Waziri Mkuu Mizengo Pinda, jana alitumia Ibada ya Shukrani iliyofanyika katika Parokia ya Hananasifu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, kumshukuru Mungu kwa kumwezesha kulitumikia Taifa kwa zaidi ya miaka 15 na kuwaomba Watanzania wamsamehe kwa matamshi aliyoyatoa akiwa kiongozi, huenda yaliwakwaza baadhi yao.
Pinda
ambaye amekuwa Waziri Mkuu kwa miaka minane na miezi tisa, Waziri kwa
miaka miwili na nusu na Naibu Waziri kwa miaka mitano, alisema anasikia
fahari kumaliza uongozi wake kwa furaha na amani.
Moja
ya kauli tata zilizowahi kutolewa na kiongozi huyo iliyozua sintofahamu
ni ile ya Juni 29, 2013 katika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma
alipoviagiza vyombo vya dola kuwashughulikia kwa kuwapiga wale
watakaokataa kutii amri wakati wakifanya vitendo vya uvunjifu wa amani.
Kauli
nyingine tata ni ile ya mwaka 2009 baada ya kuwaeleza wanaoua watu
wenye ulemavu wa ngozi (albino) pamoja na vikongwe hawana budi kuuawa
kwa kuwa wakisubiri mahakama kuwahukumu, watakuwa wanakosea.
“Katika
ibada hii ya shukrani, nimemuomba Mungu anisamehe kwa matamshi
niliyoyatoa nikiwa kiongozi yanaweza kuwa yaliwaudhi watu bila mimi
kujua.
“Uwaziri
Mkuu ni kazi ngumu yenye changamoto nyingi. Nitakuwa mtu wa ajabu
nisipomshukuru Mungu kwa uongozi wake katika kipindi chote hicho tangu
nikiwa naibu waziri hadi kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu,” alisema.
Pinda alisema katika utumishi wake kwa umma amejifunza mambo mengi lakini kikubwa zaidi ni kujua jinsi ya kuishi na watu.
Katika
hatua nyingine, Abate Thadei Mhagama wa Abasia ya Hanga, aliwataka
waumini nchini wazidishe maombi kwa kufunga na kuomba kwa siku sita
zilizobaki kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.
“Ninawaomba
waumini wote tuzidishe sala ili nchi iendelee kuwa na amani na upendo,
tumwombe Mungu pia atuwezeshe kupata viongozi aliowandaa kwa yeye kwa
maana ya rais, wabunge na madiwani,” alisema Mhagama.
Alisema uchaguzi wa mwaka huu ni wa aina yake kwani demokrasia imekuwa miongoni mwa Watanzania.
“Sote
ni mashahidi, tumeona kwenye mikutano kila mgombea akija sote tunajaa
huko. Hii ni kwa sababu hatujui yupi ni yupi, ndiyo maana nasisitiza
kuwa tumuombe Mungu atuletee yule ambaye amemuandaa yeye,” alisisitiza.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Baraza la Walei katika parokia hiyo, Arbogasti Warioba alisema:
“Sote
tunatambua kuwa kazi aliyoifanya Waziri Mkuu Pinda ilikuwa ngumu,
misafara ilikuwa ni mingi na wakati mwingine ilikuwa ya mwendo mkali,
lakini Mungu alimtetea na kumlinda hadi leo yuko salama.
"Tunakushukuru pia kwa ushirikiano ulioendelea kutuonyesha wakati ukiwa madarakani na tunakuombea uendelee kuwa na ucha Mungu katika maisha yako ya uraiani.”
"Tunakushukuru pia kwa ushirikiano ulioendelea kutuonyesha wakati ukiwa madarakani na tunakuombea uendelee kuwa na ucha Mungu katika maisha yako ya uraiani.”
Post a Comment