BARAZA
la Taifa la Mitihani (NECTA) limesema ili kutekeleza sera ya elimu ya
mwaka 2014, watoto wataanza kukariri darasa kuanzia wakiwa darasa la
pili. Alisema hatua hiyo itachukuliwa endapo watashindwa mtihani wa
kujipima ambao utaanza rasmi mwakani kwa wanafunzi wa ngazi hiyo ya
elimu.
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, aliyasema hayo mwishoni
mwa wiki alipozungumza na gazeti hili. Alisema kufanyika kwa mitihani
hiyo kunakwenda sambamba na kuipa hadhi mitihani ya kupima wanafunzi
katikati ya masomo ya darasa la nne na kidato cha pili ambayo kwa sasa
itakuwa chini ya baraza hilo tofauti na ilivyokuwa awali.
Dk. Msonde alisema kwa upande wa mitihani ya darasa la pili, matokeo ya
mitihani hiyo itasaidia kuwatenga wanafunzi hao kwenye makundi matatu
ambayo walimu watatakiwa kuyafanyia kazi kuhakikisha watoto hao
wakiendelea na madarasa ya juu watafanya vizuri.
Alisema kwa kuwaandaa watoto kwa mitihani hiyo, anaamini mpaka wakiwa
wanamaliza darasa la saba hakuna ambaye atakuwa hajapata stadi za kusoma
na kuandika kama ilivyo kwa sasa ambako baadhi uhitimu elimu ya msingi
wakiwa hawajui kusoma na kuandika. Kwa kuanza kuwapima wakiwa darasa la
pili watakuwa wanaangalia kwenye stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu
huku mitihani mingine kama ile ya darasa la nne ikipandishwa hadhi na
kuwa chini ya baraza. Tunaamini suala la watoo kumaliza darasa la saba
baadhi wakiwa hawajui kusoma na kuandika litaisha, alisema.
Alisema mipango ya sera hiyo ikikamilika, mtihani wa darasa la saba
ambao hivi sasa ni wa kuhitimu elimu ya msingi, utakuwa wa kupima kama
ulivyo ule wa darasa la nne kwa sababu elimu ya msingi mwisho itakuwa
kidato cha nne. Siwezi kusema ni lini hili litaanza kwa sababu
utekelezaji wa sera ni mchakato, lazima kwanza madarasa ya sekondari
yaongezwe.
Mitaala ibadilike kama hivi sasa ambavyo ya darasa la kwanza na la pili
imebadilika na ndiyo kwanza tunaanza kuwapima wanafunzi kwa mtihani huo
wa darasa la pili.
Faida nyingine ya mtihani huo na ule wa darasa la nne ni kuhakikisha
mpaka mtoto anafika darasa la saba, wale watakaopata alama 100 chini ya
250 ambao kwa sasa ndiyo ufaulu wawe wameongezeka, alisema Dk. Msonde.
Alisema ili kuona namna bora ya kuanza kufanya mtihani huo mwakani, leo
watoto wa darasa la pili kutoka shule 66 zilizo kwenye mikoa 11
watafanya mtihani huo ikiwa ni sehemu ya majaribio.
Alisema kwenye mikoa hiyo zimechaguliwa wilaya ambazo zimetoa shule moja
ya kijijini, moja ya mjini na nyingine ya mchepuo wa Kiingereza.
Post a Comment