Bibi harusi Doroth Msuya( Kulia ) |
Polisi mkoani Kilimanjaro imesema binti huyo hakutekwa nyara kama ambavyo wanafamilia walitoa taarifa Kituo cha Polisi Himo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alisema jana kuwa
uchunguzi uliofanywa umethibitisha kuwa bibi harusi huyo hakuwa ametekwa
nyara.
“Polisi
walifungua jalada la uchunguzi na ilibainika kuwa taarifa za kutekwa
zilizokuwa zimetolewa hazikuwa na ukweli, bali aliondoka kwa kupanda
pikipiki,” alisema.
Kamanda
Ngonyani alisema uchunguzi huo ulibaini kuwa wakati akipambwa, aliomba
kwenda kujisaidia na baadaye kuomba apelekewe kanga na ‘tishu’ lakini
akatumia mwanya huo kuondoka,” alisema.
Alisema
uchunguzi huo umebaini kuwa baada ya kupanda pikipiki ilimpeleka hadi
kituo cha mabasi na alimlipa dereva wa bodaboda kisha alipanda gari la
abiria lililompeleka hadi mjini Moshi.
Tukio
hilo lilitokea Jumamosi iliyopita saa 6.30 mchana eneo la Lole huko
Mwika, Moshi wakati bibi harusi huyo alipotoroka saluni akimwacha mpambe
wake akiendelea kupambwa.
Ndoa
hiyo ilikuwa ifungwe saa tisa alasiri katika Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Lole Dayosisi ya Kaskazini na
baadaye sherehe ingefanyika katika Ukumbi wa Mamba Complex.
Habari
zilizopatikana jana kutoka kwa familia ya Machange, zilieleza kuwa
Doroth alipatikana juzi baada ya kuonekana akiweweseka, kisha akapelekwa
hospitali ya Seliani kwa matibabu.
Ndugu
wa karibu wa familia ya Machange ambaye aliomba jina lake lisitajwe,
alisema kulikuwa na kikao kilichokuwa kikiendelea kati ya familia ya
Machange na Msuya.
“Jana
(juzi) tulipigiwa simu na kuelezwa kuwa Doroth amepatikana Arusha
lakini yuko kama hajielewielewi na hajui nini kimetokea,” alisema.
Habari
zaidi kutoka ndani ya familia hiyo, zinadai kuwa bibi harusi huyo
alikuwa ametaka harusi hiyo iahirishwe na ombi hilo alilitoa zaidi ya
mara 10 bila kueleza sababu.
Post a Comment