, televisheni na kwa njia tofauti za mawasiliano, tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyetuvusha salama.

Leo tunahitimisha safari ngumu, ndefu, iliyojaa miiba, milima na mabonde tukitembea kifua mbele kwa namna mamilioni ya Watanzania walivyojitokeza kutuunga mkono.

Kwa uchungu na masikitiko makubwa tunahitimisha safari ya kampeni, tukiwa na kumbukumbu mbichi vichwani ya kuwapoteza wenzetu kadhaa.

Ni juzi tu, wiki hii hii tumemlaza katika nyumba yake ya milele Mzee wetu, Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA, Emmanuel Makaidi.

Tumewapoteza njiani kabla yake, Deo Filikunjombe, Dk. Abdallah Kigoda, Mama Celina Kombani, kijana wetu Mohamed Mtoi na Estom Mallah, wote hawa walikuwa wagombea ubunge.

Si hao tu, tukampoteza pia mmoja wa wanasiasa ambaye ni muasisi wa mageuzi nchini, Mwenyekiti wa chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila.

Wote hao na wengine ambao sikuwataja hapa tunamuomba Mwenyezi Mungu awapumzishe kwa amani. (Tusimame dakika moja kuwakumbuka marehemu wote waliopoteza maisha katika kipindi hiki cha kampeni)

Ndugu zangu
Mimi na mgombea mwenza, Juma Haji Duni tumeona na kujifunza mengi. Tumejiandaa kikamilifu kuijenga Tanzania Mpya. Tanzania ya ndoto ya waasisi wetu.
 
Ndugu Watanzania wenzangu
Katika ziara hizi, nimeshuhudia vuguvugu la mabadiliko, kiu na ari ya Watanzania kuyapokea mabadiliko hayo.
 
Lakini pia nimejionea shida zinazowakabili wananchi hao.Nimesikia na nyakati nyingine kujionea kilio chao cha kunyanyaswa na kunyimwa haki zao na watendaji wa serikali na baadhi ya vyombo vya dola.
 
Nimekisikia kilio chao cha umaskini, afya na elimu duni.
Nimekisikia kilio kikubwa cha vijana kukosa ajira na matarajio ya kesho bora.
 
Nimesikia rai za Watanzania na ndoto zao za kupata maendeleo, maji safi, makazi bora na barabara madhubuti.
Nimesikia malalamiko ya wakulima na wafugaji kukosa maji, ardhi na namna wanavyotozwa ushuru na kodi za kero katika mazao yao.
 
Nimesikia kilio cha madaktari, wauguzi, walimu, askari na watumishi wa taasisi za umma kuhusu mazingira magumu ya kazi, kodi za juu na maslahi duni.
 
Nimesikia kilio cha wafanyabiashara wadogo wadogo kuhusu ugumu wa mazingira ya kufanyia shughuli zao, kodi kandamizi na kukosa mitaji.

Nimesikia kilio cha wanawake kuhusu haki zao na ushiriki wao mdogo katika shughuli za kiuchumi.

Nimesikia kilio cha wazee na wastaafu wasio na bima ya afya, wanaolipwa pensheni isiyokidhi mahitaji yao na ugumu wa maisha yao uzeeni.
 
Tumekisikia kilio dhidi ya rushwa na ufisadi uliokithiri
Tumekisikia kilicho cha Watanzania juu ya udhaifu wa kiuongozi na utawala dhaifu wa CCM ulioshindwa kuondoa umaskini
 
Tumekutana na vilio vya watu walioonewa, kunyanyaswa na kupuuzwa na namna haki za raia zilivyopuuzwa.
 
Jibu langu ni fupi na lile lile. TUMEONA, TUMESIKIA, TUMEELEWA NA TUTATENDA.

Baba wa Taifa, alisema Uongozi ni kuonyesha njia. Tumejipanga vyema kuwaongoza Watanzania:
1.Kwanza tumejiandaa kuongoza mapambano ya dhati ya kuukataa na kuondokana na umaskini
 
2.Tumejipanga vyema kupiga vita rushwa na ufisadi kwa matendo na si kwa maneno matupu
 
3.Tumejizatiti kuliandaa taifa kwa ajili ya mapinduzi ya kweli katika elimu, kilimo, viwanda
 
4.Tumejiandaa vyema kuwaongoza Watanzania kuachana na mawazo ya kutegemea wafadhili na kuondokana na hulka za kuwa taifa ombaomba
 
5.Tumejipanga kufufua ari, dhamira na misingi ya kujenga taifa linalojitegemea kiuchumi.
 
