Mabibi na Mabwana,
Kama
mnavyojua tarehe 25 ya mwezi huu wa Oktoba mwaka 2015 siku ya Jumapili
katika nchi yetu kutafanyika Uchaguzi Mkuu kwa ajili ya kuchagua rais,
wabunge na madiwani zoezi ambalo litawashirikisha watanzania wote
waliojiandikisha kupiga kura kwa mujibu wa sheria.
Zoezi
hili kwa mujibu wa sheria za uchaguzi litasimamiwa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi yaani NEC kama ambavyo imekuwa ikifanyika katika chaguzi
mbalimbali zilizopita ama kuwahi kufanyika katika nchi yetu.
Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi inalo jukumu kubwa la kuhakikisha ulinzi na
usalama wa raia na mali zao unaimarishwa kabla, wakati na baada ya zoezi
hilo la Uchaguzi Mkuu katika maeneo yote ya nchi yetu, ili wananchi
waweze kuwa salama na kuendelea na maisha yao ya kila siku.
Ndugu Waandishi wa habari,
Kumekuwepo
na taarifa mbalimbali za vitisho zinazosambazwa kwenye mitandao ya
kijamii na hata mitaani na watu wasio na nia njema kwa taifa letu,
zikiwataka wananchi wanunue mahitaji yao mbalimbali ikiwemo vyakula na
kuvihifadhi kwa ajili ya kuja kuvitumia wakati na baada ya uchaguzi kwa
ubashiri wa kuwepo kwa vurugu wakati ama baada ya uchaguzi.
Taarifa
hizi zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na mitaani kwa ujumla ni
taarifa potofu ambazo zinalenga kuwajengea wananchi hofu na mashaka,
wasiwasi na vitisho pasipo sababu zozote zenye tija kwa taifa letu.
Ndugu zangu Waandishi wa habari,
Nitoe
rai kwa Raia wote waishio hapa nchini yaani Watanzania na Wageni
kupuuza taarifa zote zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na
mitaani kwa kuwa taarifa hizo si za kweli, na wala hazilengi kulinda
amani iliyopo nchini kwetu.
Pamoja
na hayo kumekuwa na matamko kwa baadhi ya wanasiasa katika kampeni zao
kudai kuwa Serikali itasitisha posho za askari mara baada ya Uchaguzi
Mkuu, Taarifa hizi si za kweli kwani Posho za Vyombo vyote vya dola
vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni za kudumu kama
ilivyoelekezwa katika waraka wetu, hazitafutwa wala kubadilika na iwapo
zitabadilika ni kwa kupandishwa na wala si kufutwa.
Nawaomba
wananchi wote watii sheria za nchi na zile za Tume ya Uchaguzi
zinazoongoza Uchaguzi Mkuu sambamba na kufuata Maelekezo yatakayotolewa
na Tume hiyo kabla, wakati na baada ya kupiga kura jambo litakalosaidia
kuilinda amani ya nchi yetu, kwani kila Mtanzania anao wajibu wa
kuilinda amani kwa kufuata sheria za nchi bila kushurutishwa.
Wananchi
wanapaswa kutambua kuwa baada ya uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25
mwaka huu maisha ya watanzania yanapaswa kuendelea kama kawaida hivyo
itikadi zao za vyama vya siasa zisiwatofautishe na kuwajengea chuki,
uhasama ama uadui kwani watanzania ni wamoja na wamekuwa wakiishi kwa
amani, umoja na ushirikiano katika kuendeleza taifa hili.
Ndugu waandishi wa Habari,
Wananchi
hawapaswi kuwa na hofu yoyote kwa kuwa Serikali ya awamu ya nne ambayo
imeongoza na kuwatumikia wananchi kwa kipindi cha miaka kumi inakusudia
kwa dhati kukabidhi madaraka kwa serikali iyajo ya awamu ya tano katika
hali ya amani na utulivu.
Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama
inawahakikishia wananchi kuwa itahakikisha hali ya amani na utulivu
inakuwepo na kuimarishwa kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu mpaka
pale ambapo Uongozi wa serikali ya awamu ya tano utakapoingia
madarakani.
Wananchi watoe taarifa Polisi pale watakapoona kuna dalili za uvunjifu wa amani kwa kupiga simu ya bure namba 112.
Nawashukuru kwa kunisikiliza, Asanteni .
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Post a Comment