Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha pamoja na viongozi wengine wa Chadema Wilaya ya Mpanda, wamekamatwa na polisi leo , kwa kile kinachodaiwa kufanya kampeni katika kambi ya wakimbizi ya Katumba, wilayani Mpanda bila kuwa na kibali maalum.
Masha
ambaye alikihama chama cha CCM hivi karibuni na kujiunga na Chadema
amezungumza nasi na kusema ameshikiliwa katika kituo cha polisi cha
Mpanda baada ya kufanya kampeni katika kambi hiyo.
“Nilikwenda kufanya kampeni katika kambi hiyo ambayo ina wakimbizi ambao mimi mwenyewe niliwapa uraia mwaka 2009,” amesema Masha na kuongeza:
“Kampeni
zinafanyika kule lakini kwa sababu wanazojua wao wametukamata wakati
hao wanaoitwa wakimbizi niliwapa uraia kwa amri ya Rais.”
Pamoja
na Masha wengine waliokamatwa ni Mgombea ubunge jimbo la Nsimbo, Gerald
Kitabu, Abraham Mapunda, Mwenyekiti wa Chadema, Mpanda. Katibu wa
Chadema jimbo la Nsimbo, Stanslaus Selemani, Dalas Damian, Lameck
Constantine Momose na Francisco Sylvester .
Kwa mujibu wa Masha, polisi wamewachukua maelezo viongozi hao wa Chadema kuanzia saa 9 mchana na wamemaliza saa 10 jioni.
“Tulikamatwa
kuanzia saa 7:15 mchana tukachukuliwa chini ya ulinzi mkali wa polisi
toka Katumba hadi Mpanda mjini na kuanza kuhojiwa,” amesema.
Akizungumza
na mtandao huu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, SACP Dhahiri
Kidavashari amesema Masha amekamatwa leo saa 4 asubuhi akiwa na watu
wengine sita kwa makosa ya kufanya mkutano bila kibali katika makazi ya
wakimbizi.
Kamanda
Kidavashari amesema viongozi hao wa Chadema walitumia uwanja wa kambi
ya wakimbizi ya Kanoge na baadaye Katumba bila kuwa na kibali maalum
baada ya kuona kuwa hakuna ratiba ya mkutano mwingine katika eneo hilo.
“Kufanya
mkutano si tatizo, tatizo walifanya hivyo bila kibali, yale ni makazi
ya wakimbizi wengine wamepewa uraia lakini wengine hawajapewa,” amesema.
Post a Comment