Katibu wa Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Kilimanjaro
(UVCCM), Yasini Lema, ‘amefunguka’ kuhusu mchakato wa uchaguzi mkuu
uliopita namna ulivyokiathiri chama hicho na kukifanya kipoteze majimbo
ya uchaguzi ya Siha, Same Mashariki na Moshi Vijjini waliyokuwa
wakiyashikilia kwa zaidi ya miaka 15.
Lema amedai kuangushwa kwa mawaziri wawili wa serikali iliyopita, Aggrey
Mwanri aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Anne Kilango Malecela (Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi) na Dk. Cyril Chami, kulitokana na
ushawishi mkubwa wa aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.
“Chadema imefanikiwa kuchukua majimbo ya CCM kutokana na mkakati wa
Lowassa pamoja na kuhama kwake, kitu ambacho kilitengeneza mpasuko
ulioiua CCM na wagombea wake,” alisema.
Alidai kulitokea usaliti ndani ya CCM kwa madai kulikuwa na kundi ambalo
lilikuwa likiendelea kushiriki vikao vya ndani huku likikerwa na
kuondoka kwa Lowassa jambo ambalo lilisababisha chama hicho kushindwa
katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro. Aidha, akizungumzia mkakati wa
CCM kuyarejesha mikononi mwake majimbo ya Moshi Mjini na Rombo, Lema
alidai kuwa sababu ya kushindwa kwao ni kutokana na wagombea wa nafasi
za ubunge kupitia chama hicho kupora mamlaka ya viongozi wa wilaya.
“Wagombea ubunge katika majimbo haya mawili walikuwa na nguvu zaidi
katika chama, atakalolisema yeye na atakalopanga ndilo atakalolisimamia
lifanyike. Ukweli ni kwamba viongozi wa wilaya nao waliwaogopa, huku
kampeni zao zikikwepa kabisa kuwashirikisha viongozi wa chama ngazi za
matawi na kata” alisema Lema.
Alisema pamoja na kwamba CCM kilianzisha vikosi kazi maalum kwa ajili ya
kutafuta kura, lakini katika hali ya kushangaza wagombea wao wa ubunge
katika majimbo yote tisa ya Mkoa wa Kilimanjaro, walijiweka kando
kuwatumia viongozi wa matawi na ngazi ya kata.
Sababu nyingine ya kupoteza viti vingi vya udiwani alisema ni wagombea
wao kujiaminisha kwamba CCM ingewaletea fedha nyingi kwa ajili ya
kampeni huku wengine wakiamini wangesaidiwa na wagombea ubunge ambao
waliamini walikuwa na fedha nyingi kuwashinda wagombea wa vyama vya
upinzani.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment