Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Tanzania inaimarisha Jeshi lake – Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), siyo kwa nia ya kumchokoza mtu ama nchi yoyote, bali kwa nia ya kulinda mipaka yake kwa sababu kila hatua ya maendeleo ina changamoto tofauti za ulinzi wa nchi.
Aidha, Rais
Kikwete amesema kuwa siyo uharibifu kutumia fedha nyingi kujenga Jeshi,
kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wanadai, kwa sababu ni wajibu wa
kila nchi kuhakikisha kuwa Jeshi lake linakuwa katika utayari wa
kukabiliana na uchokozi wa aina yoyote.
Rais vile vile amesema
kuwa uchumi wa Tanzania, na hasa uchumi mpya wa gesiasilia, ambayo ndiyo
itakuwa msingi mkuu wa uchumi na maendeleo ya Tanzania lazima ulindwe
kwa njia yoyote na kwa nguvu zote.
Rais Kikwete aliyasema hayo
Jumatatu, Oktoba 19, 2015 wakati alipozungumza katika Sherehe ya
Kukamilisha Mradi wa Ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kurushia Ndegevita
na Sherehe ya Kufungua Mradi wa Kuongeza Urefu wa Uwanja wa Ndegevita
katika Kituo cha Kijeshi cha Kamandi ya Anga cha Ngerengere, Mkoa wa
Morogoro.
Rais aliwaambia walioshuhudia sherehe hiyo akiwemo
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali
Mwinyi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange na Balozi
wa Jamhuri ya Watu wa China katika Tanzania Mheshimiwa Dkt. Lu Youquing
kuwa Tanzania inajenga Jeshi lake vizuri kwa ajili ya ulinzi wa mipaka
yake.
“Hatujengi Jeshi letu kwa nia ya kumchokoza yeyote ama nchi
yoyote. Tunajenga Jeshi letu kwa nia ya kulinda mipaka yetu. Na kweli
huwezi kujua, katika dunia yetu hii wakorofi na wachokozi wapo. Kwa sasa
hawapo lakini huwezi kusema kuwa hawatakuwepo milele. Inawezakana mtu
akaamua kutuchokoza na hivyo lazima tuwe tayari kulinda mipaka yetu.
Iddi Amin alikurupuka hivyo hivyo.”
Rais kikwete aliongeza: “Na
wala tusije kujidanganya. Kutumia fedha nyingi kujenga Jeshi letu siyo
ubadhirifu wa fedha. Ni jambo la lazima kabisa. Ni matarajio yangu kuwa
sera za namna hiyo zitaendelea, hata chini ya uongozi ujao, hata kama
baadhi ya watu wanaweza hata wakaanza kufikiria sera ya kupunguza
matumizi ya kijeshi….yatakuwa ni makosa makubwa.”
Rais Kikwete
pia ameishukuru nchi ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kuisaidia Tanzania
katika masuala ya ulinzi, akisisitiza kuwa katika ujenzi wa Jeshi la
Tanzania hakuna nchi rafiki kama China duniani. “Ni wajibu wetu kuwajua
na kuwashukuru marafiki zetu wa kweli.”
China ndio inagharimia
miradi hiyo miwili ya maboresho ya Uwanja wa ndegevita wa Ngerengere
ambao ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia hata ndege kubwa za
abiria ikitokea hali ya dharura katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere wa Dar es Salaam.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
21 Oktoba, 2015
Post a Comment