Dar/Mikoani.
Siku moja baada ya Rais Mteule wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John
Magufuli kukabidhiwa cheti chake kuwa ndiye mshindi katika Uchaguzi Mkuu
wa 2015, wananchi wakiwamo wa kada mbalimbali wameelezea hisia zao na
matanio yao kuona atatekeleza ahadi alizotoa kwenye mikutano yake ya
kampeni.
Dk
Magufuli (CCM) alitangazwa mshindi wa urais na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25 kwa kupata kura
8,882,935 huku mpinzani wake, Edward Lowassa (Chadema) akiambulia
6,728,480. Wagombea wanane walikuwa wakiwania kiti hicho kupitia vyama
vingine vya siasa.
Mhadhiri
wa Chuo cha Saut Tawi la Mtwara, Michael Okoda alisema anafurahi kwa
kuwa uchaguzi huo ulifanyika kwa amani na utulivu na kwamba Dk Magufuli
anatakiwa kutekeleza ahadi alizotoa kwa wananchi wakati akijinadi kwao
kwenye mikutano ya kampeni.
Alizitaja baadhi ya ahadi hiyo kuwa ni elimu bure, afya na ajira kwa kuwa walioshiriki kumpigia.
Mwenyekiti
wa Umoja wa Jumuiya ya Vyuo Vikuu na Vyuo Vishiriki (Asas), Paul
Losolutie, alisema anataka kuona mahakama ya wezi na mafisadi inaundwa
nchini na Tanzania inakuwa nchi ya viwanda kama alivyoahidi Magufuli
kwenye kampeni.
Azaki
Mratibu
wa Taifa wa Taasisi ya Wanawake ya Ulingo, Dk Ave Maria Semakafu,
alisema anaamini wanawake wengi wamefurahishwa na ushindi huo kwa sababu
kwa umewezesha pia kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi kuwa na
Makamu wa Rais mwanamke, Samia Suluhu Hassan.
“
Tumefungua ukurasa mpya kwani miaka 20 ya tamko la Mkutano wa wanawake
Duniani wa mwaka 1995 Beijing, tumekuwa na mrejesho mzuri kuhusu
mwitikio wa Serikali kuweka ushiriki sawa wa nafasi za uongozi,” anasema
Dk Semakafu .
Beatrice
Jesta wa RRM, alisema wanachosubiri kwa sasa ni Dk Magufuli kuanza
kuwasafisha wezi wa fedha za umma na kuijenga nchi katika mazingira ya
umoja na mshikamano.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Amani mkoa wa Arusha (APET), Petro Ahham anasema uchaguzi
umemalizika kwa amani katika maeneo mengi jambo ambalo ni la kujivunia
kwa Watanzania.
“Nchi
nyingine leo kungekuwa hakuna amani, lakini uchaguzi umekwisha kwa
amani na sisi hapa Arusha amani imekuwa nzuri zaidi tunapongeza wadau
wote kwa kufanikisha amani, ’’ anasema.
Wachambuzi
Prince
Mwaihojo, mchambuzi wa masuala ya siasa mkoani Mbeya anasema ushindi wa
Dk Magufuli umeinusuru nchi kuporwa na waroho wa madaraka.
Alisema
Tanzania ya sasa inamhitaji kiongozi kama Magufuli ambaye alitangaza
kwamba atawatumikia Watanzania wote na kuwaunganisha kuwa na umoja bila
kujali itikadi za vyama vya siasa.
Makamu
Mwenyekiti wa Chama cha Chaumma, Kayumbu Kabutale anasema kama Dk
Magufuli hataweza kufanya mapinduzi katika mfumo wa CCM na kutekeleza
ahadi alizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni na kubaki kuwa ndoto.
Wananchi
Yusuph
Mwikoki, mkazi wa Songea, amemtaka Dk Magufuli atimize ahadi alizotoa
na asifanye kazi kwa mazoea kwa kuwa Watanzania wana matarajio makubwa
katika uongozi wake.
Akitoa
maoni yake, mkazi wa mtaa wa Mwambene wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya,
Edson Chuma alisema ushindi wa Dk Magufuli ni kauli ya Watanzania
wasiotaka kupelekeshwa kama ng’ombe.
Hamis
Abdallah Ally, mkazi wa Maposeni Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma
alisema anasubiri kuona Dk Magufuli akiwakamata na kudhibiti mafisadi na
kurejesha imani kwa wananchi.
Kelvin
Chale wa Manispaa ya Songea, alimtaka Dk Magufuli kuboresha mazuri ya
Rais Jakaya Kikwete na kushugulikia kero za wananchi.
Neema
Komu, mkazi wa Kibaha, Pwani alisema hana mpango wa kuandaa ada wala
michango ya shule kwa watoto wake kwani anaamini mgombea aliyepita
atafuta yote kama alivyoahid kwenye kampeni.
“Kwa sasa ninaandaa sare tu kwa mwanangu anayetarajia kuanza masomo mwakani kwani hatutakuwa na masuala ya ada,” alisema
Irine
Nkya alisema : “Tunamtarajia Dk Magufuli afanye kazi kwa bidii, juhudi
na maarifa huku akiwachukulia hatua kali watumishi wazembe kama
alivyowaahidi Watanzania.”
Paul
Shija, mkazi wa Urambo mkoani Tabora, alisema Rais Magufuli atekeleze
ahadi kwa wananchi kwa kutatua kero zao kwa sababu ameonyesha ana uwezo
wa kuwatumikia.
Mkazi
wa mkoani Geita, Shaaban Jumanne alisema ana matarajio makubwa na
Magufuli kwa kuwa wakazi wenzake uchumi wao mkubwa ni uchimbaji wa
madini na hivyo atimize ahadi yake.
Masanja
Maduhu alisema: “Dk Magufuli alivyopita kwao kuomba kura aliahidi
kuwapa maeneo ya uchimbaji wananchi, sasa tunamuomba atimize ahadi
yake.”
Mery
Ndoshi wa Geita, alisema mji wao unakabiliwa na kero sugu ya kukosa
maji safi na salama ambayo Magufuli wakati wa kampeni aliwaahidi
kuitatua na kujenga vyumba vya madarasa.
Falesi
Bunini, mkazi wa Kata ya Kwanga mkoani Mara, alisema angependa kuona Dk
Magufuli akitekeleza ahadi ya kuwalipa wazee fedha za kujikimu kwa
maisha na matibabu bure.
Joseph
Haule mkazi wa kata ya Rwamlimi alikumbusha ahadi ya kukuza uchumi na
kuhakikisha thamani ya shilingi inaongezeka ili kukabiliana na mfumo wa
bei na maisha ya Watanzania kuzidi kuwa magumu.
Mkazi wa Pansiasi mkoani Mwanza, Celine Paul alisema tatizo la ajira kwa vijana ni kati ya mambo aliyoahidi kutatua..
Peter Mwita, mkazi wa Igoma, Mwanza alisema anatarajia Magufuli ataondoa migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima.
Juma
Cosmas, mkazi wa kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga alisema
anatarajia kuona viwanda vikifufuliwa, kuanzisha vipya na kuondolewa kwa
tatizo la ajira.
Mkazi
wa kata ya Kambarage Shinyanga, Amina Yusuph alisema anachotaka kuona
ni kuboresha huduma za afya katika miji yote pamoja na upatikanaji wa
dawa.
Naye
Brayan Mshana alisema kama mwananchi asiyefungamana na upande wowote
anakubaliana na matokeo na kikubwa Dk Magufuli atekeleze ahadi
alizozitoa kwa wananchi.
CHANZO NA MWANANCHI.
Post a Comment