6.Tumejiandaa vilivyo kuhakikisha tatizo sugu la ajira linakoma.
 
7.Tumeshaanza kufanya maandalizi ya kuhakikisha serikali tutakayoiunda itafungua fursa mpya za ajira za ndani na nje ya nchi kwa vijana wa Kitanzania
 
8.Tumejizatiti kisera na kimikakati kuwajengea Watanzania misingi na utayari wa kujiamini kifikra na kuchochea fikra za kizalendo
 
9.Tumejipanga na kujizatiti vyema kuleta mabadiliko na mapinduzi katika utendaji wa kazi serikalini
 
10.Tumejiandaa vyema kuijenga na kuiimarisha sekta binafsi na kuijengea mazingira bora ya ushindani
 
11.Tumejiandaa vyema kubadili na kuboresha maisha ya wajasiriamali wadogo kama wamachinga, bodaboda na mama ntilie wakue na kukomaa kibiashara.
 
12.Tumejipanga vyema kuhakikisha raslimali za taifa tulizonazo kama madini, gesi asilia na vivutio vya utalii vinaimarishwa na kuwanufaisha Watanzania kwanza na siyo wageni kama ilivyo sasa.
 
13.Tumejizatiti kuifanya Tanzania kuwa taifa la mfano kijamii, kiuchumi na kimaendeleo Afrika Mashariki na duniani kwa kudumisha sera yetu ya uhusiano wa kimataifa ili iwe na tija kwa Watanzania.
 
14.Tumejiandaa kuiondoa Tanzania kutoka katika kundi la mataifa maskini duniani kwa kuhakikisha tunaanza kutumia vyema raslimali zetu kujiletea maendeleo ya dhati.

Mambo hayo ndiyo msingi wa dhana ya mabadiliko tunayoyataka na kuyahubiri.

Tunaamini na kutambua kwamba, mabadiliko yanaanza na fikra.

Sisi wana mabadiliko tunaamini kwa dhati kwamba MAENDELEO NI AJENDA YA DHARURA kwa taifa na siyo jambo la lelemama.

Nimepata kulisema hilo siku zilizopita na nalisema tena leo kwamba, serikali nitakayoiongoza itaanzisha mchakato mahususi wa MCHAKAMCHAKA WA MAENDELEO.

Ni kwa sababu hizo, nawaomba Watanzania watuamini na wakubali kutupa dhamana ya kuliongoza taifa kwa njia ya kura kesho.

Tuliyoona yamechochea ari na dhamira yetu ya dhati ya kuomba ridhaa ya wananchi wa Tanzania na kushirikiana nao kuleta mabadiliko ya kweli.
 
Tulichokiona kimeniongezea ujasiri wa kuzidi kuuchukia umaskini

Tumejipanga vyema na kwa kutumia Ilani yetu, utayari wetu, uthubutu tulionao kuwaongoza Watanzania katika safari isiyo tu ya matumaini, bali ya mabadiliko, uhakika na ushindi

Ndugu zangu,
Mimi na nyinyi, tuna kila sababu ya kukubaliana na Mzee wetu, Kingunge Ngombale Mwiru, mmoja wa viongozi adhimu wa taifa hili ambaye amesema CCM imeishiwa pumzi, hivyo haina uwezo tena wa kutufikisha katika kilele cha mafanikio.

Mimi na ninyi Watanzania wenzangu tunapaswa kumuelewa kwa vitendo Baba wa Taifa, aliyesema chama kimoja kinachokaa kwa muda mrefu madarakani kinafikia hatua ya kujisahau. CCM ya leo iko mahututi.

Mimi na ninyi, tunapaswa kutambua kwamba maneno aliyopata kuyasema aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, marehemu Horace Kolimba kwamba 'CCM imepoteza dira' yana maana zaidi leo kuliko ilivyokuwa miaka 20 iliyopita.

Mimi na ninyi tunapaswa kujifunza kutoka kwa majirani zetu kama Kenya ambako wananchi walichukua hatua ya kuleta mabadiliko kwa njia za kidemokrasia mwaka 2002 na leo hii Wakenya hawamo tena miongoni mwa mataifa ya dunia ya tatu na maskini kama tulivyo sisi.
 
Mimi na ninyi, tunao wajibu wa kuikataa CCM kwa njia ya kura tukitumia kauli ya Mwenyekiti, Freeman Mbowe ambaye siku zote ametufundisha kwa kusema chama kile kile, chenye watu wale wale na ambacho kina sera, fikra na itikadi ile ile hakina uwezo wa kuongoza mabadiliko.

