Aliyekuwa
mbunge wa Jimbo la Mikindani, mkoani hapa, Hasnein Murji, amesitisha
huduma ya usafiri kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Naliendele
kufuatia kushindwa ubunge katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25.
Alikuwa akitoa usafiri kwa wanafunzi wa shule hiyo tangu mwaka 2011 alipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti shuleni hapo, wanafunzi hao walisema kuwa kitendo
cha kutochaguliwa mbunge huyo kimewaathiri kiusafiri.
‘Tangu
alipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hili, alitoa magari mawili ambayo
yalikuwa yanapokezana, tulikuwa hatulipi nauli, tulikuwa tunawahi
vipindi kwa sababu tulikuwa na uhakika wa usafiri,’ alisema mmoja wa
wanafunzi hao.
Walisema usafiri wa daladala ni mchache, lakini pia wanatozwa nauli ya Sh. 500 badala ya Sh. 200.
Walidai kuwa wakati mwingine wazazi wanashindwa kumudu gharama na kushindwa kufika shuleni kwa sababu ya kukosa nauli.
Walisema
hivi sasa wanafunzi wanaofanya mitihani ya kumaliza kidato cha nne
wanalazimika kupanda mabasi ya Tandahimba na Newala ili kuwahi kufanya
mitihani.
Kharim
Mohamed, ni mwanafunzi wa kidato cha tatu, alisema kuwa ukosefu wa
usafiri wa uhakika unawafanya wachelewe vipindi na hukaa kituoni kwa saa
tatu wakingoja usafiri.
Awali
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Hittu Rashid, alisema shule hiyo ilianza
mwaka 1997, na tatizo la usafiri kwa shule hiyo limekuwa la muda mrefu.
‘Miaka ya nyuma kabla sijahamia hapa, niliambiwa kwamba wanafunzi
walikuwa wakitumia malori ya mchanga kama usafiri wa kuja shuleni, na
mwanafunzi mmoja alipata ulemavu baada ya kuvunjika mguu wakati
akipanda gari,’ alisema.
Alisema, tangu kuwepo kwa usafiri wa uhakika wanafunzi wake wamekuwa na mahudhurio mazuri darasani na utoro ukipungua.
‘Kutoka
mjini kuja hapa shuleni ni kilomita 12, na kutokana na tatizo la
usafiri kwa wanafunzi wangu aliyekuwa mbunge aliona tatizo hili akaamua
kuwasaidia, zaidi ya wanafunzi 50 walikuwa wakipanda magari yake bure,’
alisema.
Alipoulizwa
na Nipashe kuhusu kusitisha usafiri huo, Murji, alikiri kuchukua hatua
hiyo tangu Jumatatu iliyopita kwa madai kuwa alikuwa akitoa huduma hiyo
kama mbunge wao, lakini sasa sio mbunge tena ni mfanyabishara kama
walivyo wengine.
Aliwataka wamuombe mbunge wao wa sasa awasaidie.
Hata
hivyo, alisema atatoa magari kwa ajili ya kwenda Mikindani kwa wananchi
wote na nauli yake itakuwa Sh. 200 bila kujali umri wa mtu.
Akizungumzia
mpango wa kuwasaidia wanafunzi hao hata kwa kuwatoza nauli ili
kupunguza makali ya usafiri, Murji alisema: ‘Kwa kuwa mimi sio mbunge
wao tena nafikiria kama nitaweza huenda nitawapelekea, lakini sijajua
itachukua muda gani kurejesha usafiri shuleni hapo,’ alisema.
Chanzo:Nipashe
Post a Comment