NA BASHIR YAKUB -
Unaposhindwa
kesi sio mwisho wa kusaka haki. Hii ni kwasababu kushindwa
kesi kunatokana na sababu nyingi . Si kweli kuwa kwakuwa
umeshindwa kesi katika mahakama fulani basi maana yake ni kuwa
ulikuwa huna haki. Yawezekana kabisa haki ilikuwa yako
isipokuwa umeshindwa tu kutokana na sababu nyingine za
kiutaratibu na kimbinu (procedures & technicalities). Pia waweza
kuwa umeshindwa kutokana na uwezo mdogo wa kujieleza na
kushindwa kugusa nukta muhimu ambazo kimsingi ndizo zilizokuwa
zinabeba shauri lako.
Lakini
pia waweza kuwa umeshindwa kwasababu ya hila na mbinu chafu.
Na hii wakati mwingine huwahusisha hata waamuzi yaani mahakimu
na majaji. Basi ifahamike kuwa ni sababu hizi zilizopelekea
kuwepo utaratibu wa rufaa ili yule anayehisi kutotendewa haki
aende mbele ili kuona kama anaweza kupata haki yake huko.
1.RUFAA NININI.
Rufaa
ni hatua ya kisheria ya kupeleka malalamiko katika hatua ya
mahakama ya juu zaidi baada ya mmoja wa wahusika katika kesi
iliyoisha kutoridhishwa na hukumu/maamuzi. Ili ukate rufaa ni
lazime uwe ulikuwa mhusika katika kesi iliyoisha na uwe na
sababu za kwanini unadhani hukuridhishwa na maamuzi. Sababu
yoyote ya msingi inakubalika.
2. NI HAKI YAKO KUAMUA KUKATA RUFAA AU KUACHA.
Suala
la kukata rufaa halitegemei hisani ya mahakama. Sio upendeleo
ambao mtu anapewa ili kuendelea kusaka haki. Ni haki ya
msingi na ya kisheria ambayo hutumiwa na yule ambaye anahisi
kutotendewa sawa katika shauri la awali lililoisha. Pia ieleweke
kuwa rufaa tunazoongelea hapa ni zile rufaa katika mashauri ya
madai. Rufaa katika mashauri ya madai tunaongelea mashauri ya
ardhi, ndoa, mikataba, migogoro ya biashara na mauziano kwa
ujumla, migogoro ya madeni na yale yote ambayo sio jinai.
Kwahiyo katika malalamiko ya namna hiyo ni uamuzi wako ukate
rufaa kwenda mbele au uache hata kama umeshindwa. Hii ni haki
yako na katu haiondolewi na yoyote.
3. HATA ALIYESHINDA ANAWEZA KUKATA RUFAA.
Hapo
juu tumesema rufaa ni kwa mtu ambaye hakuridhishwa na maamuzi
ya mahakama. Sio kwa ajili ya aliyeshindwa bali ni kwa ajili
ya yule ambaye hakuridhishwa. Hii ina Maana kuwa unaweza
ukashinda lakini ukawa hukuridhishwa. Na kama umeshinda lakini
hukuridhishwa pia waweza kukata rufaa. Kwa mfano ulifungua kesi
ukiomba fidia ya milioni 50. Hukumu ikatoka kuwa umeshinda
lakini ikasema kuwa utalipwa milioni kumi tu. Kwa mazingira kama
haya ni kuwa umeshinda lakini waweza kukata rufaa kudai zaidi.
Utakata rufaa kwakuwa umeshinda lakini hukuridhishwa na ushindi.
Kinachotakiwa kueleweka hapa ni kuwa rufaa inaweza kukatwa
hata yule aliyeshinda kesi na si tu kwa aliyeshindwa.
4. NAMNA YA KUKATA RUFAA.
Mara
tu kesi inapoisha hakikisha unafuatilia na kupata nakala ya
hukumu pamoja na tuzo( decree). Fuatilia kwa karani wa hakimu/jaji
aliyesikiliza shauri lako na umwambie nia yako ya kutaka
nakala ya hukumu na tuzo kwa ajili ya kukata rufaa. Huwezi
kukata rufaa bila nakala ya hukumu kwakuwa ni lazima uipitie
kwa umakini na kuona ni wapi palikuwa na tatizo ili iwe ndio
sababu yako ya rufaa.
Ikiwa
hukumu ilitolewa na mahakama ya mwanzo basi rufaa itaenda
mahakama ya wilaya, na ikiwa ilitolewa na mahakama ya wilaya
rufaa itaenda mahakama kuu na ikiwa ilitolewa mahakama kuu
basi rufaa huenda mahakama ya rufaa ambayo ni mahakama ya
mwisho kiitifaki. Pia rufaa zinazotoka katika mahakama za hakimu
mkazi kama ile ya kisutu ambazo baadhi huziita mahakama za
mkoa, rufaa zake huenda mahakama kuu pia.
Unapokuwa
unaandaa sababu za rufaa hakikisha unamuona mwanasheria kwa
ajili ya kupitia hukumu na kukusaidia kuandaa sababu za rufaa.
Hii ni kwasababu ipo namna ya kisheria ya kuandaa sababu hizi
kwani haziandaliwi kama barua.
Muda
ni suala la msingi sana katika kukata rufaa. Hakikisha pale
tu hukumu inatolewa unaandika barua mahakamani ya kuomba nakala
ya hukumu. Hii itasaidia hata zile siku 30 au 45 za rufaa
zikipita kabla hujapatiwa nakala ya hukumu kujitetea kuwa
ulichelewa kwakuwa ulikuwa ukisubiria nakala ya hukumu ambayo
uliiomba ndani ya wakati stahiki.
MWANDISHI
WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA
KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE ,
GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO.
0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
Post a Comment