MAMLAKA
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imevionya vyombo vya habari
vitakavyotangaza matokeo ya uchaguzi mkuu kinyume cha sheria na taratibu
kwamba haitasita kuviadhibu.
Mbele
ya wanahabari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya
maudhui ya vyombo vya habari, Injinia Magreth Munyagi alionya kuwa
utangazaji wa matokeo ya uchaguzi kabla ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) ambao umekuwa ukizungumzwa na baadhi ya wanasiasa lazima uzingatie
taratibu zilizowekwa na tume tofauti na hapo hatua kali zitachukuliwa
na TCRA.
Kumekuwa
na mvutano baina ya Tume na vyama vya upinzani hususani vile
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kuhusu utangazaji wa
matokeo ya uchaguzi mkuu mwaka huu huku Tume ikisisitiza kuwa ndiyo
yenye mamlaka ya kutangaza matokeo na vyama hivyo vikisema hakuna sheria
inayovizuia kutangaza matokeo ya vyama vyao.
Wiki tatu zilizopita, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bara), John Mnyika alisema “hakuna
sheria inayotuzuia kutangaza matokeo ya kura zetu na ndio maana
tunasisitiza tutayatangaza matokeo yetu wenyewe iwapo tutamaliza
kujumlisha kabla ya masaa 72 ambayo NEC inasema itakuwa imemaliza.”
Akijibu
swali la mwandishi iwapo vyombo vya habari kutangaza matokeo
yatakayokuwa yametolewa na chama au vyama vya siasa ni kosa kisheria,
Injinia Munyagi alisema “Tumeshaeleza kwamba utangazaji matokeo lazima uzingatie sheria na taratibu za NEC.”
Baadhi
ya adhabu zilizotajwa kutumika kwa atakayethibitika amevunja sheria ni
kuonywa, kupigwa faini, kufungiwa kwa muda na kunyang’anywa leseni ya
utangazaji.
Pia
Mamlaka kupitia kamati hiyo ya maudhui ya vyombo vya habari, ilieleza
kuridhishwa kwa ‘wastani’ na utolewaji wa matangazo ya habari za
kampeni.
“Mpaka
sasa tumeridhishwa kwa wastani na kazi iliyofanywa na vyombo vya habari
katika kampeni za uchaguzi mkuu, taarifa za uchochezi na kutia hofu
zimepungua na waandishi wanajitahidi kutafuta vyanzo sahihi vya habari
zao,” alieleza mwenyekiti injinia Munyagi.
Kamati
ya Maudhui huteuliwa kisheria na waziri mwenye dhamana ya masuala ya
habari jukumu kubwa la kamati hiyo likiwa ni kufanya tathimini za mara
kwa mara kuhusu maudhui ya utangazaji na kupokea maoni au malalamiko juu
ya maudhui ya vipindi hivyo.
Post a Comment