Ndugu zangu
Sina shaka hata kidogo kwamba, kwa njia ya sanduku la kura, Watanzania wameamua kuongoza mabadiliko ya maisha yao na ya taifa lao.
 
Ndugu zangu.
Rais Bora ambaye Tanzania inamhitaji wakati huu Watanzania wanapotaka mabadiliko ya kweli ni yule ambaye hata kabla hajakaa na wenzake na kuafikiana mambo ya msingi ya kisera, kiitikadi na kimaandeleo, yeye mwenyewe anayo maono ambayo anayaamini na kuyasimamia kwa dhati.
        Urais si kazi ya kubahatisha.
        Urais si jambo la pata potea.
        Urais ni wajibu na dhamana ya juu kabisa katika taifa
        Urais si mamlaka ya kutisha watu
        Urais ni wajibu wa kutoa dira ya taifa
Anayeomba urais anapaswa kuwa ni mtu aliyejiandaa na kuandaliwa vyema kifikra, kinidhamu, kimaadili kimikakati na kimaono

Ili uwe rais bora unapaswa kwanza kuwa mtumishi bora wa wananchi. Tunayo rekodi ya utumishi uliotukuka.

NDUGU zangu.
Ni jambo la kujionea haya sisi wenyewe kwamba miaka 54 baada ya Uhuru, Tanzania bado ni taifa masikini, tegemezi na linalozidi kudidimia.

Ni jambo baya zaidi kwamba, CCM kwa njia za hila na rushwa kinafanya juhudi kubwa kuzuia mabadiliko hayo.

Viongozi wakuu wa chama tawala, wanajaribu bila ya mafanikio kupandikiza mbegu mbaya vichwani mwa Watanzania ili wayakatae mabadiliko.

Watanzania tunalo chaguo moja tu, kukubali kubadilika.

Tunayo fursa ya kufanya kile kilichofanyika kwa mafanikio makubwa Zambia, Malawi, Kenya na kwingi kwingineko duniani.

Hatupaswi kusubiri hadi wananchi wakose subira na kupata hasira na kukosa uvumilivu wa kuingia mitaani na kuwang'oa watawala ving’ang’anizi wa aina ya CCM kama ilivyotokea, Libya, Tunisia, Irak na kwingineko.

Tunapaswa pia kujifunza kutoka nje ya Afrika ambako yako mataifa yaliyochupa kimaendeleo kwa sababu tu ya kupata uongozi madhubuti.

Siri wa mafanikio ya mataifa kama Malaysia, Korea Kusini, Thailand na Singapore ambayo miaka 50 tu iliyopita yalikuwa katika kiwango cha maendeleo kinachofanana na chetu ni UONGOZI wenye kuthubutu.

Ni fedheha kwetu kwamba, leo hii mataifa hayo ndiyo yamegeuka kuwa nchi wahisani, wafadhili na wawekezaji wakubwa.

Je, ni sahihi kuendelea kushangaa na kuyatamani maendeleo waliyopiga wenzetu hao? Jibu ni hapana.

Tunayo njia moja tu. Kuchukua hatua na kuleta mabadiliko yetu wenyewe.

Hatuwezi tukatoka hapa tulipo iwapo tutaendelea kuwakumbatia wale wale waliotukwamisha na ambao mawazo na mikakati yao ya kiuongozi ni ile ile iliyoshindwa kutukwamua kutoka hapa tulipo kwa zaidi ya miaka 54 sasa.

Tutakuwa tukijidanganya iwapo tutawaacha watu hao ambao kwa makusudi na kwa sababu zao walifikia hatua ya kukataa mawazo ya baadhi yetu ambayo yalikuwa yanaakisi maono, fikra na mikakati tofauti na ile ya kimazoea ambayo ndiyo hasa msingi wa kukwama kwetu.

Ndugu Watanzania wenzangu,
Naomba nimalizie kwa kusema yafuatayo ambayo nayasema tena leo kusisitiza kile ambacho nimekisema mara kadhaa:
1. Natambua kuwa uongozi ni dhamana. Mkinichagua kuwa Rais wenu, nitaienzi dhamana hiyo kwa utendaji uliotukuka na kwa uadilifu mkubwa.
 
2. Namuogopa Mungu, Nawaheshimu Watanzania. Naahidi kwamba nitawatumikia kwa uwezo, akili, uzoefu na nguvu zangu zote.
 
3.Watanzania wenzangu, mabadiliko yanaendana na kuthamini utu na kukataa hadaa ya hongo ili kuuza haki yako ya kuchagua.
 
