Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amesema hakubaliani na maamuzi ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo yote ya uchaguzi na kuahirisha uchaguzi huo.
Akizungumza
jana na wanahabari makao makuu ya chama hicho, Mtendeni, Maalim Seif
alisema wamepata taarifa kwamba uchaguzi huo umeahirishwa kutokana na
kuwa haukuwa haki jambo ambalo anasema kuna njama zinazofanywa na sio
kweli kama uchaguzi huo haukuwa wa haki.
“Tunatamka
wazi kwamba CUF hatuutambui uamuzi huo binafsi wa Mwenyekiti wa Tume na
tunaitaka Serikali na CCM kuiacha Tume iendelee na kazi yake ya uhakiki
wa matokeo ya uchaguzi na kisha kutangaza mshindi,” Alisema Maalim Seif.
Maalim
alisema mwenyekiti hana mamlaka ya kufuta matokeo bila ya
kuwashirikisha makamishna wake ambao ndani yake kuna makamishana kutoka
chama cha wananchi CUF.
“Ametangaza
mwenyewe binafsi bila ya kuwashirikisha makamishna wenzake wa Tume ya
Uchaguzi, kwamba eti ameufuta uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 25
Oktoba, 2015” alisema Maalim.
Aidha
Maalim Seif alieleza kushangazwa na mwenyekiti wa tume kutoonekana
pamoja na mkurugenzi wake katika kituo kikuu cha kutangazia matokeo
ambapo Jumatano ilikuwa ni siku ya mwisho kutangazwa mshindi.
“Mwenyekiti
huyo amefanya hivyo baada ya kutoonekana tokea asubuhi katika kituo cha
majumuisho ya matokeo ya uchaguzi wa Rais kilichopo Hoteli ya Bwawani.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Salim Kassim Ali, naye hakuonekana tokea asubuhi
na haijulikani yuko wapi,” aliongeza.
“CUF
imeshtushwa na hatua hii inayokwenda kinyume na Katiba na Sheria ya
Uchaguzi ya Zanzibar na inaichukulia kauli ya Mwenyekiti huyo ni yake
binafsi hasa baada ya kujiridhisha kwamba hakukuwa na kikao chochote cha
Tume kilichofikia maamuzi hayo. Mwenyekiti kwa nafasi yake hana mamlaka
ya kufuta uchaguzi huo,” anasema Maalim Seif.
Kutokana
na hatua hiyo, Maalim Seif anasema kuna njama ambazo zinafanywa kwa
makusudi katika kuhujumu mchakato mzima wa uchaguzi.
“Inaonekana kuna njama za makusudi kutaka kuvuruga demokrasia ya Zanzibar na kuingiza nchi katika machafuko,” alisema mwanasiasa huyo.
Hata
hivyo, Maalim Seif aliwaambia wandishi wa habari kwamba mwenyekiti huyo
hakutafakari kwamba kuufuta uchaguzi mkuu wa Zanzibar kunaathiri pia
uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu
wapigakura walikuwa ni wale wale waliomo kwenye Daftari la Wapiga Kura
la ZEC.
Katibu
Mkuu huyo anasema wanatambua kwamba hatua hiyo imekuja baada ya
majaribio yote ya kutaka kulazimisha ushindi usiokuwepo wa CCM
kushindikana ambapo uhakiki wa matokeo ya uchaguzi wa majimbo yote 36 ya
Unguja na majimbo 4 ya Pemba uliokuwa umekamilika kabla ya zoezi hilo
kusitishwa umethibitisha matokeo ambayo CUF ilikuwa imeyakusanya.
Katika
hatua nyingine, Maalim Seif ameziomba jumuiya za kimataifa na marafiki
wa Tanzania kuingilia kati suala hili hasa kwa sababu waangalizi wa
kimataifa wameshuhudia hatua zote hizi pamoja na uhakiki wa matokeo
ulivyokuwa unakwenda.
Alisema
CUF imeonekana wazi kwamba ni mshindi wa uchaguzi wa Rais pamoja na
majimbo yote 18 ya Pemba na majimbo mengine tisa ya Unguja.
Post a Comment