Mkoa
wa Arusha umetajwa kati ya mikoa ya pembezoni nchini ambayo inaongoza
kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wanaomiliki silaha za moto, hasa
bastola.
Katika maeneo ya burudani katika jiji
la Arusha kumekuwapo na matukio ya watu kutishiana kwa bastola jambo
ambalo limesababisha ulinzi kuimarishwa katika maeneo haya na baadhi ya
wateja kuzuiwa kuingia ndani na silaha hizo.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na
Mwananchi umebaini kuwa idadi kubwa ya vijana katika jiji la Arusha
wanamiliki bastola, baadhi kihalali na wengine kinyume cha sheria.
Hata hivyo, kati ya wanaomiliki
kihalali, kuna kundi ambalo linamiliki bastola hizo kihalali kupitia
mawakala ambao hulipwa kati ya Sh1.5 milioni hadi Sh2 milioni.
Uchunguzi umebaini kuwa watu wengi wanaomiliki silaha hizo kinyume cha sheria ndiyo wanazitumia katika matukio ya uhalifu.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoa wa
Arusha, Liberatus Sabas licha ya kukiri vijana wengi kumiliki bastola
katika jiji hilo, alisema wengi wanaozimiliki wamezipata kwa kufuata
sheria.
Hata hivyo, katika kudhibiti silaha
hizo, alisema jeshi hilo kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama
limesitisha kutoa vibali vya umiliki wa bastola.
“Tumesitisha
kutoa vibali vya bastola lakini tunatoa vibali vya silaha nyingine kwa
mahitaji maalumu, lakini silaha zilizopo mikononi mwa watu ni zile
ambazo zilitolewa kipindi kirefu cha nyuma,” alisema.
Alisema baadhi ya waliopata bastola
kipindi cha nyuma ni wafanyabiashara na wachimbaji wa madini katika
maeneo ya Mererani kulingana na biashara zao.
Hata hivyo, alisema silaha hizo
zilitolewa kihalali lakini baadhi ya wamiliki wamekuwa si waangalifu
katika utunzaji na hivyo kufanya baadhi kuwafikia watu wasio waaminifu.
“Katika
matukio ya ujambazi ambayo yanatokea hapa Arusha, silaha ambazo
tunakamata ni zile ambazo zilizotolewa kihalali lakini wamiliki wake
waliibiwa au kupoteza,” alisema.
Alisema uhakiki wa silaha ambao
umekuwa ukifanywa na jeshi hilo na kwa kiasi kikubwa umesaidia kuziondoa
bastola mikononi mwa watu wasio waaminifu.
Kuuzwa kwa silaha
Mwananchi imebaini kuwa, baadhi ya wamiliki wa silaha hasa bastola wamekuwa wakiuza mitaani kutokana na hali ngumu ya maisha.
Joram Kaaya mkazi wa Ngulelo
alilieleza gazeti hili kuwa kipindi cha nyuma vijana wengi wa Mirerani
walinunua silaha kihalali kutokana na biashara zao lakini sasa kutokana
na kuporomoka biashara ya madini ya Tanzanite wamekuwa wakiuza.
“Bastola
zinauzwa kati ya Sh1,000,000 hadi 2.5 milioni kutoka kwa wamiliki
lakini wanakueleza kufuata taratibu za umiliki, kwa kuandika barua ya
umiliki wa silaha ngazi ya mtaa na kwenda polisi kabla ya kukabidhiwa
silaha na kitabu chake,” alisema.
Mkazi mmoja wa Arusha, aliyeomba
kuhifadhiwa jina, lake alikiri kuwapo kwa madalali wa silaha ambao
wamekuwa wakifuata taratibu za umiliki wa silaha.
“Mimi
mwenyewe nimenunua bastola yangu kwa mtu lakini kabla ya kumiliki
nilifuata taratibu zote za kipolisi na kiserikali na nimekuwa nikiilipia
kila mwaka,” alisema.
Hata hivyo, Kamanda Sabas alikemea utaratibu wa kununua silaha mitaani akisema ni kuvunja sheria.
“Ni
makosa kisheria, kuuza na kununua silaha mitaani ambao watakamatwa
watafikishwa katika vyombo vya sheria, kuna taratibu za umiliki kwa
ambao wanahitaji silaha ni vyema kuzifuata,” alisema.
Silaha kutoka nje
Wakati polisi wakieleza kuwapo
udhibiti mkubwa katika uingiaji wa silaha katika njia haramu, taarifa
zilizolifikia Mwananchi zinaeleza kuwa wapo watu wanaziingiza kutoka nje
ya nchi kupitia njia za panya.
Silaha hizo, zinaelezwa kuingizwa kwa kubadilishana na bidhaa mbalimbali kama vyakula, mifugo na fedha.
Katika Wilaya ya Ngorongoro pekee,
ambayo ipo mpakani na nchi jirani na Kenya, mara kadhaa polisi, wamekuwa
wakikamata silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria ambazo zinamilikiwa
na makundi ya wafugaji na wakulima ambao wamekuwa wakipigana mara kwa
mara kugombea ardhi.
Mwaka juzi silaha zaidi ya 80
zilikamatwa katika operesheni ya polisi katika wilaya ya Ngorongoro
pekee na kumekuwapo na taarifa za wakazi wengi wa wilaya hiyo kumiliki
silaha kinyemela.
Wilaya nyingine zenye wamiliki wengi
wa silaha ama halali au haramu ni Arumeru na Longido huku wilaya za
Monduli na Karatu zikiwa hazijaathiriwa sana na kuzagaa kwa silaha.
Post a Comment