Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imefuta
kesi ya kufanya mkusanyiko usio halali kwa lengo la kwenda
Ikulu iliyokuwa inamkabili mbunge mteule wa Jimbo la Kawe
(Chadema), Halima Mdee (35) na wenzake wanane, kwa
kuwaachia huru kisha polisi kuwatia mbaroni tena.
Kesi hiyo ilifutwa jana na Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda
akisema mahakama hiyo haioni haja ya kuendelea nayo kwa
sababu hakuna mashahidi wa kuithibitishia kama walitenda
kosa hilo.
Hakimu Kaluyenda alitoa uamuzi huo baada ya Wakili Mwandamizi wa Serikali, Mutalemwa
Kishenyi kudai kuwa kesi hiyo ilifikishwa jana kwa ajili ya kusikilizwa, lakini shahidi ambaye ni
Naibu Kamishna wa Polisi, Simon Siro hakufika mahakamani hapo kwa kuwa alikuwa amefiwa.
Hakimu
alisema kutokana na mashahidi wa upande wa mashtaka kushindwa
kuhudhuria mahakamani, anafuta kesi hiyo na kuwaachia huru washtakiwa
hao.
Alifafanua kuwa washtakiwa hao wameachiwa huru chini ya Kifungu cha 225 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Hata hivyo, alisema kifungu hicho kinaruhusu upande wa mashtaka kuwakamata washtakiwa hao
pale watakapoona inafaa na hata kuwashtaki.
Naye mdhamini wa Halima Mdee alidai kuwa mshtakiwa huyo, ameshindwa kufika mahakamani
hapo kwa sababu ni mgonjwa.
Alipotakiwa kuthibitisha madai hayo kwa kutoa cheti cha daktari, alidai hakukabidhiwa.
Kwa
upande mwingine, Wakili Kishenyo, alimuomba hakimu huyo kutoa hati ya
kuwakamata mshtakiwa wa tatu, Renina Peter maarufu kama Lufyagila, mkazi
wa Kinondoni Mkwajuni na wa
sita, Sophia F Angel (28), wa Mbezi Beach kwa kutofika mahakamani hapo
bila ya kutoa taarifa
yoyote.
Alidai ugonjwa na vifo ni vitu visivyozuilika na kuiomba mahakama hiyo iwape wiki mbili ili kesi
dhidi ya washtakiwa hao wawili iendelee kusikilizwa.
Baada ya Hakimu Kaluyenda kuwaachia huru washtakiwa hao, askari polisi waliwakamata tena
na kuwaweka chini ya ulinzi kisha kuwapeleka katika kituo cha polisi.
Kesi
hiyo pia ilikuwa inawakabili Rose Moshi (45), mkazi wa Kinondoni ‘B’,
Anna Linjewile (48)
wa Mbezi Luis, Mwanne Kassim (32) wa Pugu Kajiungeni, Edward Julius (25)
wa Msasani, Martha Mtiko (27) wa Mikocheni ‘A’ na Beuty Mmari (35) wa
Kinondoni Mkwajuni.Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Oktoba 4, 2014 katika
mtaa wa Ufipa, washtakiwa hao bila
halali walikiuka amri ya kutawanyika iliyotolewa na Mrakibu wa Polisi
(SP), Emmanuel Tillf kwa
niaba ya jeshi hilo.
Ilidaiwa
kuwa washtakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 124 cha
Sheria ya
Kanuni ya Adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002. Katika
shtaka la pili,
washtakiwa hao wanadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, katika eneo hilo, kwa
pamoja walifanya mkusanyiko usio halali kwa lengo la kutembea kwenda
Ofisi ya Rais, kinyume na kifungu cha 74
na 75 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, sura ya 16 iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2002.
Post a Comment