Hofu ilitanda jana katika kiwanda cha MM Steel cha jijini Dar es Salaam, baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa mashine ya kusajili wapigakura kwa mfumo wa elektroniki (BVR) inatumika kuandikisha wafanyakazi katika kiwanda hicho.
Kutokana
na hofu hiyo, baadhi ya maofisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), wakiongozwa na Mwanasheria wa chama hicho, John Mallya,
Polisi na Tume Taifa ya Uchaguzi (Nec), walifika kiwandani humo na
kufanya upekuzi ikiwamo kuondoka na baadhi ya vifaa vilivyokuwa
vinatumika.
Baada
ya kukubaliana pande zote, vifaa hivyo ambavyo ni vya kuchukua alama za
mikono, macho, scanner na kompyuta mpakato, vilichukuliwa na Polisi ili
baadaye vikakabidhiwe Nec.
Polisi,
Chadema na Tume, walielezwa na Meneja Mawasiliano wa kampuni hiyo,
Abubakari Mlawa, kuwa kampuni hiyo imeamua kuandikisha wafanyakazi wake
kutokana na kukithiri kwa vitendo vya wizi katika viwanda saba
walivyonavyo na kushindwa kuwatambua wafanyakazi.
“Tunaendesha
zoezi la kuweka ‘data base’ kwa ajili ya wafanyakazi wetu wote kwa
maana ya kupiga picha na kuandika taarifa zake zote; amezaliwa wapi,
amesoma wapi na ameanza kazi lini, wakati tunaendelea na zoezi letu
walikuja watu wakajitambulisha kuwa ni polisi wakawaweka chini ya ulinzi
watu wanaofanya zoezi hilo. Tulipowauliza ni kina nani, walisema
wanatoka Chadema na wamepewa taarifa kuwa tunatoa vitambulisho vya
kupigiakura,” alisema na kuongeza:
"Ili
tujiridhishe, tuliamua kuwaita Nec na polisi kuthibitisha wamechukua
mashine kwenda kujiridhisha. Tunafanya zoezi hili wiki nzima na
tumeandikisha wafanyakazi zaidi ya 100 na tuna zaidi ya wafanyakazi
900.”
Hata
hivyo, wakati anahojiwa na Polisi na Chadema kama kifaa cha alama za
vidole wametoa wapi, Meneja huyo alisema walitoa zabuni kwa kampuni
ambayo hakuitaja na alipotakiwa kuitaja hakufanya hivyo.
Afisa
wa ICT wa Nec, Amosi Madaha, akizungumza mara baada ya kufika na
kulinganisha mashine ya alama za vidole ya Nec na yao, alisema ni mapema
sana kueleza kama vifaa hivyo ni sehemu ya vifaa vya BVR hadi
watakapokwenda kuvichunguza zaidi.
Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango wa Nec, Salvisius Mkwera,
alisema walipata taarifa kuna uandikishaji wa wapigakura unafanyika
ndani ya kiwanda hicho na walipofika walikuta baadhi ya vifaa ambavyo ni
ngumu kusema.
“Tulichokiona
ni baadhi ya vifaa ambavyo vinafanana na vifaa vya Tume, lakini
hatuwezi kuhakikisha kama ni vyetu au siyo, tulichokubaliana na polisi
ni kuchukua vifaa hivyo vifanyiwe uchunguzi zaidi tujiridhishe na vifaa
tulivyonavyo,” alisema.
Alitaja
kifaa kinachofanana na cha Nec kuwa ni `finger print machine,' lakini
wamechukua na vifaa vingine kama kompyuta mpakato na scanner.
Alisema pia wataingia kwenye data base ya kampuni hiyo ili kujiridhisha na taarifa zilizoingizwa.
Alisema
pia wamechukua orodha ya wafanyakazi waliorodheshwa kwenye karatasi ili
kuangalia kwenye daftari la kudumu la wapigakura kama kuna uwiano
wowote.
“Tutatoa
taarifa mapema na kwa wakati ili kuondoa wingu lililotanda kwa sasa,
tunataka pande zote zijiridhishe hivyo tutafanya kwa uwazi kueleza kama
hizi ni mashine zetu,” alisema.
Baadhi
ya wafanyakazi ambao hawakutaka kutajwa majina yao, walisema
wameshtushwa na uandikishaji huyo kwa kuwa unafanana na BVR hasa kwenye
uchukuaji wa alama na kuamua kutoa taarifa.
NIPASHE
Post a Comment