RAIS Jakaya Kikwete amemteua Awadh Massawe kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA). Rais alitangaza uamuzi huo Ijumaa iliyopita wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bandari mpya ya Bagamoyo inayotajwa kuwa kubwa katika Afrika.
Akihutubia katika hafla hiyo, Rais Kikwete alisema yeye alishamaliza
uteuzi huo na kumwambia Massawe afuatilie barua yake rasmi ya uteuzi.
Kabla ya uteuzi huo, Massawe alikuwa akikaimu nafasi hiyo tangu Februari
mwaka huu, huku akitajwa kufanikiwa hadi sasa kufanya mageuzi makubwa
katika kuleta ufanisi katika bandari hapa nchini.
Kabla ya kukaimu nafasi hiyo, alikuwa Meneja wa Bandari ya Dar es
Salaam. Baada ya kuwa Kaimu Mkurugenzi, alianzisha mikutano ya wadau
yenye lengo la kurudisha mahusiano yaliyokuwa yameyumba kati ya pande
hizo mbili.
Mikutano hiyo inayofanyika kila Alhamisi ya mwisho ya kila mwezi
inalenga kuhusisha wadau mbalimbali katika majadiliano ya jinsi ya
kuboresha ufanisi katika bandari ya Dar es Salaam.
Mwishoni mwa Juni mwaka huu, TPA ilifungua ofisi ndogo katika mji wa
Lusaka, Zambia. Mafanikio mengine ya hivi karibuni ni kuanza kwa mfumo
mpya wa malipo kwa njia ya mtandao katika Bandari ya Dar es Salaam.
Inatarajiwa kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi huo wa bandari ya
Bagamoyo unaotarajiwa kugharimu dola za Marekani bilioni 10, kutaongeza
uwezo wa bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara zinazohudumia tani
milioni 12 za mizigo kwa mwaka, makasha 6,000 na kuajiri watu 3,200 na
vibarua 1,500.
Post a Comment