Kufuatia taarifa iliyotolewa na Ikulu Dar es Salaam, na pamoja na
jitihada za awali za Makamu wa Kwanza wa Rais na Mgombea Urais wa
Zanzibar kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kujaribu kuwasiliana na
Rais Jakaya Kikwete kwa njia ya simu, leo hii Maalim Seif amemuandikia
barua rasmi kumuomba wakutane ili kuzungumzia hali ya kisiasa ya
Zanzibar kufuatia uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad akiwa
na viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikristo katika kutafuta ufumbuzi wa
mkwamo wa kisiasa Zanzibar.
Kwa upande mwengine, kufuatia maelekezo ya Rais Kikwete, CUF imekubali
kufanya mawasiliano na wasaidizi wa Rais ili kupanga utaratibu wa
kukutana na Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
Jenerali Davis Mwamunyange, ili kuzungumzia hali ya usalama ya Zanzibar
kufuatia uchaguzi mkuu huo wa tarehe25 Oktoba, 2015.
Katika hatua nyengine, leo Maalim Seif Sharif Hamad alikutana na
viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikristo wa hapa Zanzibar kuzungumzia
suala zima la uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba na kuwaomba viongozi hao
kuingilia kati suala hili ili kuhakikisha nchi inabaki katika hali ya
amani na utulivu na pia kuhakikisha maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya
kupitia uchaguzi huo yanaheshimiwa.
Tunapenda kuwahakikishia kuwa tutachukua kila juhudi zilizomo kwenye
uwezo wetu katika kuupatia ufumbuzi mgogoro uliojitokeza na kufanya kazi
na kila aliye tayari kushirikiana na sisi katika kutunza amani ya nchi
yetu na kuilinda demokrasia yetu.
Chanzo: Zanzibaryetu
Post a Comment