Rais
Jakaya Kikwete (katikati) akiwasili katika uwanja wa Jamhuri, Dodoma
katika maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge na Kumbukumbu za kifo
cha Mwalimu Julius Nyerere
RAIS
Jakaya Kikwete ametangaza vita na wapigakura watakaobakia maeneo ya
vituo vya uchaguzi baada ya kupigakura zao, akisema watakuwa wanavunja
sheria za nchi. Anaandika Charles William … (endelea).
Akiwa ni
Amiri Jeshi Mkuuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, Rais Kikwete ameonya
kwamba watakaokaa vituoni ‘watashughulikiwa’ na serikali.
Ametoa
tamko hilo mchana leo alipokuwa akihutubia kilele cha mbio za mwenge wa
uhuru kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma. Hafla hiyo ilihudhuriwa
pia na Waziri wa Habari, Vijana na Michezo, Dk. Fenella Mukangara pamoja
na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa.
Rais
ambaye dhahiri ametoa majibu ya kilichojitokeza kuwa ni malumbano
yanayoendelea kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jeshi la Polisi
na Serikali kwa upande mmoja na kwa upande wa wili viongozi wa vyama vya
siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Wakati
Tume na serikali wamekuwa wakisisitiza kuwa wananchi hawatakiwi kukaa
maeneo ya karibu na vituo vya uchaguzi baada ya kupiga kura, viongozi wa
UKAWA – Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD – wanahimiza watu kubakia
vituoni masafa ya mita 100 nje ya vituo kwa ajili ya kujiandaa kulinda
kura za wagombea wao.
Oktoba
mosi mbele ya umati mkubwa wa wananchi kwenye viwanja vya Tanganyika
Packers, Kawe, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema, “mkishapiga
kura, wanawake nendeni nyumbani, wanaume mtakaa umbali wa mita 200
unaotakiwa kisheria na mtakaa hapo mkilinda kura zenu mpaka matokeo
yatakapopatikana.”
Viongozi
wa UKAWA wanasema kwamba hakuna haki kwa wananchi kuambiwa waende
kusubiri matokeo ya uchaguzi majumbani kwao wakati kuna dalili nyingi za
kutokuwepo uhakika kuwa Tume itamudu kuzilinda kura dhidi ya
kuchakachuliwa.
Tume ya
Uchaguzi imekuwa ikijitahidi kuonesha uwazi katika mifumo ya
ushughulikiaji kura ingawa imekataa katakata kuonesha mifumo ya
ujumlishaji wa kura wakati daftari lenyewe imelitoa jana kwa ajili ya
kuhakikiwa na vyama vinavyoshiriki uchaguzi.
Katika
hali hiyo ya malumbano, Rais Kikwete anajitokeza kusema kuwa serikali
haitamvumilia mtu yeyote anayekusudia kuvunja sheria kipindi cha
uchaguzi kwa kuwa hayuko tayari kuona demokrasia “inatekwa nyara.”
Rais
analalamika kwa kuhoji, “Mnakaa nje ya vituo vya kupigia kura kufanya
nini? Wewe upo nje ya kituo, utalindaje kura? Mtu wa kulinda kura ni
wakala wa chama chako, labda kama ni mzembe.”
“Mipango
ya kuvuruga amani inafahamika na itadhibitiwa watu wao wapige kura
mapema na wanawake waende nyumbani, wanaume wabaki kulinda kura,
wanadhani wengine hawawezi kuwahi… msiilazimishe serikali kufanya mambo
yasiyopendeza, wanaotaka kufanya fujo hawatavumiliwa waatadhibitiwa,”
amesema.
“Mkishapiga
kura nendeni nyumbani Tume ya Uchaguzi imeshafafanua vizuri suala hili…
tofauti na hapo ni vurugu, na sisi kama serikali hatutawavumilia
watakaokiuka sheria. Tutawadhibiti kwa nguvu ileile watakayoitumia,”
amesema katika hotuba iliyotangazwa moja kwa moja na vituo vya
televisheni.
Rais
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa amedai suala la kulinda
kura ni mkakati wa viongozi wa vyama vya siasa kuwazuia baadhi ya
wananchi kupigakura baada ya wanachama wa vyama vyao kupiga kura.
Huko
nyuma, viongozi wa UKAWA walishatangaza kuwa watayatangaza matokeo ya
kura za urais hata kabla ya Tume, kwa kuwa sheria inaruhusu kutangaza
kura zinazokamilika kuhesabiwa na kuidhinishwa na wagombea na mawalaka
wao almuradi sio matokeo ya majimbo yote.
CHANZO: MWANAHALISI ONLINE
Post a Comment