Aliyekuwa
mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Edward Lowassa, ambaye pia alikuwa akiungwa mkono na vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), anatarajiwa kunguruma
jijini Arusha Jumamosi ambapo atatoa tamko kuhusu uchaguzi mkuu
uliopita.
Akizungumza
katika mkutano wa kampeni za ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless
Lema, anayetetea tena nafasi hiyo, alisema Lowassa atazungumza na
Watanzania Jumamosi kupitia wakazi wa Arusha.
Alisema
pamoja na kuja kumnadi yeye katika kinyang’anyiro cha ubunge, Lowassa
pia anatarajiwa kutoa tamko kuhusu uchaguzi mkuu uliopita na namna
alivyoibiwa kura za urais.
“Angetoa
tamko siku ile ya kwanza ya matokeo ya uchaguzi, tungeharibu nchi,”
alisema na kuongeza: “Lowassa alishinda kwa asilimia nyingi kuliko kura
alizopata Rais Dk. John Magufuli, aliyekuwa mgombea wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Alisema nchi imenusurika kutokana na busara za viongozi wa Ukawa kutotoa tamko lolote wakati huo.
“Atakuja Jumamosi, hivyo tusubiri tamko kuhusu hatua gani zinachukuliwa…tuwe na subira,” alisema.
Akizungumzia
uchaguzi wa ubunge unaotarajiwa kufanyika Desemba 13, mwaka huu jijini
hapa, Lema aliwataka wakazi wa jiji hili kutokata tamaa na matokeo ya
uchaguzi mkuu uliopita.
“Hatuna
namna yoyote ile kushindwa kuleta maendeleo jimboni hapa iwapo tumepata
madiwani 24 kati ya kata 25 zilizopo. “Kama tutashindwa kuleta
maendeleo hadi mwaka 2020 huku meya, naibu wake na wenyeviti wa kamati,
wote ni wa Chadema, basi mtupige chini na kuwachagua wengine.
Mapema
Mbunge Mteule wa Jimbo la Mbeya, Joseph Mbilinyi (Chadema), alisema
ingawa wakazi wa Arusha wana hasira kufuatia matokeo ya uchaguzi mkuu
uliopita, lakini hasira zao haziwezi kuzidi zile za wakazi wa Mbeya.
Alisema viongozi wao mara zote wametaka kutoa tamko kwa kuzungumza na wananchi, lakini CCM imekuwa ikikaba hadi penati.
Alisema
katika jimbo lake, wananchi wamewachagua madiwani 26 wa Chadema na
kuwaachia CCM kata tisa, hivyo watapata nafasi nzuri ya kujadili
maendeleo katika Baraza la Madiwani na siyo siasa kama ilivyokuwa awali.
Mbunge
wa Viti Maalum kutoka Kilimanjaro, Lucy Owenya, alisema Lema alifanya
kazi katika mazingira magumu ya halmashauri ambayo ilikuwa ikiongozwa na
madiwani wa CCM.
Alisema
kwa vile wakazi wa Arusha wamewachagua madiwani wa Chadema 24 kati ya
25, Lema sasa atafanya kazi nzuri ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Mbunge
Mteule wa Simanjiro, James Ole Millya (Chadema), alisema amefanya kitu
kimoja kikubwa cha kuondolewa bungeni mpiga kelele bungeni.
Alisema
wakifika bungeni, kitu cha kwanza ni kudai Tume Huru ya Uchaguzi, jambo
ambalo alisema bila kuwa na tume hiyo CCM itaendelea kuwaibia kura.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment