Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu ukomo wa madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwisho wa uhai wa Baraza la Mawaziri kwa kadri Tanzania inavyoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaofanyika Jumapili, Oktoba 25, mwaka huu, 2015.
Taarifa iliyotolewa jana jioni, Jumatano, Oktoba 21, 2015, Ikulu, Dar
es Salaam na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Yohana Sefue
imesema kuwa Serikali imetoa ufafanuzi huo kuwasaidia wananchi kuelewa
maelekezo na matakwa ya Katiba na Sheria kuhusu ukomo wa madaraka ya
Rais na mwisho wa Baraza la Mawaziri kufuatia mijadala ya karibu katika
vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Taarifa hiyo imekariri Ibara ya 42(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo inasema kuwa ukiacha sababu nyingine,
mtu anayechaguliwa kuwa Rais atashika madaraka ya kiti cha Urais hadi
Rais Mteule atakapoapishwa.
Ibara hiyo ya 42(3) inasema: ”Mtu
anayechaguliwa kuwa Rais, atashika kiti cha Rais hadi – (a) siku ambako
mtu anayemfuatia katika kushika kiti hicho atakula kiapo cha Rais.”
Taarifa hiyo imesema: “Hivyo, kwa mujibu
wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais anaendelea kuwa Rais,
akiwa na madaraka na mamlaka yote na kamili yanayoambatana na nafasi
hiyo, hadi Rais Mteule anakapokula kiapo cha Urais. Hivyo, ni vyema
wananchi waelewe kuwa hakutatokea wakati wowote ambapo hakuna Rais na
Amiri Jeshi Mkuu mwenye mamlaka kamili na aliye tayari kuyatekeleza
mamlaka hayo. Lengo ni kuhakikisha kuwa haitokei wakati wowote nchi yetu
ikakosa Rais na Amiri Jeshi Mkuu.”
Imesisitiza taarifa hiyo: “Madaraka na
mamlaka ya Rais yapo, na hayapugui kwa namna yoyote ile, hata baada ya
Uchaguzi Mkuu, mpaka Rais Mteule atakapoapishwa.”
Kuhusu ukomo wa Baraza la Mawaziri, taarifa imefafanua kuwa kwa mujibu
wa Ibara ya 57(2) ya Katiba, Waziri na Naibu Waziri ataendelea
kushikilia mamlaka ya nafasi yake hadi, ukiacha sababu nyingine, Rais
mteule atakapoapishwa.
Ibara hiyo 57(2) inatamka: “Kiti cha
Waziri au NaibuWaziri kitakuwa wazi litokeapo lolote kati ya mambo
yafuatayo – (f) Ukiwadia wakati wa Rais Mteule kushika madaraka ya Rais,
basi mara tu kabla ya Rais Mteule hajashika madaraka hayo.”
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wanaendelea
kushikilia nafasi zao, wakiwa na madaraka na mamlaka kamili
yanayoambatana na nyadhifa zao hadi mara tu kabla ya Rais Mteule
hajashika madaraka.
Imemalizia taarifa hiyo: “ Naomba vyombo
vya habari, vyenye jukumu la kuelimisha jamii, kuwaelewesha Watanzania
kuhusu utaratibu huu wakubadilishana madaraka kati ya awamu moja ya
uongozi wa nchi na nyingine. Madaraka na mamlaka ya Rais yapo, na
hayapungui kwa namna yoyote ile, hata baada ya uchaguzi Mkuu mpaka Rais
Mteule atakapoapishwa.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
21 Oktoba, 2015
Post a Comment