Aliyekuwa
Mbunge wa Jimbo la Bunda kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri wa
Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, amesema hakubaliani na
matokeo yaliyotangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, Lucy
Msoffe, kwa kumpa ushindi wa ubunge Esther Bulaya, wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Mwanza, Wasira alisema matokeo ya ubunge
yalichakachuliwa kutokana na uhesabuji kura kutofuata utaratibu.
Wasira
alisema kutokana na hilo, msimamo wake ni kutoyatambua matokeo hayo
yaliyomshangaza na kumwangusha katika mbio hizo za kulitetea jimbo
hilo.
Alisema kura katika uchaguzi huo ziliibwa na kilichotangazwa hakitokani na uamuzi wa wapigakura wa jimbo hilo.
Wasira alitolea mfano wa kituo kimoja cha kupigia kura, akisema kura 1,000 ziliongezwa kwa lengo la kumsaidia mpinzani wake.
Alifafanua
kuwa kituo hicho cha kupigia kura kilionyesha kilikuwa na wapigakura
waliojiandikisha 367, waliopiga kura 276, kura halali zilikuwa 271.
Lakini
alisema matokeo katika kituo hicho yalionyesha kuwa chama cha ACT-
Wazalendo kilipata kura moja, CCM kura 120 na Chadema kura 749, na
Msimamizi wa Uchaguzi akatangaza waliojiandikisha walikuwa 1,367.
Alisema
hatasaini matokeo hayo kwa sababu ni batili na hawezi kuafikiana nayo
wala kuyatambua huku akisisitiza uchaguzi huo haukufanyika kwa haki.
Hata hivyo, Wasira alisema Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, Msoffe
hakutilia maanani barua ya malalamiko aliyoandika kupitia kwa
Mwanasheria wake ili kusitishwa utangazaji wa matokeo hayo. Hata hivyo,
alikanusha tuhuma za kukimbilia jijini Mwanza kwa kile kilichodaiwa ni
kukwepa aibu ya kushindwa, bali alikwenda huko kwa lengo la kupata
ushauri wa nini cha kufanya katika kipindi hiki.
Post a Comment