GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Professa Benno Ndulu (Pichani), ameshinda tuzo ya ‘Gavana Bora wa Afrika kwa mwaka 2015.
Tuzo
hiyo inayojulikana kama ‘Central Bank Governor of the Year’ ilitolewa na
taasisi ya Africa Investor (Ai) jijini New York, Marekani hivi karibuni
katika mkutano wake wa nane uliohudhuriwa na zaidi watu 250 maarufu
katika biashara, serikali, maendeleo, sekta ya fedha na wakuu wa nchi
tano za Afrika.
Prof.
Ndulu aliibuka kidedea kwa kuwashinda magavana wa benki kuu 10 zingine
za Afrika za Afrika Kusini, Uganda, Botswana, Sierra Leone, Rwanda,
Nigeria, Namibia, Misri na gavana wa Benki Kuu ya nchi za Afrika ya Kati
inahudumia nchi sita za Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad,
Guinea ya Ikweta, Gabon na Jamhuri ya Congo.
Ai ni
taasisi inayoongoza ya uwekezaji na mawasiliano barani Afrika ambayo
inawaleta pamoja wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali duniani wenye
vitega uchumi vyao barani Afrika.
Vigezo
viliyotumika kumpata gavana bora wa mwaka wa Afrika ni umahiri katika
eneo la kazi na kuonesha jinsi umahiri huo ulivyonufaisha sekta ya
uwekezaji katika nchi husika na mchango wa magavana katika kuendeleza
mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na kikanda (sub-region).
Vingine
ni mchango wa magavana katika kukuza uchumi na maendeleo endelevu ya
nchi zao na nafasi zao katika kukuza mtazamo wa Afrika kama kituo bora
cha kupokea vitega uchumi.
Katika
taarifa yake ya ushindi, Ai ilimpongeza Gavana Ndulu kwa ushindi katika
kipengele hicho cha Gavana Bora wa mwaka barani Afrika.
“Mafanikio
yako bila shaka yataendelea kutoa hamasa na kivutio kwa viongozi wakuu
wa serikali na sekta ya biashara wanaofanya juhudi za kuikuza taswira ya
sekta ya uwekezaji barani Afrika,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya
Ai.
Hii ni
mara ya pili kwa Profesa Ndulu kushinda tuzo ya kimataifa tangu
alipoteuliwa kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania mwaka 2008. Mwaka
2009, jarida maarufu la Emerging Markets linalochapishwa jijini London,
Uingereza, lilimtangaza Profesa Ndulu kuwa ‘Gavana Bora wa Bara la
Afrika kwa mwaka huo. Jarida hilo hutambua mafanikio yanayofanywa na
watendaji wakuu wa benki kuu na mawaziri wa fedha na kuwapa tuzo wakati
wa mikutano ya Benki Kuu ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa
(IMF) inayofanyika kila mwaka.
Imetolewa na:
Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki
Oktoba 12, 2015
Post a Comment