4. Rushwa ya uchaguzi ndiyo sera ya CCM na ndiyo nyenzo yao ya kuwakandamiza Watanzania. Tukatae.
Tuchague mabadiliko, tuichague CHADEMA. Tuchague wagombea wa UKAWA.
 
5. Mabadiliko ni fikra. Ili tubadilike ni sharti tuanze sasa kufikiri na kutenda tofauti na ilivyo sasa.
 
6. Hatuwezi kuendelea kufikiri na kutenda kana kwamba hatuna dharura ya maendeleo. Tunaweza kujitegemea na kuleta maendeleo yetu wenyewe bila kutegemea wafadhili.
 
7. Nchi nyingi zimefanikiwa kuondoa umaskini katika kizazi kimoja. Tujifunze kutoka kwao. Tanzania pia inaweza. Tuchague Mabadiliko.
 
8. Tunapaswa tangu sasa kuwa taifa linalotumia rasilimali zake kwa ufanisi zaidi kujiendeleza na siyo kwa kuwanufaisha wageni na kuwafanya Watanzania watwana katika nchi yao.
 
9.  Umaskini si joho la ufahari. Tuukatae. Lazima tuache kuwa taifa ombaomba. Hakuna faraja katika umaskini.
 
10.  Mabadiliko hayawezi kuletwa na CCM. Miaka zaidi ya hamsini ya utawala wake Watanzania bado ni maskini. Tusitegemee kuwa wanalo jipya hii leo.

Ndugu zangu. Ilani yetu imechambua na kuainisha masuala ya msingi ambayo serikali tutakayoiunda itayasimamia na kuyatekeleza hatua kwa hatua.

1.Katiba
 – Hili ndiyo msingi wa umoja na mshikamano wetu ndani ya CHADEMA na ndani ya UKAWA.
- Tutalifanya kwa umakini mkubwa huku tukiimarisha misingi ya umoja na mshikamano wetu kitaifa.

2.Elimu
- Hiki ndicho kipaumbele chetu. Elimu Elimu Elimu
-Tunakwenda kuleta mapinduzi makubwa katika elimu.
-Mfumo mzima wa elimu yetu utafumuliwa
-Serikali nitakayounda itagharamia elimu bora tangu elimu ya msingi hadi Chuo Kikuu.

3.Ajira
-Hili ni tatizo sugu
-Tusipotatua tatizo hili tunatayarisha bomu litakalolipuka
-Ni kwa kutambua umuhimu wa ajira ndiyo maana nawatambua na kuwaheshimu vijana wabunifu – bodaboda, mama ntilie na wamachinga.
-Hawa si wa kubezwa. Hawa si wa kuburuzwa na kutishwa. Wanapaswa kuimarishwa ili waimarike kibiashara na kiuchumi
-Hawa kwangu ni mashujaa wa ajira.

4.Afya
-Huku kunatakiwa mapinduzi makubwa.
-Tumejizatiti kujenga Hospitali za Rufaa zenye hadhi katika kila wilaya
-Afya ndiyo msingi wa mafanikio yote mengine. Pasipo afya hakuna tija
         
5.Miundombinu
-Hii ndiyo injini ya uchumi wa mataifa yote yaliyoendelea
-Miundombinu ni zaidi ya barabaraba
-Miundombinu ni reli, bandari, viwanja vya ndege na kadhalika.
-Tumejipanga vyema kuimarisha eneo hili kwa kujenga reli mpya
 
6.Maji
-Hili ni tatizo mama
-Tunazidiwa hata na mataifa yaliyo jangwani. Hii ni aibu kubwa
-Tunakwenda kujenga upya miundombinu ya maji.
-atizo la uhaba wa maji litakuwa historia
 
7. Michezo, Sanaa na Utamaduni
-Tumekuwa wasindikizaji katika eneo hilo zima
-Tunayo mikakati ya kulikwamua taifa kutoka huko
-Tanzania haitakuwa tena kichwa cha mwendawazimu katika ulimwengu wa michezo

Tunayo Ilani ya CHADEMA na UKAWA inayotoa DIRA YA MABADILIKO katika sekta na maeneo yote hayo.

Ndugu zangu Watanzania. Mkituamini, mkatuchagua. Hatutawaangusha.
 
USHINDI WETU NI USHINDI WA WATANZANIA
NI WAKATI WA MABADILIKO
TUNAOMBENI KURA
Ahsanteni kwa kunisikiliza
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top