STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 24.10.2015
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein
amesisitiza kuwa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kesho utakuwa huru,
haki na wenye utulivu na kuwahakikishia washirika wa maendeleo likiwemo
Shirika la Misaada la Uingereza (DFID) kuwa Zanzibar itaendea kuwa na
amani kwani ndio msingi wa maendeleo.
Dk.
Shein aliyasema hayo katika mazungumzo kati yake na Kiongozi wa Shirika
la Misaada la Uingereza anayefanya kazi zake nchini Tanzania Mhe. Vel
Gnanendran, huko Ikulu mjini Zanzibar.
Katika
mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo wa Shirika la DFID
ambaye alifuatana na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. Dianna
Melrose kuwa Zanzibar itaendelea kuwa visiwa vya amani na utulivu katika
kipindi chote cha uchaguzi mkuu na hata baada ya uchaguzi.
Dk.Shein
alisema kuwa hatua za maendeleo zilizofikiwa na Zanzibar sambamba na
amani na utulivu uliopo ndivyo viliyoyapelekea mashirika mbali mbali ya
Kimataifa ulimwenguni kuendelea kuiunga mkono Zanzibar likiwemo Shirika
la DFID kwa kuthamini na kutambua juhudi zake hizo.
Dk.
Shein alimuhakikishia kiongozi huyo wa Shirika hilo kuwa Zanzibar
itaendelea kushirikiana na Shirika hilo kwa lengo la kuleta maendeleo
endelevu nchini.
Katika
mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema kuwa juhudi kubwa zimechukuliwa na
vyombo vya ulinzi kwa kuendelea kusimamia amani na utulivu pamoja na
vyama vya siasa wakati wote wa kampeni hivyo ni matarajio yake kuwa
hatua hiyo itaendelezwa hata kwa siku za usoni ikiwemo siku ya kupiga
kura hapo kesho.
Aidha,
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwahimiza wawekezaji kutoka nchini
Uingereza kuja kuekeza Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo
ikiwemo sekta ya kilimo pamoja na utafiti wake.
Sambamba
na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuweko mpango maalum wa nafasi
za masomo nchini Uingereza kwa vijana wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na
kupitia Shirika hilo la DFID.
Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano kati yake na Shirika hilo la DFID.
Nae Kiongozi
huyo wa Shirika la DFID Mhe. Vel Gnanendran alimueleza Dk. Shein kuwa
Shirika hilo limeazimia kuiunga mkono Zanzibar kwa kutambua juhudi zake
katika sekta za maendeleo.
Alisema
kuwa juhudi zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuimarisha sekta zake za maendeleo zinahitaji kupongezwa na kuungwa
mkono ili zizidi kuimarika.
Aidha,
kiongozi huyo alimpongeza Dk. Shein kwa kuendelea kusimamia amani,
utulivu na mshikamano hapa Zanzibar na kueleza kuwa hiyo ndio nguzo
pekee itakayoendelea kuikuza Zanzibar kiuchumi na kimaendeleo.
Balozi
wa Uingereza Mhe. Dianna Melrose kwa upande wake alimuhakikishia Dk.
Shein kuwa nchi yake inatambua na inathamini uhusiano na ushirikiano wa
muda mrefu kati ya Zanzibar na Tanzania nzima pamoja na Uingereza uliopo
ambao aliahidi kuuendeleza.
Balozi
Melrose alimueleza Dk. Shein kuwa wawekezaji wengi wa nchi hiyo
wanavutiwa kuja kuekeza Zanzibar kutokana na kuwepo kwa amani na utulivu
sambamba na vivutio kadhaa vya utalii.
Kwa
upande wa mashirikiano katika sekta ya elimu alisema kuwa juhudi za
makusudi zinaendelea kuchukuliwa na zitachukuliwa katika kuhakikisha
nafasi za masomo kwa Zanzibar nchini humo zinaongezeka.
Sambamba
na hayo, Balozi huyo alimpongeza Dk. Shein kwa kuisimamia vyema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa ambayo
imepata mafanikio makubwa na kuwa kigezo ndani na nje ya bara la
Afrika.
Pia,
Balozi huyo aliisifu na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa kutoa fursa sawa ya kufanya Kampeni
zilizokuwa huru na amani kwa vyama vyote hapa nchini.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
Post a Comment