THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Miaka 10 inatosha kwa yeyote kutumikia Urais – Rais Kikwete
· Awataka watumishi wa Ikulu kumsaidia Rais ajaye kwa ari na nguvu zaidi kuliko walivyomsaidia yeye.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa miaka 10 ya uongozi inatosha kabisa kwa mkuu wa nchi
kufanya mambo mengi na kuwa hahitaji muda zaidi kuweza kumaliza ajenda
yake.
Aidha,
Rais Kikwete amewataka watumishi wa Ikulu kumsaidia Rais ajaye hata kwa
ari na nguvu zaidi kuliko hata walimvyosaidia yeye katika miaka yake
yote 10 ya uongozi wake.
Rais
Kikwete aliyasema hayo usiku wa Ijumaa, Oktoba 16, 2015, wakati
alipozungumza na watumishi wa Ikulu katika hafla ya chakula cha jioni
ambako watumishi hao waliagana na Rais Kikwete ambaye wamemtumikia kwa
vipindi tofauti, wengine wakiwa wamekaa naye kwa miaka yote 10 ya
uongozi wake.
Akizungumza
na watumishi hao, Rais Kikwete amesema kuwa anaondoka madarakani kwa
furaha sana hata kama anaona huzuni kuagana na watumishi hao wa Ikulu
ambao amekaa nao kwa miaka mingi, baadhi miaka 10.
“Kwa
hakika, naondoka mwenye furaha sana. Ni kweli nasikitika kuwa
tunaachana lakini mambo yote mazuri yana mwisho wake. Nimeifanya kazi ya
urais kwa miaka 10, nyie mnajua aina ya kazi hii.
Miaka
10 ni mingi. Ni miaka inayotosha kabisa kwa mkuu wa nchi kukamilisha
ajenda yake. Sidhani kama mtu anahitaji zaidi ya miaka 10 kutekeleza
ajenda yake ya msingi,” amesema na kuongeza:
“Na
hata ukitaka kukaa zaidi huwezi kuyamaliza yote. Mzee Nyerere alikaa
miaka 23 hakumaliza yote na yaliyobakia alimwachia Mzee Mwinyi ambaye
naye alimwachia yaliyobakia Mzee Mkapa. Rais Mkapa naye alifanya mengi
lakini hakumaliza yote na akaniachia mimi. Na mimi nitamwachia
yaliyobakia Rais ajaye.”
Kuhusu
Rais ajaye ambaye atakuwa mkazi mpya ndani ya Ikulu, Rais Kikwete
amesema: “Napenda kuwaombeni msaidieni sana Rais wetu ajaye. Kwa hakika
nawaombeni tumsaidie kwa ari na nguvu zaidi kuliko hata mlivyonisaidia
mimi.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
19 Oktoba, 2015.
Post a Comment