Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chadema, Reginald Munisi (kulia) akifafanua jambo. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Prof. Abdallah Safari |
ZIKIWA zimebaki siku tatu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimefichua mikakati iliyopangwa kuvuruga uchaguzi huo.
Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa Chadema, Reginald Munisi amebainisha mipango ‘ovu’
inayoratibiwa ili kuvuruga uchaguzi mkuu huku mipango hii ikishirikisha
baadhi ya makampuni ya simu za mkononi, Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) na wakurugenzi wa uchaguzi katika majimbo mbalimbali.
Munisi
ametaja baadhi ya mipango hiyo kama ifuatavyo, huku akitahadharisha
watakaoshiriki mipango hiyo kuwa wataliingiza taifa katika machafuko
bila sababu ya msingi.
Mpango wa kukata mawasiliano ya simu na data;
upo mpango wa kuzuia mawasiliano ya simu za mkononi kwa kusitisha
huduma ya kupiga na kupokea simu, kuzuia ujumbe mfupi wa maneno (sms),
kuzuiwa kwa intaneti (data) na hivyo mawasiliano kuwa magumu, hasa
wakati wa matokeo kubandikwa vituoni.
Mpango
huu unatajwa kuwa na lengo la kukwamisha watu kuwasiliana na kupeana
matokeo yatakayokuwa yakibandikwa vituoni ili kujumlisha na kupata
matokeo ya jumla ya nafasi za udiwani, ubunge na urais. Utekelezaji wa
mpango huu utashirikisha baadhi ya makampuni ya simu ambayo hakutaka
kuyataja.
“Tunaziomba
kampuni za simu zenye mpango huo, kuacha mara moja kwani zitajiongeza
katika orodha ya watuhumiwa watakaoenda ‘The Hague’ mara baada ya
uchaguzi kumalizika,” alieleza Munisi bila kuyataja makampuni hayo kwa kuwa bado chama hicho kinakusanya vielelezo.
Mpango wa kukata umeme maeneo yenye nguvu kubwa ya upinzani;
maeneo ambayo vyama vya upinzani vina nguvu kubwa umeme utakatwa baada
ya giza kuingia ili kuhakikisha mchakato wa kuhesabu na kujumlisha
matokeo unaingia dosari na hata vurugu kutokea ili katika taharuki hiyo
wizi wa kura uweze kufanyika.
Baadhi ya wakurugenzi wa uchaguzi kutoruhusu mawakala wa akiba wa upinzani kuapishwa;
wakati uapishaji wa mawakala ukiendelea katika maeneo mbalimbali
nchini, baadhi ya maeneo vyama vya upinzani vinazuiwa kuapisha mawakala
wa akiba na wakurugenzi kutaka mawakala waape idadi sawa na idadi ya
vituo vya kupigia kura.
Mkakati
huu unalenga kuvifanya vyama vya upinzani vikose mawakala wa akiba
iwapo itatokea dharura miongoni mwa wale walioapishwa, dharura
zinazoweza kujitokeza ni kuumwa, kusafiri nje ya vituo, au kutekwa kabla
ya kufika katika vituo vyao.
Iwapo
mawakala hao watakosekana kwa dharura, baadhi ya vituo watabaki
mawakala wa CCM pekee kwani hakutakuwa na mawakala wa akiba wa kuziba
nafasi zao kwa kuwa ni lazima mawakala wawe wamekula viapo vya kisheria
ili kupata uhalali wa kufanya kazi hiyo.
Reginald
Munisi ameleza kuwa Chadema na Ukawa kiujumla wamejipanga vyema
kuzikabili mbinu hizo chafu huku akiwaonya wale watakaoshiriki mipango
hiyo kuachana nayo mara moja kwani tayari imefahamika na wanaweza
kukumbana na nguvu ya Umma.
Post a Comment