POLISI Mkoa wa Temeke, imewakamata vijana wawili wanaodaiwa kujifanya
waganga wanaotoa tiba kwa wanawake, ambayo masharti yake ni kushiriki
nao ngono bila kinga na kuacha nguo za ndani, ili zifanyiwe dawa zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo, alidai vijana hao Juma Hemedi
(32) na Abrahman Mulsin, wote wakazi wa Tandika, baada ya kushiriki
ngono na wagonjwa wao huwaambia waache nguo za ndani. Kamanda Kiondo
alidai baada ya kupata malalamiko, Jeshi la Polisi lianzisha msako na
kuwapekua waganga hao, ambapo walikutwa na nguo za ndani za kike 22,
ambazo alisema zitakuwa ushahidi wa kuingiliwa kimwili kwa wanawake hao.
Vitu vingine wanavyodaiwa kukutwa navyo ni pembe, tunguli, makopo ya
dawa na vibuyu. “Sheria iko wazi, inasema mganga anapofanya ngono kama
uganga anakuwa amebaka, na hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya
Adhabu 130 sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002,” alisema
Kamanda Kiondo.
Kwa mujibu wa madai ya Kamanda Kiondo, vijana hao wamekuwa wakijifanya
waganga wa tiba asili, husambaza vipeperushi sehemu mbalimbali za jiji
kutafuta wateja. Mbali na tiba hiyo ya kupata watoto, inayotolewa kwa
kushiriki ngono na mganga, Kamanda Kiondo alidai watuhumiwa hao wamekuwa
wakidai kutibu magonjwa mengine kama kisukari, vidonda vya tumbo, nguvu
za kiume, kukuza maumbile, kupata kazi, kufaulu mtihani, mvuto wa
biashara, kumilikishwa jini na kupewa pete ya bahati.
Katika tukio lingine, Polisi inamshikilia kijana mwingine mkazi wa
Tandika Devis Corner, Maalim Kimti Rita au kwa jina lingine, Joseph Rita
anayedaiwa kutapeli Sh milioni 11 akijidai kumfanyia dua mfanyabiashara
aweze kukuza biashara yake. Alidai kuna mfanyabiashara mwanamke ambaye
alitoa Sh milioni 11 kwa Maalim Rita, akidanganywa kuwa atafanyiwa
uganga ili afanikiwe katika biashara yake, lakini alipoona hakuna
alichopata, akaamua kutoa taarifa Polisi.
Kamanda Kiondo alisema jamii inapaswa kuelimishwa kuachana na mambo
hayo, kwa sababu tiba yake haipo kwa waganga wa jadi na kwamba hakuna
uhusiano kati ya kufaulu na kwenda kwa waganga isipokuwa bidii ya kazi.
“Watu wengi wamelalamikia matukio ya namna hiyo, sasa tumeamua kuweka
wazi kwa umma kwa kuwa watu wanateketea kwa kukosa elimu… watu wanauza
nyumba magari na mali zao, kwa ajili ya kupata fedha za kupeleka kwa
waganga wakiamini kuna tiba, huu ni utapeli vijana kama hawa hawawezi
kukupa utajiri wala mtoto,” alisema Kamanda Kiondo. Alisema waganga hao
wamepata vyeti vya kufanyia kazi hiyo ya uganga wa jadi, lakini
wanachofanya ni kinyume na kazi hiyo ambapo aliahidi vyeti vyao
kuchunguzwa, kuona wamevipataje na kuwasiliana na Wizara ya Maliasili na
Utalii, ili watambue pembe wanazotumia ni za mnyama gani.
Source: Jipange101.com
Post a Comment