Rais Kikwete leo amezindua miundombinu ya kuchakata na kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara na Songo Songo hadi Dar es Salaam kupitia Somanga, katika hafla iliyofanyika katika eneo la Madimba mkoani Mtwara.
Katika
hotuba yake Rais Kikwete amesema uzinduzi huo ni hatua muhimu kuelekea
katika taifa lenye uchumi wa kati kwa kuimarisha huduma za nishati ya
umeme pamoja na uchumi katika Nyanja mbalimbali ikiwemo viwanda kwa kuwa
gesi hiyo itamaliza kabisa tatizo la umeme.
Katika
uzalishaji wa umeme, Rais Kikwete amewaagiza watendani wa shirika la
umeme nchini TANESCO na lile la mafuta TPDC kuwa makini katika mchakato
wa manunuzi kwa kufuata sheria ili matatizo yaliyowahi kulikumba taifa
hili kutokana na ukiukwaji wa taratibu mwaka 2006 yaliyosababishwa na
uhaba wa umeme, yasijirudie tena.
Rais
Kikwete licha ya kuishukuru serikali ya China kuwa tayari kujenga
miundombinu hiyo, ameziagiza mamlaka husika kuhakikiksha kwamba zinatoa
huduma muhimu za jamii ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na
salama, pamoja na barabara kwa wakazi wa Mtwara ili wanufaike na gesi
hiyo.
Awali
akitoa maelezo ya utangulizi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la
Maendeleo ya Petroli (TPDC) Tanzania Dkt. James Mataragio ameeleza kuwa
miundombinu hiyo imekamilika na tayari gesi imeshaanza kusukumwa kutoka
Mtwara hadi Dar es Salaam.
Dkt
Mataragio amesema kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo umegharimu dola za
kimarekani bilioni 1.53 sawa na trillion 2.926 za kitanzania ikiwa ni
pamoja na gharama ambazo hazikuwa ziko nje ya gharama halisi ya
miundombinu hiyo.
Amesema kuwa asilimia 95 ya gharama hizo zinatokana na mkopo kutoka Benki ya Exim ya China huku asilimia 5 ikitoka serikalini.
Akizungumzia
faida za miundombinu hiyo, Dkt Mataragio ametaja faida kadhaa za gesi
hiyo ikiwa ni pamoja na kutumika katika uzalishaji wa umeme jambo
litakaloifanya Tanzania kuwa na umeme wa uhakika.
Ametaja
faida nyingine kuwa ni pamoja na kuongeza pato la taifa kutokana na
uuzaji wa gesi hiyo nje ya nchi, kuokoa fedha za kigeni ambazo hutumika
kuagizia mafuta kutoka nje ya nchi, kukuza uchumi kupitia ukuzaji wa
sekta ya viwanda, kuongeza mapato ya halmashauri kupitia mirabaha pamoja
na kuchochea utafiti wa mafuta na gesi.
Amesema
miundombinu hiyo itakuwa na uwezo wa kusukuma futi za ujazo milioni 784
kwa siku ifikapo mwaka 2020, ambapo kwa sasa inasukuma futi za ujazo
milioni 80 pekee.
Akimkaribisha
Rais Kikwete, waziri wa Nishati na madini George Simbachawene, amesema
kuwa huo ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi, na kwamba
serikali ina mpango wa kujenga mitambo ya umeme mkoani Mtwara
itakayozalisha zaidi ya Mega Watt 600 kwa ajili ya mikoa ya kusini.
“Mheshimiwa
Rais tunakupongeza sana kwa jitihada zako, kuna watu wanabeza wanahoji
eti utatuachaje, mimi nawaambia kwamba ulipoingia ulitukututa na gesi ya
futi za ujazo trillion 8, lakini unatuacha na futi za ujazo trillion
52”, amesema Simbachawene na kuongeza kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo
utazalisha ajira zaidi ya 1363 katika eneo hilo la Mtwara.
Post a Comment